Likizo ya corona ilivyoliza watoto

30Jun 2020
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Likizo ya corona ilivyoliza watoto

WANAFUNZI wote Bara na Visiwani wameanza masomo jana baada ya kupumzika kwa miezi mitatu na nusu. Kwa wengi wawe wazazi, walezi, watoto na hata walimu kilikuwa kipindi kigumu.

Mzuri Issa Mkurugenzi wa Tamwa Zanzibar. PICHA MTANDAO

Leo dunia inapokabiliwa na janga la corona na watoto kusimama kimasomo licha ya kwamba hapa nchini wamerudi shuleni, watoto waliotakiwa kulindwa wakiwa wametulia nyumbani kuanzia Machi hadi Juni 28, wapo mafisadi wa maadili waliotumia mwanya huo kuwadhalilisha.

Tangu Machi mwaka huu liliporipotiwa janga la corona na shule kufungwa watoto 10 wamedhalilishwa kijinsia Zanzibar na hizo ni rekodi za Chama cha Wanahabari Wanawake Zanzibar (Tamwa), ambao waliwapokea waathirika wakiomba msaada..

Licha ya takwimu hizo za kipindi hicho kifupi pia watoto 1,049 wamedhalilishwa Unguja na Pemba kwa miaka miwili kuanzia 2017 hadi 2019, ambao pia waliripoti Tamwa kwa kipindi hicho..

Mzuri Issa ,Mkurugenzi wa Chama cha Tamwa Zanzibar, anaeleza kusikitishwa na ongezeko la vitendo vya ubakaji watoto katika likizo ya corona, ambavyo baadhi ya watuhumiwa ni watoto wenyewe.

Anasema hiyo ni sehemu ndogo ya taarifa zilizofikishwa Tamwa na huenda hali ni mbaya zaidi, anataka jamii, wazazi, walezi na viongozi wa dini na vyombo vya sheria kusaidia kurekebisha tabia kwa watoto wa rika la miaka 16 ambao baadhi yao wanatuhumiwa kufanya makosa hayo.

Anaiomba serikali kuweka mipango madhubuti ya kubadilisha tabia ya vijana wa kiume ili kuruhusu wanawake na watoto kuishi kwa amani na kufikia malengo ya kimaisha.

Dokta Mzuri anaziomba mamlaka zinazohusika kuzishughulikia kesi hizo kwa haraka na kutoa adhabu zinazostahiki.

KWANINI UNYANYASAJI

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Zanzibar Dk.Sikujua Omar Hamdan, akizungumzia sababu za kuendelea vitendo vya watoto kudhalilishwa ikiwamo wazazi kumaliza kesi hizo mitaani na kushindwa kufika polisi na mahakamani anasema:

“Hufanya hivyo wakiwa na hofu ya kuona kwamba hawatasaidiwa, pamoja na kujua sheria.Wanabakia nyumbani na watoto wao. Hii inaonekana kwamba bado kuna mwamko mdogo wa kwenda kuripoti kesi polisi na mahakamani”, anasema.

Hamdan anasema ushahidi bado ni tatizo na bado watu hawahudhurii mahakamani kutoa ushahidi jambo ambalo linapelekea kesi hizo kukosa hukumu.

Anakumbusha kuwa hakuna utaratibu mzuri wa kurikodi kesi hizo mahakamani na tafsiri ya sheria si makini kutokana na adhabu zinazotolewa zinaonekana kuwa hazistahiki.

“Kesi zilizoropitiwa mahakamani ni nyingi hivyo wadau wanatakiwa kukaa pamoja kwa ajili ya kuleta ufanisi vipi kesi za udhalilishaji zitafanyiwa mapitio”,anashauri mhadhiri huyo.

Anaeleza kuwa kesi za ubakaji ndizo zinazoripotiwa kwa wingi mahakamani lakini hukumu zake haziridhishi kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo mahakama kukosa ushirikiano wa jamii hasa kutoa ushahidi.

RUSHWA INAKWAMISHA

Fatma Juma Mahmoud, Mkuu wa Dawati la Jinsia Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, anasema kuwa jamii haijawa tayari kutoa ushahidi mahamakani na pia imetawaliwa na rushwa hali ambayo imepelekea kesi hizo kukosa hukumu.

“Lengo ni kuvitokomeza vitendo vya udhalilishaji hivyo cha muhimu ni utayari wa jami kutoa ushahidi mahakamani ili kuwasaidia watoto waliodhalilishwa”,anasema.

