Madudu miradi ya 'Force Account'

18Jul 2021
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Madudu miradi ya 'Force Account'

​​​​​​​HIVI karibuni kumeshuhudiwa miradi mingi ya serikali ikitekelezwa kwa utaratibu uliopewa jina la 'kizungu' la 'Force Account', Waswahili tunauita 'mafundi jamii'.

Aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa miaka minane kuanzia mwaka 2006, Ludovick Utouh, anaifasili dhana ya 'Force Account', akisema:

"Ni utaratibu wa utekelezaji wa miradi ya ujenzi kupitia usimamizi wa wataalamu waliopo katika taasisi husika."

Wakati utaratibu huo ukipamba moto katika utekelezaji wa miradi mingi ya serikali kwa sasa, wadau wa uwajibikaji, ikiwamo Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT), wamebaini kuwapo shida kwa serikali kutumia utaratibu huo kutekeleza miradi yake.

Uchambuzi wa Ripoti ya CAG kwa mwaka 2019/20 uliofanywa na Taasisi ya WAJIBU, umebaini upungufu katika utekelezaji wa miradi kwa kutumia utaratibu huo.

Taasisi hiyo ambayo Utouh ni Mkurugenzi Mtendaji, imebaini matumizi ya 'Force Account' yana dosari zinazojumuisha kukosekana kwa wataalamu wanaoweza kusimamia na kufuatilia kitaalamu miradi inayotekelezwa kwa utaratibu huo, hususani kwenye kamati za shule.

Taasisi hiyo inarejea kazi ya kusimamia miradi yenye thamani ya Sh. milioni 152 hadi milioni 259 iliyotekelezwa katika halmashauri za wilaya za Nzega, Nachingwea na Mpwapwa iliyofanywa na wahandisi wasio na sifa, hivyo kuwa na majengo yasiyo na kiwango kinachostahili.

Inasema hali hiyo inahatarisha maisha ya watumiaji wa majengo hayo na kusababisha kutokuwapo kwa thamani ya fedha ya miradi iliyotekelezwa.

Taasisi hiyo pia imebaini utaratibu wa Force Account unasababisha kutotumika kwa Mfumo wa Ununuzi wa Umma (TANePS) katika utekelezaji wa miradi.

Inafafanua kuwa hiyo inatokana na mwongozo wa Force Account kutokuweka mkazo wa matumizi ya mfumo huo.

"Mfano, watekelezaji wa miradi 23 iliyokaguliwa na CAG, hawakutumia TANePS," taasisi hiyo inabainisha katika Ripoti zake za Uwajibikaji Mwaka 2021.

WAJIBU pia inabainisha kuwa wasimamizi wa miradi inayotekelezwa kwa Force Account, hawazingatii Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2011 na Aya ya 4(1) ya Mwongozo wa Force Account uliotolewa na Ofisi ya Rais - TAMISEMI, unaozitaka taasisi zinazofanya ununuzi kuandaa takwimu za vifaa vitakavyotumika katika utekelezaji wa miradi.

"Kwa mfano, taasisi nunuzi 23 hazikufanya majadiliano ya punguzo la bei kabla ya kutia saini mkataba au kununua bidhaa," taasisi hiyo inabainisha kwa kurejea Ripoti ya CAG kwa mwaka 2019/20 iliyowasilishwa bungeni Aprili mwaka huu.ATHARI TATU

Taasisi hiyo inasema upungufu huo uliotokana na matumizi ya Force Account umesababisha athari, ikiwa ni pamoja na kuwapo kwa viashiria vya rushwa na udanganyifu katika mchakato wa ununuzi wa umma.

"Mfano, kuna shaka kutokuwapo ushindani katika ununuzi kwenye miradi 21 yenye thamani ya Sh. bilioni 2.13 inayotekelezwa kwa utaratibu wa Force Account kutoka na nyaraka za zabuni zilizowasilishwa kuwa na miandiko inayofanana na kutokuwa na mhuri wa mtoa huduma," taasisi hiyo inabainisha.

Athari ya pili ni kuwapo kwa upotevu wa fedha za umma, taasisi hiyo ikinyooshea kidole ununuzi uliofanyika kwa bei ya juu kuliko bei ya soko na kusababisha upotevu wa Sh. milioni 100.16 ambazo zingeokolewa kama Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2016, Kifungu cha 4A(3) ingezingatiwa.

Taasisi hiyo inaitaja athari ya tatu kuwa ni kukosekana kwa thamani ya fedha katika miradi iliyotekelezwa.

"Mfano, majengo kupata nyufa muda mfupi baada ya kukamilika katika Shule za Sekondari Berege na Mazae zilizoko Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa na Shule ya Sekondari Bulunde iliyoko Halmashauri ya Nzega Mjini," taasisi hiyo inabainisha katika ripoti yake hiyo.

WAJIBU inashauri mambo matatu kwa serikali ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kuandaa vigezo au mahitaji ya awali yatakayoziwezesha halmashauri kutekeleza kikamilifu miradi kwa utaratibu wa Force Account.

Katika hilo, taasisi hiyo inashauri PPRA kufanya tathmini ya uwezo wa halmashauri zote nchini kama zinaweza kuendelea kutekeleza miradi kwa utaratibu huo uliobainika kuwa na dosari.

Jambo la pili linalopendekezwa na taasisi hiyo ni halmashauri zitoe elimu kwa wasimamizi wa miradi inayotekelezwa kwa utaratibu wa Force Account, hususan kamati za shule, ili kuongeza ufanisi katika miradi.

"Tatu; serikali iboreshe muundo wa utendaji katika ngazi ya kata ili kuongeza wataalamu watakaoshirikiana na Ofisa Mtendaji wa Kata katika kusimamia miradi ya maendeleo.

"Baadhi ya wataalamu wanaokosekana katika ngazi ya kata ni kama vile ofisa TEHAMA, mhasibu na mhandisi," taasisi hiyo inabainisha.

Ripoti ya taasisi hiyo kuhusu ufanisi, rushwa na ubadhirifu, imechambua ripoti saba za ufanisi kati ya 15 zilizotolewa na CAG kwa mwaka 2019/20.

Mbali na utaratibu wa Force Account, maeneo mengine yaliyochambuliwa na taasisi hiyo ni pamoja na udhaifu katika mifumo ya TEHAMA nchini na utoaji usioridhisha wa vitambulisho vya taifa.

Mengine ni: Uchafu na uchakavu katika masoko ya chakula nchini; upungufu katika ukusanyaji wa kodi; viashiria vya rushwa na ubadhirifu; mashirika yaliyofuta madeni bila idhini ya Wizara ya Fedha na Msajili wa Hazina; na matumizi yasiyokuwa na tija katika taasisi za serikali ikiwamo Sekta ya Utalii.

Habari Kubwa