LATRA: Tunatamani tusahau ajali kupitia vidhibiti mwendo kila basi

14Jan 2021
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
LATRA: Tunatamani tusahau ajali kupitia vidhibiti mwendo kila basi
  • Kasi, mbwembwe njiani, uegeshaji ovyo

SHIRIKA la Afya Duniani (WHO), linasema watu 3,400 wanapoteza maisha kila siku duniani kupitia ajali za barabarani, huku dira ya ripoti yake ya usalama barabarani kuanzia 2011 hadi mwaka jana, iliangaza kufuta nusu ya ajali, majeruhi na vifo.

kuhusu yanayojiri barabarani na kelele za vidhibiti mwendo. PICHA: MTANDAO.

Ni tatizo linalogusa maisha ya watu hata kitaifa, mfano hai ikirejewa kauli za mwanzo za Inspekta Jenerali wa Polisi Mstaafu, Said Mwema, aliwahi kueleza hatua ya mafanikio kudhibiti uhalifu katika siku zake za mwanzo, lakini akikiri kutiwa ukakasi wa kusumbuliwa na usalama barabarani.

Kimsingi, usalama wa barabarani ni suala mtambuka lisiloishia mkononi mwa polisi pekee, bali linagusa mamlaka zingine za kiserikali na zisizo za kiserikali zinazosimamia usalama huo, kuanzia sheria hadi utendaji, abiria, madereva na watumia barabara.

WHO inaitaja ajali kuwa jambo linalowaacha pia waathirika katika ulemavu wa kudumu kimaisha na kuathiri mustakabali wa familia nyingi duniani, huku vifo hivyo vya ghafla vikiacha makovu ya kudumu kwa familia.

Inazitaja athari hizo ni kuwaacha majeruhi kila kona ya dunia na inaongeza mamilioni wanaosalia kuwa tegemezi wa kudumu katika baadhi ya mambo, kutokana na athari hizo.

Kinachofanywa na WHO ni sehemu ya kutimiza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s), mahususi Namba Tatu, linalohusu afya na ustawi wa watu kwa rika zote ifikapo 2030.

Ni lengo linalohusu ambalo katika mustakabali wake mpana, unaangukia kupunguza vifo vya mama wajawazito, pia watoto wanaozaliwa.

Kuna hatua mbalimbali ambazo serikali na wadau zimeshachukua katika tafsiri na lengo la ama kupunguza au kumalizika kabisa nchini.

Hapo inajumuisha ushuhuda kama vile kuweka mfumo wa kisatelaiti wa kufuatilia mwenendo wa magari barabarani uitwao ‘Vehicle Tracking System’ (VTS), ambao unaofanana na mifumo iliyopo kwenye magari.

VIDHIBITI MWENDO

Mkurugenzi wa Udhibiti Usafiri wa Barabara (LATRA), Johansen Kahatano, anasema hadi kufika mwishoni mwa mwaka jana, takribani mabasi 5,000 ya safari ndefu kivuka mikoa na mipaka ya nchi, yalifungiwa mfumo huo.

Kahatano anasema, licha ya kuendelea kuwapo matukio ya ajali barabarani, kwa kiasi kikubwa mfumo huo umepunguza ajali zilizosababisha vifo na majeruhi wengi nchini.

"Kufungwa mfumo huo kwenye baadhi ya mabasi, malalamiko ya abiria kuhusu madereva kuendesha vibaya yamepungua na hayajitokezi sana kama zamani," anasema Kahatano.

Pia, anafafanua kuwa ni mfumo unaorahisishia ufuatiliaji, kupata taarifa sahihi na za haraka, zitokanazo na mwenendo wa madereva kila kona ya nchi.

"Wito wangu ni kwa baadhi ya wamiliki wa mabasi wote wabadilike ili tusaidiane katika vita hii ya kudhibiti ajali, wahakikishe madereva hawachezei mfumo huo katika mabasi yao," anaeleza.

Anafafanua mfumo huo unavyofanya kazi, kwamba inarekodi spidi kuanzia dereva atakavyoendesha, lakini mwendokasi unapofika kasi ya kilomita 85 kwa saa, kengele hulia kumtahadharisha mwendeshaji.

"Mfumo huu unaruhusu ufuatiliaji wa basi wakati huo huo likiwa safarini, kwani ofisa wa LATRA, mmiliki au Jeshi la Polisi, wanaweza kukaa ofisini na kufuatilia kila basi mwenendo wake na kuchukua hatua kwa wakati," anasema.

Kahatano, anafafanua kuwa, mfumo haulizuii gari kuvuka spidi iliyowekwa, lakini unahifadhi rekodi za kasi barabarani, mahali na muda anaosimama njiani.

WANAOTETEA ABIRIA

Hassan Mchanjama, Mwenyekiti wa Chama cha Kutetea Abiria Tanzania (CHAKUA), anaeleza kuunga mkono juhudi zinazofanywa na wadau wa usafiri kusaka usalama wa abiria.

"Kama wadau wa usafiri, tunaunga mkono juhudi za kuhakikisha abiria anasafiri na kufika salama kule aendako na pia apate huduma sahihi, hivyo suala la VTS na tiketi za kielektroniki ni vya muhimu," anasema Mchanjama.

Anafafanua: "Tunaamini kwamba kuna mafanikio kwenye mfumo huo, ingawa zipo changamoto mbalimbali hasa zinazotokana na baadhi ya wamiliki wa mabasi kutotumia au kutofuatilia madereva wao, ili wasichezee mfumo huo katika mabasi yao."

Kuhusu ukatishaji tiketi za mabasi kwa njia za kielektroniki, anakiri kukubaliana na mfumo huo mpya, jambo wanaoamini itawaondolea abiria usumbufu wa walio nao kila mara.

"Hatua hii ya kuwapo tiketi hizo itaondoa wapigadebe vituoni, pia itakomesha wajanja wachache ambao wamekuwa wakipandishia abiria nauli kwa kujali maslahi yao zaidi," anasema.

Mwenyekiti huyo anasema, chama chao kimekuwa kikitoa elimu kwa abiria kujua haki zao, kuanzia usalama katika safari na hata kuepuka kuibiwa mali au kuzindishiwa nauli wanapotaka kukata tiketi.

Habari Kubwa