Lissu amedhalilisha wapinzani Bungeni

07Feb 2016
Nipashe Jumapili
Lissu amedhalilisha wapinzani Bungeni

Mnadhimu wa kambi ya upinzani Bungeni, Tundu Lissu alidai kuwa kutokana na Spika wa Bunge Job Ndugai kuteua “kiholela” wajumbe wa kamati, wabunge wa upinzani hawatashiriki uchaguzi wa kamati mbili ambazo zinapaswa kuongozwa na kambi ya upinzani.

Lissu alisema kwenye kamati hizo za hesabu za serikali (PAC) na hesabu za mashirika ya Umma (LAAC), Spika ameteua wabunge wa upinzani ambao hawana uwezo mkubwa katika kutekeleza majukumu hayo.
Alisema “hili bunge litakuwa la vichekesho, maana unasema kamati za usimamizi wa fedha za umma zitaongozwa na wapinzani halafu unawachagua nani aongoze hizo kamati, hatushiriki uchaguzi acha waendelee”.
Kauli yake hii ilinishtua na kuniacha hoi. Sikuamini na sijaamini kama ndiye yule Lissu anayefahamika kwa kujenga hoja zenye mantiki bungeni, eti ndiye aliyetamka maneno hayo ya kushangaza.
Siamini na nitaendelea kutoamini kama Lissu ambaye ni Mwanasheria kitaaluma na anayejua taratibu na sifa za mtu kustahili kuchaguliwa kuwa mbunge, angethubutu kusema wabunge wenzake hawana uwezo. Eti spika hawezi kutuchagulia viongozi dhaifu.
Kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 67 imeweka bayana sifa za mtu yeyote kustahili kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa mbunge kwamba:
Ni raia wa Jamhuri ya Muungano aliyetimiza umri wa miaka ishirini na moja (21) na ambaye anajua kusoma na kuandika katika Kiswahili au Kiingereza.
Ni mwanachama na ni mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa, pia katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya uchaguzi hakuwahi kutiwa hatiani katika mahakama yoyote kwa kosa lolote la kukwepa kulipa kodi yeyote ya serikali.
Maelezo hayo hapo juu, ndiyo hasa sifa za Mbunge. Sijui sifa za ziada za kutokuwa na uwezo wa kuteuliwa kwenye kamati za kudumu zimeelezwa wapi?
Kwa msisizo Lissu aliendelea kusema; “sisi tunataka mwenyekiti imara. Spika hawezi kutuchagulia viongozi dhaifu... hizi kamati haziwezi kuongozwa na Wabunge dhaifu”.
Kwa muono wake Lissu hatambui kanuni zinazompa haki mbunge yeyote kuteuliwa katika kamati za kudumu. Ajuavyo yeye, kuna kamati nyeti ambazo siyo sahihi spika kuwateua wabunge bila ridhaa yake.
Ni vema Lissu angekuwa muwazi na kutamka hadharani kuwa Mbunge fulani wa jimbo fulani hafai kuwa kwenye kamati ya PAC au LAAC.
Kwa ushauri wangu, angetumia busara kama mnadhimu wa kamati ya upinzani kukaa na wabunge wa upinzani kujadili hoja hiyo, kisha wangewaomba baadhi ya wabunge miongoni mwao wapishane na wabunge wenzao. Wabunge hao wangeridhia wenyewe kuwaachia wale wanaohitajika ambao wana uwezo kulingana na muono wa Lissu.
Sipendi kumung’unya maneno, alichokifanya Lissu ni aibu na udhalilishaji kwa wabunge wenzake. Kikubwa awaombe radhi kwani kila mbunge alichaguliwa na wapiga kura kutoka jimboni kwake wakiamini anafaa kuwawakilisha popote pale.
Siyo busara kuwadharau wabunge wengine eti kwasababu tu yeye ana taaluma ya sheria. Nijuavyo, ndani ya Bunge letu kuna wasomi zaidi ya Lissu wenye taaluma tofauti tofauti. Wako waheshimiwa maprofesa, madaktari (PHD’s), uzamili (Masters), lakini hawavumi.
Kwa ushuhuda huo, Lissu ameanika wazi udhaifu wa wabunge wa kambi ya upinzani kwasababu mara kadhaa tumeshuhudia wakitolewa nje ya Bunge.
Watanzania waliokuwa wakishutumu utaratibu wa wabunge wa upinzani kususia Bunge na kutoka nje sasa wameanza kuona ukweli wa udhaifu walionao kulingana na ushahidi wa Lissu.
Kwa mujibu wa kanuni za bunge ibara ya 50 (2), mbunge anapozungumza Bungeni, atawajibika kuwa na uhakika kwamba maelezo anayotoa ni sahihi, na siyo mambo ya kubuni au ya kubahatisha tu na kwamba; Spika au mbunge mwingine yeyote aweza kumdai mbunge huyo anayesema atoe uthibitisho wa usemaji wake unaohusika.
Ni aibu Lissu kuwaita wabunge wenzake viongozi dhaifu na hawafai kuongoza.

Mob: 0713 399 004/0767 399 004
Email: _HYPERLINK "mailto:[email protected]"[email protected].com_

Habari Kubwa