Maabara zinavyogeuzwa madarasa kuokoa jahazi

12Jan 2021
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Maabara zinavyogeuzwa madarasa kuokoa jahazi
  • *Hakuna kusubiri awamu ya 2

WAKATI shule zimefunguliwa kuanza mwaka mpya wa masomo jana, wanafunzi 155 wa kidato cha kwanza katika Halmashauri ya Musoma mkoani Mara, waliokuwa wasubiri kukamilika ujenzi wa madarasa, wako madarasani wakifurahia masomo ndani ya vyumba vya maabara.

Moja ya madarasa ya Shule ya Sekondari ya Seka, ambayo inatarajiwa kuanza kuchukua wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka huu. PICHA: MPIGAPICHA WETU

Kwa nini imekuwa hivyo? Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk. Vincent Anney, anasema, hakuna haja ya kuwa na maabara tupu, wakati ni darasa linaloweza kutumiwa na watoto badala ya kubakia nyumbani wakisubiri awamu ya pili, jambo linaloweza kukwamisha mipango ya kishule.

“Lengo ni kutaka wasiwapo wanafunzi watakaokaa nyumbani kusubiri awamu ya pili, tunataka wote waanze masomo kwa pamoja.” Anasema na kuongeza kuwa watasomea kwenye maabara wakisubiri ujenzi wa madarasa kukamilika.

"Kwa pamoja tumefikia hatua hiyo kwa kuwa kuna umuhimu wa wanafunzi kuanza masomo kwa pamoja badala ya kuwaacha wapishane huku wote wakiwa ni wa kidato kimoja," anasema Dk. Anney katika mahojiano na Nipashe.

Wilaya ya Musoma ina halmashauri mbili ikiwamo manispaa na kwamba kwa upande wa Halmashauri ya Musoma yenye Jimbo la Musoma Vijijini kuna sekondari za kata 20.

"Vilevile kuna tano zinazoendelea kujengwa ili zianze kuchukua wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka huu zikiwamo za Seka iliyopo Kata ya Nyamrandirira na Kigera kwa ajili ya wakazi wa kata ya Nyakatende," anaasema.

Mkuu huyo wilaya anazitaja nyingine kuwa ni Nyasaungu iliyoko Ifulifu, Bukwaya ya Kata ya Nyegina na Ifulifu na kwamba ujenzi wake unakwenda kwa kasi.

IDADI YA WALIOCHAGULIWA

Jumla ya wanafunzi 4,089 walichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza, katika sekondari za Halmashauri ya Musoma, lakini 155 kati yao walitakiwa kusubiri awamu ya pili ya kuanza masomo, kwa mujibu wa maelezo yake.

"Lakini tumetafakari na kuona hakuna mwanafunzi kubaki nyumbani, badala yake wasome katika majengo ya mabara kwa muda wa wiki mbili kisha waende kwenye madarasa yanayotarajiwa kukamilika wakati kuliko kusubiri nyumbani," anasema.

Wananchi kwa kushirikiana na serikali, wamefanya kazi kubwa hasa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa maktaba, maabara, nyumba za walimu, madarasa na vyoo, anasema mkuu wa wilaya.

"Kazi hiyo si kwa shule za sekondari tu bali za msingi na shikizi (awali), wamejitolea nguvukazi na fedha pia, lengo likiwa ni kuhakikisha kila shule inakuwa na miundombinu inayohitajika," anasema na kuongeza kuwa anaamini ujenzi wa madarasa utakamilika hivyo wanafunzi wote 4,089 watakapata madarasa na kusoma bila usumbufu.

JEKI YA MFUKO WA JIMBO

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Musoma, Charles Magoma anasema, Sh. milioni 52.43 za Mfuko wa Jimbo zimetumika kukamilisha ujenzi wa madarasa katika sekondari mbalimbali.

"Halmashauri yetu inayotunza fedha za mfuko huo inafanya manunuzi ya vifaa vya ujenzi baada ya kupata maelekezo kutoka kwenye Kamati ya Mfuko wa Jimbo chini ya Mwenyekiti ambaye ni mbunge Profesa Sospeter Muhongo," anasema Magoma.

Anafafanua kuwa Mkuu wa Wilaya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Musoma, John Kayombo, wamefanya juhudu kubwa ya kusimamia ujenzi wa madarasa hayo.

Kuhusu mgawo wa fedha hizo anasema kilichofanyika ni pamoja na ununuzi wa mabati 1,134 na mifuko 1,020 ya saruji vyote vikiwa na thamani ya Sh. milioni 52.18 ili kukamilisha miundombinu ya shule mpya ili zifunguliwe mwaka huu.

Mwenyekiti huyo anasema, sekondari za Seka na Kigera, kila moja ilipata mabati 216 na mifuko 200 ya saruji, huku Nyasaungu ikiwa na mgawo wa mabati 54 na mifuko 80 ya saruji.

"Hizo ni sekondari mpya, lakini mgawo wa vifaa umekwenda pia kwa zile zilizofunguliwa mwaka jana ikiwamo Dan Mapigano Memorial na Busambara ambazo zote kila imepata mabati 216 na mifuko 180 ya saruji," anasema.

Aidha, anasema shule shikizi ya Mwikoko iliopo kitongoji cha Mwikoko, Kijiji cha Chitare, Kata ya Makojo, imepata mabati 108 na mifuko 10 ya saruji, wakati ile ya Nyasaenge ya Kijiji cha Kataryo, Kata ya Tegeruka ikipata mabati 108 na mifuko 100 ya saruji.

HATUA ZILIPOFIKIA

Magoma anasema, shughuli zote za ujenzi wa miundombinu ya shule zimekuwa zikifanywa na wananchi, serikali, mbunge na wadau wengine wa elimu zikiwamo taasisi za fedha.

Anasema, kwa sasa kuna shule shikizi 12 na kwamba ujenzi na upanuzi wa shule hizo unaendelea, huku baadhi yake zikiwa tayari zimeanza kutoa elimu ya awali kwa watoto wa chini ya miaka sita.

"Halmashauri yetu ina shule 111 za msingi na sasa ujenzi wa madarasa mapya katika shule hizo unaendelea huku madarasa 380 yakiwa tayari yamejengwa kwenye shule hizo ndani ya miaka mitano kuanzia 2016 hadi 2020," anasema.

Magoma anasema, madarasa 120 yamejengwa kwenye sekondari 20 ndani ya miaka hiyo mitano na kuchangia sekonadari sekondari za Dan Mapigano Memorial na Busambara kufunguliwa mwaka jana.

Anasema jitihada hizo zinafanikishwa kwa usimamizi wa viongozi wa serikali, maofisa elimu na mbunge na kwamba maktaba zinaendelea kujengwa na nyingine zimekamilika na zinatumika kwenye baadhi ya shule na pia kazi ya kuboresha na kujenga nyumba za walimu na vyoo vipya inaendelea.

Habari Kubwa