Mabinti watano shuleni walivyoibua kifaa kinachodhibiti mbu wa malaria

08Apr 2021
Christina Mwakangale
Dar es Salaam
Nipashe
Mabinti watano shuleni walivyoibua kifaa kinachodhibiti mbu wa malaria
  • Ngurumo aina yake inayomfukuza
  •  Wagunduzi vyuo vikuu, imo udaktari

MTU anapozungumzia kuwapo ugonjwa wa malaria, katika nchi zinazoendelea utabaini ni kati ya vinavyosababisha kurudisha maendeleo nyuma.

Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dk. Amos Nungu. picha mtandao

Kwa maana malaria huathiri zaidi mataifa ya Kusini mwa Jangwa Sahara, katika baadhi ya mataifa ya Asia na Amerika ya Kusini, ambayo ugonjwa huo una tiba, licha kusababisha vifo vingi duniani.

Shirika la Afya Duniani (WHO), linasema kuna kifo cha mtoto mmoja kila baada ya dakika mbili, huku ongezeko jipya la wagonjwa zaidi ya milioni 200 wakiripotiwa kila mwaka.

Jukumu la kukabiliana na ugonjwa huo linaendelea kutafutiwa ufumbuzi na wataalamu wa afya, huku WHO ikipendekeza walio katika hatari ya kupata malaria wakingwe kwa kutumia mbinu zilizothibitishwa kuwa bora zaidi.

Hapo zinatajwa mbinu kama matumizi ya vyandarua vilivyotiwa dawa (ITN) na kupulizwa dawa ndani na nje ya nyumba (IRS).

WABUNIFU WAJITOKEZA

Katika kuongeza juhudi za kupambana na ugonjwa huo, wapo wanasayansi wanaochipukia, wasichana watano wahitimu wa Shule ya Sekondari Jangwani, wamebuni mbinu mpya ya kujikinga malaria, wakiitaja kuwa rafiki wa mazingira.

Paulina Haule, mmoja wa wabunifu hao wa kifaa hicho kiitwacho ‘Ultraltraconic Mosquito Repellent’ anasema wazo la ubunifu wao, umeboreshwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kupitia Atamizi ya Teknohama ya Dar es Salaam (DTBi).

Kupitia ubunifu huo mwaka 2019, Paulina pamoja na wenzake wane; Grace Yusto, Julieth Maisorry, Bupe Mayala na Nia Mfaume, walitunukiwa tuzo iitwayo ‘Project Pitching Winners 2019’ iliyotolewa na mradi wa Future STEM Business Leaders (FSBL).

Mpango huo huwaendeleza kwa kuwapa ujuzi wanafunzi wa masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) kutoka katika shule mbalimbali ambao ulioanza mwaka 2017.

Akizungumza na hivi karibuni kwa niaba ya wenzake Nipashe, Paulina anasema, mradi huo umekuwa mpya na kugundua mambo kadhaa maishani.

“Nimekuwa mtu mpya kabisa na nimegundua kwenye maisha yetu kuna matatizo ambayo ni mengi tunaweza kuyatatua, licha tu ya kuwa na elimu ya darasani.

“Elimu ya darasani tunaweza kuibadili kuwa halisi hata katika biashara na kufanya mambo mengi katika maisha yetu ya kawaida. Natamani wanafunzi wanaokuja wajue namna ya kutumia elimu ya darasani,” anasema Paulina.

Paulina anasema, amehitimu masomo ya kidato cha sita katika Shule ya Sekodari Jangwani mwaka, jana na sasa anasoma Shahada ya kwanza katika chuo cha St. Joseph akiwa katika taaluma ya utabibu.

“Watu huchukulia sayansi ni somo la jinsia, gumu labda watoto wa kike hawawezi wakalimudu, kila mmoja anaweza akalisoma akitulia.

“Ni ‘exposure’ (uelewa) kupitia mradi huu na nimepata mwamko mkubwa wa kusimama mbele za watu. Kwanza, ifahamike kisayansi mazingira yetu mbu ni muhimu na hawatakiwi kufa katika mazingira yetu, sababu kuna viumbe wanawategemea, hivyo kifaa hiki kinafukuza mbu na si kuua,” anasema.

Anasema, kifaa hicho kinatumia sauti zenye mlio wa chini ambao binadamu hausikii ila mbu pekee na kwamba mbu akizisikia sauti hizo huhisi usumbufu na kukimbia.

“Kifaa kinatumia frequency (mzunguko) wa mawimbi sauti yenye mlio mdogo ambao unampiga mbu na kumfanya akimbie asikae eneo hilo.

