Mabadiliko ya tabianchi, udhalilishaji unavyodumaza wanawake

11Mar 2017
Abdul Mitumba
Dar es Salaam
Nipashe
Mabadiliko ya tabianchi, udhalilishaji unavyodumaza wanawake

ATHARI za mabadiliko ya tabia nchi zinazoendelea kuikumba Tanzania zikihusisha kukauka kwa vyanzo vya maji kama mito na maziwa, ongezeko la joto, mafuriko na tetemeko la ardhi pamoja na kukosekana kwa usawa kijinsia,

Hayo ni miongoni mwa mambo yanayokwamisha jitihada za wanawake kujiletea maendeleo kwa wakati.

Japo mabadiliko ya tabianchi ni la hoja ya kisayansi zaidi, lakini athari zake zimeonekana kwenye ukame, vimbunga vya nchikavu na baharini kama tsunami, vipindi vya baridi kali na mabadiliko ya misimu ya mvua vyote huwatatiza wanawake si Tanzania na sehemu nyingine duniani.

Wakati wiki hii tunaendelea kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, iliyosherehekewa Machi 8, wadau wa masuala ya wanawake wanaona kuwa matokeo ya changamoto hizo, wanawake hulazimika kutumia muda mwingi kusafiri umbali mrefu kila wakati kusaka maji. Muda huo wangeutumia kwa shughuli za uzalishaji iwe mashambani, viwandani au maeneo mengine wanayojiajiri.

Mathalani, ripoti ya Mpango wa Kulinda Mazingira wa Umoja wa Mataifa(Unep), inaeleza kuwa vyanzo vikuu vya maji vinavyolisha nchi za Afrika Mashariki ambavyo ni Mlima Kilimanjaro na Mto Pangani vinakauka.

Athari zake ni pamoja na ukosefu mkubwa wa maji mikoa ya Kilimanjaro, Tanga, Arusha, Manyara, Morogoro na , Pwani. Athari zake zinafika pia nchini Kenya na yote haya yanagusa maisha ya wanawake na watoto.

Ukame huo na mvua haba au zisizo na utaratibu husababisha ukosefu wa chakula na kuwaweka wanawake kwenye wakati mgumu kwa vile hawana cha kuwalisha watoto wala familia.

Lakini, sanjari na mabadiliko hayo ya tabia nchi, pia kukosekana kwa usawa wa kijinsia miongoni mwa wanajamii, kunachangia wanawake kudumaa kimaendeleo.

Tatizo hili nalo ni kubwa kiasi cha kuwa kikwazo cha maendeleo kwa wanawake kiuchuni, kielimu, kijamii na kitamaduni kwa sababu linaanzia katika ngazi za familia.

Kutokana na vikwazo hivi, shirika lisilo la kiserikali la Fikra Huru (Kikhu) lenye makazi yake Kibaha mkoani Pwani, limeona kuna kila sababu ya kubuni na kuendesha mradi wa wanawake, usawa wa kijinsia na mazingira.

Mradi huu umelenga kuwajengea uwezo wanawake katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na ushiriki wa karibu katika kutambua sera na miongozo mbalimbali inayowagusa kuanzia ndani ya familia hadi kimataifa.

Mratibu wake, Alice Ndubwene, anasema pamoja na kutatizwa na tabianchi wanawake wanaishi na ‘simba’anayewatafuna naye ni unyanyasaji kijinsia.

Anataka wanawake kufahamu kuwa kuna aina 15 za unyanyasaji dhidi ya wanawake, lakini mradi umelenga kufundisha watambue angalau aina saba ambazo ndizo zimetumika kuwaelimisha wanawake wa kata ya Kongowe Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani.

UKATILI
Aina hizo ni ukatili wa kimwili, kijinsia, kiakili, kiuchumi, mila na desturi na ukatili wa kingono ambao anasema umekuwa ukiwakwaza wanawake wengi katika kufikia malengo waliyojiwekea katika kila sekta.

Mwezeshaji wa mafunzo ya mradi huo, Aisha Vijavara, anasema aina zote hizo za ukatili zinawanyima haki na usawa wanawake mbele ya jinsi nyingine.

“Madhara yatokanayo na ukatili wa kimwili ni vipigo vinavyowasababishia majeraha na wakati mwingine ulemavu.

“Ukatili wa mila na desturi umesababisha wanawake wengi kunyimwa fursa ya kutoa maoni wakati wa vikao vya familia, huku ukatili wa kingono ukiibuka zaidi wakati wanawake wanapohitaji ajira au haki za kisheria,” anasema Aisha.

Anafafanua kuwa aina hii ya ukatili inawaumiza zaidi wanawake katika matukio ya kubakwa au kulazimishwa kufanya tendo la ndoa hata wakiwa na waume zao bila ridhaa yao.

“Ukatili wa kijinsia unajielekeza zaidi katika kumshambulia mwanamke kwa maneno ya kashfa ikiwamo matusi na maumbile yake,” anasema.

Akizungumzia ukatili wa kiuchumi, Aisha anasema kuwa aina hii ya ukatili ni mbaya zaidi kwa sababu wahusika wanashiriki katika kuwanyima wanawake kumiliki mali za kurithi au za familia na wakati mwingine huzuiwa kufanyakazi kwa kisingizio cha ndoa.

Anawataka wanawake kusimama imara dhidi ya watu wanaowafanyia aina hizi za ukatili na nyinginezo kwa kutambua kuwa wanaweza kupata kila wanachokihitaji bila kuruhusu kunyanyaswa ili mradi watambue kuwa ni mambo ambayo hawapaswi kutengewa.

Wakizungumza katika mahojiano na gazeti hili muda mfupi baada ya kumaliza mafunzo hayo, washiriki Rachel Allan na Sada Mzelu wanakiri kuwapo kwa aina hizo za ukatili katika jamii na athari za wazi zinazatokana na mabadiliko ya tabia nchi hasa katika maeneo yao.

“Kwa mfano, maeneo mengi ya mkoa wa Pwani hasa wilaya ya Kibaha nyanzo vya maji vimekauka na vilivyobaki havina maji ya kutosha, hivyo kutulazimu wanawake kuhaha kusaka maji kwa ajili ya matumizi ya lazima,” anasema Allan.

Anasema wametambua wajibu wao kwa kiasi kikubwa na kwamba sasa wapo tayari kukabiliana nazo kikamilifu, ikiwamo kuzuia watu kukata miti ovyo, kutunza na kuvilinda vyanzo vya maji ikiwa ni pamoja na kupanda miti katika maeneo wanayoishi.

Kuhusu vitendo vya kikatili, Mzelu anasema kuwa, mafunzo hayo yamewafumbua macho na masikio hivyo watayatumia kukabiliana navyo.

“Kama ni ukatili tumefanyiwa sana, ni kwa sababu tulikuwa hatujui, lakini kuanzia sasa tutapambana na matukio yote yanayoashiria ukatili dhidi tu,” anasema.

Mradi huo umefadhiliwa na Mfuko wa Wanawake Tanzania (TWF) na malengo ya Fikhu ni kuchangia katika kujenga jamii yenye uelewa ili ipiganie usawa na utu wa kila mmoja bila kujali jinsia, kipato au itikadi yake.

Habari Kubwa