Machungu  petroli, dizeli yanapochagiza...

18May 2022
Gaudensia Mngumi
DAR ES SALAAM
Nipashe
Machungu  petroli, dizeli yanapochagiza...
  • * Janga uhaba wa kuni, mkaa  latikisa

INGAWA Tanzania  ina utajiri mkubwa wa rasilimali za misitu  na pengine muuzaji mkubwa wa mbao ghafi Afrika Mashariki, uhaba wa mkubwa wa mkaa na kuni kupikia majumbani na majiko ya biashara ni kitisho kinachokaribia  kulikabili taifa.

Mchakato wa kupata nishati ya uhakika kwa ajili ya  matumizi ya jikoni vijijini na mijini haujawa wa uhakika, hali inayodhoofisha juhudi za kufikia nishati endelevu kulinda mazingira.

Sekta ya nishati majumbani inayotumia kuni na mkaa imekuwa changamoto jijini  Dar es Salaam na kutishia hatima ya familia nyingi.

Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa licha ya bei za petroli, dizeli, mafuta ya taa na gesi kupaa kila mwezi, upatikanaji wa kuni na  mkaa kupikia majumbani na migahawani nayo ni shida japo  haijazungumzwa.

Malalamiko mengi ni ongezeko  bei ya petroli na dizeli  kupandisha gharama za  kila kitu,  sababu kubwa ikitajwa kuwa ni vita ya Urusi na Ukraine.

Licha ya gharama za  kuni na mkaa zinazotumiwa na wakazi wengi mijini nazo zimekuwa juu kupindukia, lakini ni haba, mkaa ni wa  miti michanga na myepesi inayogeuka majivu muda mfupi ikiwekwa kwenye jiko.

Kwa  Dar es Salaam mkaa na kuni vinavyotumiwa kupikia ni haba na ghali kupindukia na familia nyingi zinatumia nishati isiyo rasmi kama vipande vya ‘marine body’ vinavyotumika kwenye ujenzi .

Zinapokaangwa chips na vyakula vingine  uhaba unaonekana wajasiriamali wakijiongeza kwa kchanganya mkaa, kuni, makuti, makumbi na vifuu.

Sehemu nyingine kinamama na babalishe wanatumia vipande vya makasha ya mbao yaliyofungashia bidhaa mbalimbali zilizoingizwa nchini kutoka ng’ambo. Wapo pia wanaokusanya vipande vya mbao kutoka kwenye `saiti’ zinazojengwa,vumbiranda,pumba za mchele.

KUNI MKAA GHALI

Familia za kipato kidogo hutumia kuni hata  miti ya mihogo na vinginevyo, wanavyoviokota mashambani.

Baadhi wananunua kuni  sehemu unapouzwa mkaa, kipande kidogo pengine cha mwarobaini kikianzia shilingi 500 na kuendelea wakati mzigo wa vipande 10 unaweza kuzidi hata shilingi 5,000.

Baadhi ya mamalishe wa soko la Buguruni wanaozungumzia uhaba huo wanasema kuni ni ghali  hasa zinapokuwa za miti migumu hufikia hata zaidi ya Shilingi 2,000 kwa kipande na hazipatikani.

“Wenzetu wanalalamikia mafuta ya pampu sisi hatuna wa kutusemea kuni na mkaa ni ghali mno. Kipimo kidogo cha mkaa ni Shilingi 2,000 hakiivishi maharage nusu kilo, ” anasema mamalishe wa sokoni Buguruni.

Analalamikia: “Mkaa ni mwepesi mno labda wa matawi ya mwarobaini na mkurunge maana ndiyo miti iliyopo Dar. Miembe inapasuliwa mbao zinazotengeneza samani siyo kuchoma mkaa tena, sijui tunapoelekea...” anasema mjasiriamali huyo.

JANGA LA NISHATI

Wafanyabiashara wa kuni na mkaa wa maeneo ya Mbagala, Manzese na Buguruni, wanaamini miji mingi  huenda inakabiliwa na uhaba mkubwa wa  kuni  na mkaa wakihofia ni tatizo la kitaifa.

