Mabeki wa kulia bora zaidi Ulaya

17Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mabeki wa kulia bora zaidi Ulaya

MABEKI wa pembeni wamekuwa ndio watengenezaji wa nafasi za kufunga mabao katika soka la kisasa. Chukua hata mfano wa mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, Liverpool.

Joshua Kimmich.

Mabeki wao wa pembeni, Andy Robertson na Trent Alexander-Arnold wametengeneza nafasi nyingi zaidi za pasi za mwisho.

Bayern wana nyota kama Joshua Kimmich, David Alaba na usajili wao mpya, Benjamin Pavard ambao wametawala winga zote. Wachezaji kama Jonny na Matt Doherty wamekuwa na kiwango cha kuvutia katika klabu yao ya Wolves kwenye Ligi Kuu ya England msimu huu.

Mabeki wa kulia ndio wameonekana kuwa wa muhimu zaidi kwa kipindi cha muongo mmoja uliopita. Beki anayecheza kwa ubora wake katika majukumu yake, kulinda lango lake kushambuliwa. Huwa pia anatambaa na mipira pembeni na kuitupia katikati kwa ajili ya kutengeneza mashambulizi kwa timu pinzani. Yote kwa yote hapa tunawaangalia mabeki wa kulia watatu ambao ndio bora zaidi kwa msimu huu barani Ulaya...

Kwanza, heshima kwa kuwataja mabeki wengine ni: Matt Doherty (Wolves), Noussair Mazraoui (Ajax), Łukasz Piszczek (Borussia Dortmund), Achraf Hakimi (Borussia Dortmund).

 

3. Aaron Wan-Bissaka (Crystal Palace)

Kama timu kama Arsenal, Manchester City na Manchester United zinakimbizana kuwania saini yako ukiwa kwenye umri wa miaka 21, inamaanisha kwamba umefanya kazi kubwa. Wan-Bissaka alilazimika kuwa chaguo la pili mbele ya Timothy Fosu-Mensah aliyekuwa akicheza kwa mkopo msimu uliopita, lakini baadaye akaanza kuaminiwa na kocha Roy Hodgson, ambaye amemfanya kuwa chaguo la kwanza la beki wa kulia wa Palace kwa msimu wote.

Si mabeki wengi wa kulia ni bora duniani kuliko yeye hasa linapokuja suala la mtu kwa mtu. Amekuwa na uwezo mkubwa wa kusukumiza mashambulizi mbele hasa kutokea pembeni, hasa baada ya kuhakikisha kwamba lango lake liko salama. Uwezo wake bado umeonyesha kuwa ana uwezo mkubwa mno wa kuwazuia mawinga wakali kuleta madhara langoni mwake. Katika orodha hii anashika nafasi ya tatu kama beki bora wa kulia barani Ulaya akiwa na wastani wa kukaba 3.7 kwa mchezaji mmoja mmoja na 2.4 kwa mchezo.

 

2. Joshua Kimmich (Bayern Munich)

Phillip Lahm ni jina kubwa kwenye mpira wa miguu, hasa kwa Bayern Munich. Shukrani kwa Bayern, walikuwa na mtu sahihi wa kurithi mikoba yake na huyo ni Joshua Kimmich ambaye anafananishwa mno na Lahm. Kwa miaka mingi mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24, amekuwa nyota mwenye mafanikio makubwa kwa klabu yake na timu ya taifa.

Kwa msimu huu amecheza mechi 34 za Ligi Kuu akitoa pasi za mwisho 13, huku akifunga mara mbili na kuwa na mafanikio ya pasi zake kuwa sahihi kwa asilimia 90. Wakati ambao kikosi hicho cha Niko Kovač kilishindwa kutawala kama ilivyotarajiwa, Kimmich aliendelea kuwa bora zaidi na nyota kwa klabu hiyo.

 

1. Trent Alexander- Arnold (Liverpool)

Bila shaka. Kile ambacho Alexander-Arnold amefanikiwa mwaka huu ni ndoto ya kila mchezaji duniani. Hasa ikizingatiwa kwamba, ndio kwanza ana umri wa miaka 19, lakini amefanya mambo makubwa. Ni mmoja wa bidhaa muhimu zaidi ya kocha Jurgen Klopp msimu huu, akitengeneza pasi za mwisho 12 kwenye Ligi Kuu ya England, akivunja rekodi ya kuwa beki aliyetengeneza pasi nyingi zaidi kwa msimu mmoja.

Huku akiwa na stamina ya kukimbia wakati akiwa na mpira, amekuwa akigawa mipira kwa uhakika mkubwa kwa winga. Akiwa anatumia mguu wake wa kulia, pia alifunga bao matata kwenye mchezo dhidi ya Watford.

Wakati linapokuja suala la akili na uwezo mkubwa dimbani, huwezi kusahau kile alichokifanya kwenye mchezo wa pili wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Barcelona, na kuisaidia timu yake kufuzu kwa fainali ambayo walishinda taji hilo kwa mara ya sita katika historia yake. Na katika umri wake wa miaka 19, ana safari nzuri zaidi mbele yake.

Habari Kubwa