Madhara ya kutotambua na kutotumia kipaji chako-2

05Dec 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Madhara ya kutotambua na kutotumia kipaji chako-2

WIKI iliyopita tulianza kuzungumzia mada hiyo ya madhara ya kutotambua na kutotumia kipaji chako ambapo mwandishi alibainisha kwamba maendeleo ya taifa lolote duniani huchangiwa na uwezo binafsi wa utendaji kazi wa wazalishaji.

Kwamba ikiwa kama kuna taifa lililoendelea, basi sababu kuu ni uwezo au nguvu ya asili ya kiutendaji wa watu wake ni kubwa sana.

Akabainisha kwamba tatizo la mataifa mengi yanayoendelea likiwemo taifa la Tanzania kuwa na maendeleo hafifu kuna natokana na uwezo mdogo wa utendaji kazi katika uzalishaji, hivyo kushindwa kuzalisha kwa kiwango cha juu na kunarudisha maendeleo nyuma.

Akafafanua kuwa uwezo au nguvu ya asili ya utendaji kazi aliokuwa akiuuzungumzia ni kipaji na kwamba sababu ya taifa kutoendelea au kuchelewa kuendelea inatokana na kutotambua nguvu au uwezo wa asili wa utendaji kazi wa watu katika kuzalisha.

Akamalizia kwa kujikita zaidi katika mazingira ya malezi ambayo huwa na athari kubwa sana kwa watoto kutambua vipaji vyao.

Sasa endelea na sehemu hii ya pili ya mada hii:

HIVYO, uwezo binafsi wa watoto huchangiwa sana na mazingira ya malezi wanayolelewa kwani watoto hujifunza zaidi kwa kuona vitendo na sio maneno.

Pia kama kipaji kinaweza kurithishwa toka kwa mzazi hadi kwa mtoto kutegemea vinasaba basi pia jinsi atakavyokuwa mzazi kuna uwezo mkubwa wa mtoto kuwa sawa na wazazi wake.

Kama mzazi atakuwa na kipaji cha uchoraji na mtoto akalelewa katika mazingira ya uchoraji kuna uwezekano mkubwa wa mtoto kuwa mchoraji pia kutokana na mazingira aliyolelewa na pia anaweza akawa na kipaji cha uchoraji kutokana na vinasaba vya wazazi.

Tukichunguza kwa makini tutakuta kwa asilimia kubwa ya watu wenye vipaji takribani ukoo mzima una watu wenye uwezo unaofanana.

Chunguza uwezo wa watoto wa walimu, utakuta ni mkubwa sana kutokana na malezi waliyolelewa nayo, yaani mazingira ya kitaaluma. Ni nadra sana kukuta mtoto wa mwalimu kuwa na uwezo mdogo wa kitaaluma.

Chunguza familia za waigizaji, waimbaji, wachoraji na zingine zenye vipaji, utakuta waimbaji hurithisha uimbaji kwa watoto wao kwa njia ya vinasaba na pia kwa njia ya mazingira.

Lakini pia chunguza koo nyingi za viongozi hukuta familia zao ni viongozi wa kada mbalimbali, vipaji hivi vya uongozi hutokana na mazingira ya malezi waliyolelewa nayo pia kwa njia kurithi vinasaba.

Tunaweza kusema vipaji vinaweza kutengenezwa au kuwezeshwa kutokana na mfumo wa malezi kimazingira yaani kipaji kinaweza kukuzwa kwa njia ya elimu na pia vipaji vinaweza kurithishwa kwa njia ya vinasaba kutoka kizazi hadi kizazi.

Hivyo tunaweza kurithisha vipaji vyetu kwa watoto wetu kama tutaweza kuwajengea mazingira rafiki kwa kuvifanyia mazoezi vipaji vyetu ili watoto wetu waweze kujifunza kutoka kwetu.

Kama sisi wazazi hatutambua uwezo wetu wa asili wa utendaji kazi ni wazi kabisa tunajenga mazingira magumu kwa vipaji vya watoto wetu.

Watoto wetu wanaweza kutambua vipaji vyao kwa kuwajengea miundombinu mizuri ya elimu, na pia kwa kuanzisha vituo mbalimbali vya maendeleo na ukuzaji wa vipaji.

Viashiria vizuri vya vipaji kwa watoto wetu ndio njia ya kuweza kuvitambua vipaji. Ili uweze kuvitumia ni lazima tuvitambue kwanza na kisha kuvitumia.

Njia rahisi sana ya mtoto kutambua kipaji chake ni kwa kujaribu vitu vingi sana na kupima uwezo wa utendaji wake katika vitu alivyojaribu kwa kupima kati ya vitu vingi alivyojaribu ni vingapi amefanya vizuri zaidi kuliko vyote?

Kama katika vitu alivyojaribu vipo alivyofanya vizuri kuliko vyote basi anaweza kutambua kipaji chake.

Lakini pia njia nyingine ya kutambua kipaji ni kuangalia ni kitu gani mtoto anakipenda kufanya kuliko vyote? Kile anachokipenda huenda kikawa ndio kipaji chake.

Mfano mtoto anapenda sana kuangalia mpira kuliko michezo mingine yote tunaweza kusema mtoto huyu anaweza baadaye akawa na kipaji cha uchambuzi wa mpira, akawa mkufunzi (kocha) akawa mwamuzi wa mpira au pia akawa mchezaji mpira mzuri sana.

Vilevile kama mtoto anapenda sana kufuatilia masuala ya mziki mtoto huyu anaweza akawa mwanamuziki mzuri baadaye, mtunzi wa nyimbo au akawa mwalimu wa muziki na pia anaweza akawa mchezaji wa muziki baadaye.

ITAENDELEA

Mwandishi ni Mwalimu wa shule ya sekondari ya Majengo, Moshi. Anapatikana kwa simu: 0674-513851

Facebook page.MwlAndsam

Instragram:Mwl.mwambungu

 

 

Habari Kubwa