Dkt. Felcian Kilahama, Mkurugenzi mstaafu wa Idara ya Misitu na Nyuki, anapoulizwa kuhusu hofu ya uhaba wa nishati hiyo anasema ni suala linalohitaji utafiti kujua ukweli.

Anakumbusha kuwa misitu imekuwa chanzo kikuu cha riziki kwa Watanzania  wengi, nguzo kuu ya  ustawi wa taifa kuanzia uhifadhi wa mazingira, kilimo, wanyamapori na utalii, uwiano kiikolojia na uzalishaji wa  bidhaa na  rasilimali muhimu kama mbao, kuni na mkaa au nishati lakini haijalindwa kikamilifu.

“Sekta ndogo ya misitu ya asili inahitaji kusimamiwa ipasavyo, inakosa ulinzi inaharibiwa na hii itachangia pakubwa katika ukosefu wa mikaa na kuni mijini na vijijini kama watu wanavyodai.”

Anaeleza kuwa hata mkaa unaozalishwa leo ni wa miti michanga na kiwango cha kuni kinachouzwa na kuingizwa mijini ni kidogo na kinazidi kupungua.

Anasema  juhudi zinahitajika na kukumbusha kuwa bila menejimenti na usimamizi madhubuti wa misitu ni muhimu na kwamba misitu ni mlinzi na mwendelezaji  sekta zote zinazozalisha mapato na ajira nchini.

Anatoa mfano kuwa misitu ina umuhimu kwenye kilimo inaleta mvua, ni chanzo cha mvua na maua kwenye asali, ndiyo makao ya wanyama na viumbe pori, vyanzo vya maji, kusafisha hali ya hewa na kuondoa hewa ukaa angani.  Aidha ni malighafi ya  mbao kwenye ujenzi na  karatasi,  lakini ni chanzo cha nishati hasa kuni na mkaa zinazotumika nchini kote.

Mtaalamu huyo wa misitu anasema:

“Mahitaji ya kuni na mkaa yanaelekea kupita uwezo wa uzalishaji, hivyo, uvunaji wa rasilimali za misitu kwa mahitaji ya nishati na ujenzi  yalihitaji kupangwa na kusimamiwa vizuri kwani kuna hatari kwa mazingira.”

 

UVUNAJI Vs UPANDAJI

 

Dk. Kilahama anasema watu wanalalamikia ukosefu wa kuni na mkaa mijini, lakini Watanzania wengi wavuna zaidi kuliko kupanda kutumia kuni na mkaa kwa fujo kuliko kuwa waangalifu na wanaobana matumizi.

Anasema kwa mfano, ukifika vituo vikuu  vya kupika vyakula kwenye barabara kuu wengi wanapika vyakula kwa mkaa mwingi, bila majiko banifu, tena wengine wakitumia majiko ya ‘ringi za matairi’ bila kujali kuwa mkaa na miti vinakaribia kutoweka kama ambavyo uoto wa asilia unavyomalizika.

“Nimefanya utafiti nikagundua kuwa  wanatumia mkaa kwa fujo kwa sababu wanaupata pengine kwa njia zisizo rasmi kwa ujanja na gharama nafuu, hivyo hawaoni hasara, japo ni janga kwao na kwa taifa. Itafika siku hakuna miti wala mkaa na kuni wote tutaumia...” anaonya.

MKAA NI HASARA

Anasema  kama watu wanavyolalamikia kupungua mkaa mijini ni jambo ambalo lilifahamika kwa kuwa kuchoma mkaa  kunamaliza miti na misitu.

“Ni wakati wa kuboresha matumizi ya kuni na kuachana na mkaa unaoleta hasara kubwa kwenye misitu ya asili na mifumo ya                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                           ikolojia, kwa mfano kuchoma tani 10 za miti ili kupata tani moja ya mkaa. Huo ni uharibifu mkubwa wa mazingira  na maliasili miti,” anaonya Dk. Kilahama.

Anasema licha ya kuwepo teknolojia ya uchomaji mkaa kisasa unaopunguza uharibifu lakini hata teknolojia hiyo ya kisasa zaidi haina manufaa kwa vile huchoma tani sita za  miti kupata tani moja ya mkaa ambayo ni hasara pia.

