Licha ya corona Makumbusho Kidijitali yang’ara D’ Salaam

02Jun 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Licha ya corona Makumbusho Kidijitali yang’ara D’ Salaam

MAADHIMISHO ya Siku ya Makumbusho Duniani yalianzishwa na Baraza la Makumbusho Duniani (International Council of Museums – ICOM) mwaka 1977 kwa lengo la kujenga uelewa kwa jamii kwamba taasisi hiyo ina muhimu kipekee.

Biashara ya utumwa ni moja ya mambo yaliyoidhalilisha Afrika kwenye karne ya 17, vielelezo vyake vipo Makumbusho ya Taifa . PICHA MTANDAO.

Ndilo eneo ambalo urithi wa asili na utamaduni unahifadhiwa na jamii kubadilishana utamaduni hai kwa mazingira ya sasa.

Siku hiyo ya makumbusho ni muhimu kwani ina nguvu ya kuleta utengamano na jamii na kujenga umoja wa kitaifa, uzalendo na kufanya watu kuelewana zaidi.

Aidha, huleta kuthamini na kuhifadhi urithi wa asili na kiutamaduni kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.

Siku hiyo huadhimishwa kila mwaka Mei 18, ambapo makumbusho zote duniani hufanya shughuli mbalimbali zenye lengo la kupeleka elimu kuhusu umuhimu wa makumbusho kwa wananchi.

Sherehe hizo huambatana na maandamano na shamra shamra za kila namna. Katika siku hiyo makumbusho zote duniani zinakuwa wazi kwa wananchi kuingia na kutoka bila kulipia gharama za kiingilio ili kujionea kazi mbalimbali.

Mirindimo ya maadhimisho hayo kwa mwaka 2020 nchini na duniani kwa ujumla imekuwa tofauti kwa sababu ya janga la ugonjwa wa korona ulioikumba duniani yote.

Kama moja ya njia ya kujikinga na maradhi huo mikusanyiko hairuhusiwi na jamii inahimizwa kuwa na tahadhari ili kuepuka corona.

Kaulimbiu ya maadhimisho mwaka huu ni Makumbusho kwa Usawa, Anuai na Ushirikishwaji (Museum for Equality: Diversity and Inclusion).

Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Makumbusho Duniani, baadhi ya nchi zimefunga shughuli za kimakumbusho kwa muda ili kupisha janga la corona.

Kwa upande mwingine, Tanzania inaungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha siku hiyo kwa kutekeleza maelekezo ya serikali na Shirika la Afya Duniani (WHO) katika kupambana na ugonjwa wa corona kupitia onyesho la kigitali liitwalo “Makumbusho Salama”.

Katika uzinduzi uliofanyika siku hiyo inaonyesha ni jinsi gani Makumbusho ya Taifa yamejizatiti katika kudhihirisha kuwa kila anayeyatembelea anakuwa salama.

Sambamba na huduma kwa wageni zinazoendelea kutolewa kwa tahadhari, Makumbusho ya Taifa, imeendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi hususani kufanya utafiti, kukusanya mikusanyo, kuhifadhi, kuelimisha jamii kwa njia ya maonyesho, semina na programu za kielimu juu ya masuala mbalimbali kuhusu urithi wa asili na utamaduni wa taifa kwa lengo la kurithisha, kutoa elimu na kuburudisha.

Akizungumza katika uzinduzi wa onyesho la “Makumbusho Salama”, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dk. Noel Lwoga, anasema kuwa japokuwa kuna ugonjwa wa corona makumbusho zote zinaendelea kufanyakazi lakini tahadhari kubwa imewekwa ili kuwakinga watumishi wa makumbusho hizo pamoja na wageni wanaozitembelea.

“Tumechukua kila tahadhari kulingana na maelekezo ya Wizara ya Afya kuhakikisha kuwa kila mgeni anayetembelea anaingia akiwa salama na anatoka akiwa salama pia”, anasema Dk. Lwoga.

Kulingana na onyesho hilo hakuna mgeni anayeruhusiwa kuingia makumbusho bila kuwa na barakoa na akiingia tu anapimwa joto ili kujua hali ya afya yake.

Anatakiwa kunawa mikono na sabuni na maji yanayotiririka au kutumia vitakasa mikono huduma ambazo zipo katika kila mlango wa kuingilia na kutoka makumbusho.

Lengo la kutengeneza onyesho la kidigitali ni kuhakikisha ujumbe unawafikia watu wote si wale tu wanaoweza kutembelea makumbusho zetu bali hata wale walio nje ya nchi ili wajue Makumbusho ni salama, anasema Ezekiel Chance, Mkuu wa Idara ya Programu, Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni, Dar es Salaam.