"Sauti hizo binadamu huwezi kuzisikia, lakini kwa mbu kwake ni sauti kubwa mno. Kifaa hicho ni rafiki wa mazingira hakitoi harufu hakina kelele na kinabebeka. Tulipogundua kifaa hiki ukikiona kina muonekano mkubwa, lakini kikiendelea kuboreshwa kitapungua,” anasema.

Paulina anabainisha kwamba, kwa sasa hakuna teknolojia kama hiyo popote duniani, huku wakisubiri kukamilisha usajili na kupata haki miliki.

“Tunasubiri tukamilishe kila kitu ili tupate haki miliki na kuingia sokoni. Tunashukuru programu hii ya FSBL kuibua huu ubunifu. Kifaa kina uwezo kutumia umeme wa jua au umeme wa kawaida,” anaeleza Paulina.

Paulina anakamilisha kwa kusema  mradi huo umemjengea ujasiri wa kuongea na ilikuwa si rahisi kujinadi mbele ya watu, sasa amebadilika.

WADAU COSTECH

Mkurugenzi Mkuu COSTECH, Dk. Amos Nungu, akizindua rasmi mradi wa Future STEM Business Leaders (FSBL) kupitia Atamizi ya Teknohama ya Dar es Salaam (DTBi), wiki hii jijini, anasema mradi huo ulianza mwaka 2017 kupitia DTBI.

Hadi sasa anaeleza kuwa ana uzoefu wa kuwajengea uwezo vijana kubuni na kukua kibiashara, unafanyika kwenye shule 13, kati yake nane kutoka Dar es  Salaam na tano Arusha.

Dk. Nungu anasema, ni mradi utakaowajengea uwezo wanafunzi hao katika kupitia masomo ya sayansi na kubaini fursa za kujiajiri na kuajiri.

“Wadau wa elimu na jamii iwaandae vijana ili kuitumia elimu wanayoipata shuleni hususan somo la sayansi, kutatua matatizo kwenye jamii,” anasema Dk. Nungu.

Anasema kutokana na dunia kukua kidigitali, ipo haja ya wanafunzi kuandaliwa tangu sekondari badala ya kusubiri wafike ngazi ya juu kama chuo kikuu.

"Mradi unasimamiwa na COSTECH kupitia DTBi, umefadhiliwa na Idara ya Fizikia ya nchini Uingereza. Unatekelezwa pia tukishirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Fizikia na Arusha Tech," anasema Dk. Nungu.

Kadhalika, Dk. Nungu anatoa wito kwa vijana kuwa sehemu ya utatuzi wa matatizo yaliyopo kwenye jamii kwa kutumia teknolojia.

"Msiikimbie sayansi! Vijana wengi wanakuja na mawazo yenye ubunifu lakini hayafanyiwi kazi, kupitia mradi huu wataibuliwa wenye wazo zuri ambalo ni la kibiashara na kusaidia jamii," anasema Dk. Nungu.

Anasema vijana wenye wazo mazuri watapata mafunzo ya miezi sita, ili kuwezesha walichojifunza kuwa uhalisia na kukuza uelewa, kisha kuwekeza kipato chao na taifa, kwenda sambamba na dunia ya kidigitali.

Pia, anautafsiri ni mradi maalumu wa kisayansi, unaobeba wazo la ubunifu kutengeneza ajira na uchumi.

"Tuna shule nane za Dar es Salaam kwenye mradi, pia tano kutoka Arusha. Tunawapa elimu ya ziada kufanya sayansi wanayoisoma kuwa biashara kupitia ubunifu wao," anasema Josephine Sepeku, Meneja wa Mradi huo.

Ofisa Utafiti Mwandamizi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Rodgers Msuya, anasema wizara inatambua mchango wa mradi huo kukuza sayansi na vipaji.

MALARIA IKOJE?

Mwaka 2017, karibu nusu ya idadi ya watu duniani walikuwa hatarini kuugua malaria.

Pia, katika kundi hilo waliokufa, asilimia 61 au theluthi mbili ni watoto, huku wajawazito na watu walio na mfumo hafifu wa kinga waliangukia katika hatari.

Mwaka 2017 kwa mujibu wa WHO, kuliripotiwa watu milioni 219 waliougua malaria kutoka nchi 87 na inakadiriwa 435,000 walifariki dunia.

Barani Afrika, kunatajwa kuwapo maambukizi asilimia 92 ya malaria duniani. Pia, sehemu kubwa zaidi ya vifo kwa takwimu za mwaka huo, ni zilichangiwa na malaria.

Habari Kubwa