Ofisa wa Wanawake na Watoto wa Wizara ya Uwezeshaji Ustawi wa Jamii Maendeleo ya Wazee, Wanawake na Watoto, Muhamed Jabir, anasema kuna uwezekano kuwa majukumu ya baadhi ya wazazi yamepungua katika kipindi hiki cha corona hali ambayo imepelekea ongezeko la udhalilishaji.

Watoto wamepewa uhuru wa kupitiliza na kipindi hiki ambacho hawaendi shuleni wanazurura mitaani huku wazazi na walezi wakikwepa majukumu yao.

“Watoto wanahitaji uwangalizi mkubwa muda wote lakini licha ya shule kufungwa bado watoto wanazurura na kuwapa wadhalilishaji huitumia nafasi hiyo, “ anaonya.

Cha kuzingatiwa ni kauli mbiu ya mwaka huu katika Siku ya Mtoto wa Afrika ni “upatikanaji wa mifumo ya haki iliyo rafiki kwa watoto wa Afrika”.

Mwanaidi Ali Said , mratibu wa mradi wa kuimarisha familia ya kijiji cha kulelea watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu (SOS) anasema katika kukumbuka vifo vya watoto hao wa Afrika wanaharakati wanatafakari na kuchukua hatua namna gani ya kushughulikia changamoto za watoto zikiwamo za elimu na haki nyingine.

Anasema siku hiyo hutumika kama ni sehemu ya kufanya ushawishi na utetezi wa kuimarisha uelewa wa mkataba wa Afrika kuhusu haki za watoto.

“Sisi wanaharakati tumeona ni muhimu kuangalia upatikanaji wa elimu kwa watoto katika kipindi hiki cha corona ikizingatiwa kuwa hivi sasa ni muda wa miezi mitatu shule zimefungwa kutokana na corona,” anasema.

Anaeleza kuwa kutokana na corona haki ya elimu kwa watoto imekosekana na baada ya ugonjwa huo kumeibuka mifumo mbalimbali ya kupata masomo ikiwamo ya kimtandao ambayo mengine si rafiki kwa watoto na imeathiri haki za watoto na maendeleo ya elimu.

Anasema kuna hatari zaidi ya baadhi ya watoto kutorudi tena shuleni baada ya kufunguliwa hasa watoto wanaoishi katika mazingira magumu na watoto wengine kurudi nyuma kielimu.

ATHARI KIMAZINGIRA

Mkurugenzi wa taasisi ya Vijana (Zanzibar Youth Foram) Maulid Suleiman, anasema njia zozote zinazotumika ambazo hazijazoeleka kusoma na kufundisha zitakuwa si muafaka katika kutoa elimu.

Anaona kuwa utoaji wa elimu unategemewa kufanyika nyumbani unaonekana kuwa si muafaka kwa sababu sehemu ya kuwafundisha watoto masuala ya kitaalama.

“Licha ya kuwa kipindi hiki cha corona baadhi ya shule zimewaandalia wanafunzi masomo wakiwa nyumbani sio shule zote waliofanya hivyo,”anasema.

Aidha, anasema Wizara ya Elimu imeweka utaratibu wakutoa elimu kupitia vyombo vya habari lakini jamii haikuwa na muamko huo hivyo kiwango cha elimu miongoni mwa watoto kimeporomoka.

Mkurugenzi huyo anawataka wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wao hivyo ni vyema kuwatayarisha na kuweka mazingira ya kufikia azma hiyo.

‘Hivi sasa tumepata nafuu na maradhi yamepungua hivyo tunaimani kuwa shule zinavyofunguliwa watoto watapata elimu kama ilivyokusudiwa,”anasema.

LIKIZO YA CORONA

Baadhi ya wazazi waliozungumza na gazeti hili wanasema hivi sasa ufahamu wa watoto katika elimu umepungua na wameelekeza ufahamu wao katika michezo mbalimbali ikiwamo kuangalia ‘game’ kwenye simu na kompyuta, gololi, mpira wa miguu na rede kwa wasichana.

Safia Aboud ni mzazi wa watoto wawili, mkazi wa Unguja, anasema anawahimiza watoto wake kusoma lakini ufahamu wao umepungua.

Akizungumzia Wizara ya Elimu kuweka utaratibu wa kufundisha kwenye runinga , anaukosoa kuwa haujasaidia kwa sababu baadhi ya watoto hawana uelewa na pia hawakuandaliwa kujifunza kupitia TV na redio.

Hata hivyo, anaona kuwa hakuna kilichoharibika na kwamba tathmini ifanyike kufahamu mafanikio na changamoto za likizo ya corona.

Habari Kubwa