   Lakini, anasema vifaa vyake ni  ghali na  siyo wengi wanaoweza kumudu, akisema unatumia mapipa makubwa ya kuchoma mkaa yenye matanuru na mifuniko ambayo baada ya kujaza miti moto huwashwa, mifuniko hufungwa kuzuia hewa ya oksjeni kuiingia ndani ya tanuru.

Anaeleza kuwa mapipa hayo au ‘wood retorts’ yangeweza kutengenezwa nchini na kupiga marufuku uchomaji mkaa wa kizamani ambao unatishia hatima ya miti, misitu na mazingira. 

MAJIKO BANIFU YA KUNI

Dk. Kilahama anataka kuwekeza zaidi kutengeneza majiko banifu  ya kuni, ambayo yataboresha muundo wa matumizi ya kuni ili zitumike kidogo kwa ufanisi mkubwa  kupika chakula kingi kwa nishati kidogo zaidi.

Anasema majiko hayo yatumike nchi nzima ili kuokoa miti na misitu na kuhamasisha ulinzi wa misitu ya asili, upandaji kwa kasi kubwa wa miti ya asili pia kupunguza shughuli  zinazotishia hatima ya sekta ya misitu.

Anakumbusha kuwa misitu ni mlinzi wa  hali ya hewa na mdhibiti wa mabadiliko ya tabianchi,  ndiyo mtoaji wa hewa safi, mlinzi wa bioanuwai za viumbe, maeneo ya maji, udongo, nishati na kilimo cha mazao ya chakula na utoaji wa vifaa vya ujenzi vya mbao na miti.

TEKNOLOJIA JIKONI

Baada ya kusikia kuhusu uhaba na ughali wa kuni na mkaa  uchunguzi ulifanywa kwenye  baadhi ya maduka kuchunguza bei ya majiko ya kisasa yanayotumia nishati kwa ufanisi.

Jiko la presha (linalopika kwa mvuke)  la umeme au ‘electric pressure cooker’  linaloelezwa kuwa hutumia umeme ‘kiduchu’ kupika vyakula vigumu kama kande na maharage, hupatikana  kuanzia Shilingi 180,000.

 Majiko hayo huuzwa kwenye maduka makubwa ‘super market” na kwingineko lakini si rahisi kwa Watanzania wengi kuyamudu hasa wanaotumia kuni, vifuu, makumbi ya nazi.

  Taasisi ya kuendeleza huduma za nishati endelevu TaTEDO, ni moja ya maeneo yanayozalisha jiko sanifu la umeme lenye presha (mvuke),  ambalo linaelezwa hupika kwa ufanisi mkubwa na kwa nishati kidogo.

Ripoti za TaTEDO zinaeleza kuwa imefanya utafiti pamoja na vyuo vikuu vya kiteknolojia na kutengeneza jiko sanifu  la umeme lenye mvuke (JULEP) linalopika kwa ufanisi mkubwa na kwa kutumia gharama ndogo ya umeme.

Baadhi ya vyakula vinavyopikwa ni makande ya kilo moja na nusu kwa dkakika 60 kwa umeme wa nusu ‘unit’ ikumbukwe ‘unit’ moja ya umeme ni shilingi 360  hivyo hutumia nusu au shilingi 180 kupika chakula hicho ambacho kwa mkaa kingepikwa kwa vipimo viwili vya Shilingi 3,000 kwa kuwa kipimo kidogo ni 1,500.

Aidha, maharage, nayo hutumia muda mfupi na unit chache za umeme jambo ambalo  lingetunza mazingira kwa kupunguza moshi wa kuni angani unaoongeza hewa ukaa na  kuokoa misitu.

Pengine ni wakati wa serikali kuanzisha mfuko wa nishati na kutoa ruzuku kwa wazalishaji wa majiko hayo kama TaTEDO ili kuwawezesha Watanzania wa kipato kidogo mijini na vijijini wasiomudu kupikia gesi na umeme kutumia majiko sanifu na kuokoa taifa na janga uhaba wa kuni na mkaa pamoja na misitu kutoweka.

Juhudi za kusambaza umeme vijijini ziende pamoja na kufikisha majiko sanifu ya umeme kwa wanavijiji ili walinde misitu.

Habari Kubwa