Lukuvi aanika ilikoegemea vita visivyoisha wakulima vs wafugaji

12Jan 2017
Elizaberth Zaya
Nipashe
Lukuvi aanika ilikoegemea vita visivyoisha wakulima vs wafugaji

MIGOGORO ya ardhi nchini bado ni tatizo kubwa.

Kwa kipindi kirefu imeendelea kusikika katika maeneo tofauti nchini na wakati mwingine kusababisha baadhi ya wananchi ama kuuawa au kuumizwa vibaya na kuachwa walemavu.

Miongoni mwa mikoa ambayo imekuwa ikiathiriwa na migogoro hiyo ni Morogoro, wakulima wakipambana na wafugaji.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, anasema pamoja na Tanzania kuwa na ardhi yenye rutuba na hali nzuri ya hewa, bado kuna changamoto ya migogoro ya ardhi.

Lukuvi anasema nchi bado ina ardhi ndogo iliyopimwa, hali inayochangia migogoro katika umiliki wake.

Anasema changamoto hiyo inaondoa tija na kuchangia umasikini katika mazingira ya teknolojia ya uzalishaji, mdogo, hususani katika sekta ya kilimo na viwanda.

WAKULIMA VS WAFUGAJI

Kwa mujibu wa Lukuvi, migogoro kati ya wakulima na wafugaji inasababishwa na mwingiliano wa matumizi ya ardhi kati ya makundi hayo ambayo mwisho wake huzaa vurugu.

Anasema kuna wakati wachungaji wa ng`ombe wanalazimika kuingiza mifugo yao mashambani, vivyo hivyo wakulima nao wanaingia kwenye maeneo ya wafugaji, kwa ajili ya kuongeza mashamba, ili wavune zaidi.

“Migogoro hii hutokana na vijiji kukosa mipango ya matumizi ya ardhi, inayoweza kuainisha maeneo kwa ajili ya wafugaji na wakulima na huduma nyinginezo,” anasema Lukuvi.

WAKULIMA NA WAWEKEZAJI

Anataja migogoro mingine ni kati ya wanakijiji na wawekezaji na kwamba baadhi ya migogoro inayohusu makundi hayo, hutokana na wanakijiji kukalia ardhi yenye hati milki au kutoshirikishwa kwa wananchi, pale ardhi inapotolewa kwa ajili ya uwekezaji.

Waziri huyo anarejea Sheria ya Ardhi ya Vijiji Namba 5 ya mwaka 1999, kuhusu utolewaji wa ardhi ya wananchi kwa wawekezaji.

KAMISHNA WA ARDHI

Kaimu Kamishna Msaidizi wa Ardhi, Christian Mwalugaja, anasema ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo katika utoaji ardhi ya kijiji, nayo inachangia migogoro hiyo.

Anatoa mfano wa kanuni za ardhi ya vijiji za mwaka 2002, zinazoainisha idhini ya viwango vya juu vya kumiliki ardhi.

Mwalugaja anasema, Halmashauri ya Kijiji inaruhusiwa kutoa ardhi si zaidi ya hekta 20, ambayo ni sawa na ekari 50.

Kamishna huyo anasema kwamba kunapotokea ombi linalozidi hekta kati ya 21 na 50, Halmashauri ya Kijiji inatakiwa kuwasilisha maombi kwa Kamishna wa Ardhi.

Anasema vijiji vingi, hutoa ardhi bila ya kuzingatia sheria hiyo, kitendo ambacho ni kosa lenye kawaida ya kuzua migogoro hiyo.

Kuhusu migogoro ya mipaka kati ya watu, vikundi na mamlaka mbalimbali, Mwalugaja anasema imekuwa ikijitokeza zaidi kati ya majirani binafsi, vijiji, wilaya na mkoa, jambo linalochangia msuguano wa mipaka.

UVAMIZI WA MASHAMBA

Mwalugaja anasema eneo la mabishano zaidi liko katika matukio kama vile ya kutolewa au kuhamishwa kwa alama za mipaka kwa bahati mbaya au makusudi, ikiwamo kukosekana kumbukumbu ya pande zenye mgogoro.

Uvamizi wa mashamba na viwanja, nayo imekuwa vyanzo vya migogoro hiyo, hasa baadhi ya wananchi wanapoamua kuvamia mashamba yaliyopimwa kwa muda mrefu na yameachwa bila ya kuendelezwa.

“Mmiliki wa shamba anapotaka kuendeleza eneo lake na kuwakuta wananchi wamevamia, inakuwa vigumu kuwatoa, kwa sababu tayari wameishi kwa muda mrefu.

“Kutokana na hali hiyo, mgogoro mkubwa baina ya pande hizo hujitokeza, hasa pale wananchi wanapokuwa tayari wamefanya mashamba hayo makazi ya muda mrefu,” anafafanua Mwalugaja.

UWEKEZAJI,HAZINA
NA FIDIA

Kuhusu migogoro ya wananchi kutoridhishwa na fidia wakati wa serikali kutwaa ardhi, Mwalugaja anasema watu wengi wanalalamika kuwa viwango vya fidia ni vidogo na haviendani na hali halisi ya soko.

Anasema katika hali hiyo, hutokea mgogoro na wakati mwingine ama kukwamisha au kuchelewesha utekelezaji wa mradi uliokusudiwa.

Mwalugaja anataja suluhisho kuwa serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo na Makazi, hivi sasa ipo katika mchakato wa kuanzisha Hazina ya Ardhi(Land Bank), itakayotumika kuwezesha uwekezaji kwenye ardhi nchini.

Anasema uanzishwaji wa Hazina hiyo, utasaidia kupunguza migogoro ya ardhi, pasipo kuathiri ardhi za vijiji.

Anasema tayari wizara yake imeanzisha kitengo mahsusi cha uwekezaji katika Ofisi ya Kamishna wa Ardhi.

Jingine linalotajwa na Mwalugaja kama chanzo cha mgogoro wa ardhi, ni ukosefu wa wataalamu, vitendea kazi na bajeti ndogo inayotengwa kuhudumia sekta hiyo.

Mwalugaja anataja changamoto nyingine ni kuwepo makundi ya watumiaji ardhi wanaogombana na hususan kwenye mipaka ya vijiji, wilaya na mkoa.

MWAROBAINI

Mwalugaja anaeleza imani yake kuwa mwarobaini utakaosaidia kupunguza migogoro hiyo ni kupima ardhi na kuimilikisha kuwa mali binafsi, pia huduma za umma kama shule na matumizi mengine isiwe na mtu wa kuivamia.

Mwalugaja anasema wizara inaandaa mipango ya matumizi ya ardhi katika ngazi zote za, ili kuimilikisha kisheria na wakati huohuo, kuweka miundombinu ya msingi.

Mwalugaja anataja jitihada zinazofanywa na serikali hivi sasa ni kutoa hati milki za kimila kwa wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi mkoani Morogoro, kupitia programu yake ya miaka mitatu ya kuwezesha umiliki wa ardhi.

Anasema, sababu ya kuanzisha programu hiyo kwa mkoa wa Morogoro sasa, ni kutokana na kuwepo migogoro mingi, ikilinganishwa na mikoa mingine.

Habari Kubwa