Anasema wananchi wanaweza kutembelea makumbusho zote bila kuwa na wasiwasi kwa sababu taasisi imechukua kila hatua stahiki kuhakikisha kuwa wanaotembelea wanakuwa salama.

Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wa Makumbusho ya Taifa, Lusekelo Kaisi, anasema kuwa pamoja na maonyesho na programu za kielimu taasisi ya Makumbusho ya Taifa inaendelea kuimarisha mifumo yake ya mawasiliano ya ikiwemo tovuti na mitandao ya kijamii ili kuwawezesha wananchi na jamii kwa ujumla kupata taarifa mbalimbali za kimakumbusho kwa urahisi zaidi.

“Kupitia njia hizi za mawasiliano jamii inaweza kupata taarifa, machapisho na maonyesho kwa urahisi bila wao kufika makumbusho,” anasema Kaisi.

TIBA YA NYUNGU

Kama sehemu ya maadhimisho hayo, Kijiji cha Makumbusho kilichoko Kijitonyama jijini Dar es Salaam kiliandaa onyesho la mila na tiba asili ambapo wanajamii kutoka kabila la Wamakonde na Wafipa walionyesha jinsi ambavyo tiba za asili zilitumika kutibu magonjwa mbalimbali.

Kazi hiyo iliyokuwa mubashara katika mitandao ya kijamii ya instagram, facebook na youtube lilionyesha majani yanayotumika katika kujifukiza na jinsi ya kujifukiza kwa magonjwa mbalimbali yakiwamo mafua makali, kichwa na tumbo.

Mkurugenzi wa Kijiji cha Makumbusho Dk. Gwakisa Kamatula, anasema Makumbusho ina hazina kubwa ya urithi wa utamaduni.

Anaeleza kuwa ukiachilia mbali uhifadhi wa nyumba za asili za jamii mbalimbali za Tanzania, Kijiji cha Makumbusho kinahifadhi msitu wa asili wenye ukubwa wa takribani heka tano wenye miti na mimea mbalimbali ambayo inaweza kutumika katika tiba asili.

“Tupo hapa kwa lengo la kutoa elimu kwa jamii juu ya matumizi mazuri ya tiba asili hususan suala zima la kujifukiza” anasema Dk Kamatula.

Mary Mangazini kutoka kabila la Wafipa anasema katika jamii yao kujifukiza siyo jambo geni kwa sababu kunatumika sana kwa magonjwa mbalimbali ambapo majani ya mwarubaini, tangawizi pori, mpera, mkaratusi hutumika.

Anasema majani hayo huchemshwa kwa pamoja kwenye chungu kwa muda wa dakika 20. Maji hayo huipuliwa na kuwekwa pembeni kisha mgonjwa hufunikwa na nguo nzito (shuka au blanketi) kulingana na uzito wa mgonjwa.

“Akiwa mnene anatakiwa atumie nguo nzito zaidi ukilinganisha na mtu mwembamba” anasema Mangazini.

Anasema mgonjwa anatakiwa kujifukiza kwa muda wa dakika tano mpaka 10 kutegemeana na ukubwa wa tatizo lake.
“Tiba hii ni rahisi sana na mara baada ya kujifukiza mgonjwa hupata nafuu au kupona kabisa,” anaeleza Mangazini.

KUOMBEA TAIFA

Nayo Makumbusho ya Majimaji Songea ilitumia maadhimisho hayo kuombea nchi dhidi ya ugonjwa wa corona.

Baraza la Kimila la Songea kwa kushirikiana na wanajamii walifika katika kaburi la halaiki la mashujaa wa vita vya Majimaji kuiombea nchi dhidi ya janga hilo.

UTALII NDEGE

Makumbusho ya Elimu Viumbe Arusha walitumia maadhimisho hayo kuzindua programu ya ushirikishwaji wa vijana kwenye makumbusho hususani kupitia vikundi vya vijana vya utazamaji na utalii wa ndege katika mkoa wa Arusha.

Kaimu Mkurugenzi wa Makumbusho ya Elimu Viumbe Christine Ngereza, anasema kuwa vijana ni kundi muhimu katika suala zima la uhifadhi, hivyo, ni muhimu washirikishwe ili kujenga uelewa na uzalendo.

“Kijana akielewa inakuwa rahisi katika kuendeleza uhifadhi wa mazingira na maliasili ya taifa, anasema Ngereza.

Habari Kubwa