Magari ya zimamoto kuundwa Tanzania

20Sep 2016
Margaret Malisa
Kibaha
Nipashe
Magari ya zimamoto kuundwa Tanzania

HISTORIA imeandikwa. Tanzania imejenga kiwanda cha kuunganisha magari ya kuzimia moto ili kukabiliana na upungufu mkubwa wa magari hayo nchini. Uzalishaji wa magari hayo unatarajiwa kuanza Novemba mwaka huu.

Ujenzi wa kiwanda hicho kilichoko Mlandizi unatekelezwa na kampuni ya Equator SUMAJKT iliyoko Ruvu mkoani Pwani, baada ya kuingia makubaliano ya kuhamisha teknolojia ya kuunda magari ya zimamoto na kampuni iitwayo St Auto ya Russia.

Kampuni ya Equator SUMAJKT ambayo inatokana na ubia kati ya Shirika la uzalishaji Mali la JKT (SUMAJKT) na kampuni binafsi ya Equator Automech.

Kimsingi Suma JKT ni kamouni ya umma inayomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa(JKT) na Equator Automech inamilikiwa na Watanzania, baadhi yao ni wastaafu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Kwa mujibu wa makubaliano hayo kampuni hiyo ya ubia- Equator SUMAJKT itaunganisha magari ya zimamoto ambayo yatauzwa nchini na katika baadhi ya nchi za Afrika, huku kampuni ya St Auto ambayo ni mbia wa Equatormech ndiye, mwakilishi rasmi wa soko la magari hayo barani Afrika .

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni Equator SUMAJKT Robert Mangazeni anasema, magari hayo yataunganishwa kwa kutumia vigezo vya viwango vya kimataifa huku chassis zitakazotumika ni za aina mbalimbali kutoka mataifa tofauti.

Takwimu za matukio ya moto nchini zinabainisha kuna mahitaji makubwa ya magari ya zimamoto ili kukabiliana na majanga hayo.

Majanga ya moto hayachagui sehemu. Huyakumba maeneo ya majiji, shule, viwanja vya ndege, mabenki, bandari viwanda, maghala, masoko, mbuga za wanyama na maeneo mengine.

Kwa hiyo hatua hiyo ya ujenzi wa kiwanda hicho, itasaidia sana nchi kukabiliana kikamilifu na majanga ya moto ambayo yamekuwa yanateketeza mali na kusababisha vifo au kudhuru mwili.

Miongoni mwa matukio ya ajali ya moto ambayo yameikumba nchi hivi karibuni ni yale la kuungua kwa mabweni ya shule za sekondari katika mikoa mbalimbali.

Mkoa wa pwani una magari matatu ya kuzimia ikiwa ni pungufu ya magari sita.

Mkurugenzi Mangazeni anasema St. Auto itakuwa na jukumu la kuunda vifaa mbalimbali vya kuzimia moto ili viunganishwe kwenye chassis za ukubwa na aina mbalimbali kulingana na mahitaji ya mteja.

" Tangu nchi ipate Uhuru, hatujawahi kuwa na kiwanda wala karakana za kutengeneza magari ya kuzimia moto yanapoharibika au kuyahudumia kwa kiwango cha kuridhisha. Kazi hiyo, hufanywa na kampuni za kigeni.Kwa mara ya kwanza Equator SUMAJKT tutafanya Kazi hiyo, tunayetengeneza pia kuyahudumia yatapoharibika, " anasema Mangazeni.

Mkurugenzi huyo anasema, watakuwa na uwezo wa kutoa huduma na matengenezo kwa magari ya zimamoto ya aina mbalimbali katika majiji, manispaa, miji, wilaya na taasisi mbalimbali za serikali na makampuni binafsi.

Kampuni hiyo, inawaalika wateja wenye magari ya zimamoto ya zamani yaliyoharibika yafanyiwe matengenezo na kuyarejesha katika hali nzuri badala ya kuyauza kama vyuma chakavu.

“Tuna uwezo wa kumuunganishia mteja mwenye mahitaji maalumu ya mitambo ya magari ya zimamoto kama bandari, endapo atakuwa na chassis zake maalumu za aina yoyote na ukubwa wowote,” anafafanua.

Magari ya kuzimia moto yanatumika nchini kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, yametengenezwa kwa ukubwa kulingana na mahitaji ya nchi iliyotengeneza bila ya kuzingatia miundo mbinu ya nchi yetu hivyo wakati mwingine yamekuwa yakishindwa kufika kwenye tukio kutokana na ukubwa wake, ufinyu ama ubovu wa barabara.

“Kiwanda chetu kina uwezo wa kutengeneza magari ya kuzimia moto kulingana na mahitaji ya sehemu husika kwa ukubwa wowote na hata kama mtu ama taasisi kwa wenye magari mabovu ama taasisi zenye maboza ama magari mabovu wayalete, tutawabadilishia kwa gharama nafuu”, anasema Mangazeni.

Mangazeni anasema, kiwanda pia kitakuwa na uwezo wa kuunganisha magari na matrekta kwa kuhamisha teknolojia kutoka escorts farmtrac India na farmtrac Europe (Poland) kwa ajili ya masoko ya Tanzania , Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Lengo la kiwanda hicho ni kuunganisha magari mbalimbali yakiwamo ya kuzimia moto, mabasi, matrekta na zana za kilimo.

Miongoni mwa zana za kilimo zitakazozalishwa nchini zinalenga kusaidia kuchochea ukuaji wa sekta ya kilimo na kukua kwa uchumi wa Tanzania hata kuwezesha azma halisi ya Kilimo Kwanza kutimia.

“Tutashirikiana na viwanda vya nchini ili kuzalisha vipuli mbalimbali vya magari ya zimamoto, matrekta na zana za kilimo. Viwanda vya kuzalisha vipuli vitateuliwa kwa kuzingatia viwango vya ubora. Tunatarajia kushirikiana na kampuni ya Automech, kiwanda cha TATC, Nyumbu, SIDO, na vinginevyo,” anasema.

Mkurugenzi huyo anasema kwa upande wa matrekta kwa kuanza wataunganisha matrekta ya Escort Farmtrac India na Farmtrac Europe (Poland).

Anasema awali hapa nchini hapakuwa na watu wenye ujuzi wa kutengeneza matrekta yanapoharibika hivyo kupitia kiwanda hicho watakarabati matrekta yote mabovu na watatoa mafunzo kwa madereva na mafundi ili waweze kudhibiti uharibifu wa matrekta uliokuwa ukijitokeza kwa sababu ya upungufu wa ujuzi wa matumizi sahihi ya matrekta na zana za kilimo.

Kimsingi anasema kuwa, wataalamu kutoka nje kwa ajili ya ufungaji wa mitambo wameshafika na hatua za awali za ujenzi wa majengo ya kiwanda hicho na ufungaji wa mitambo na vifaa umeshaanza. Hadi sasa zimetumika Sh. Bilioni mbili na hadi ukamilishwaji wa kazi hiyo gharama halisi zinatarajia kufikia Sh. bilioni tatu.

Mkurugenzi anasema, kiwanda kitakapoanza kufanya kazi, kitakuwa na uwezo wa kuajiri wafanyakazi zaidi ya 100 huku idadi hiyo itaongezeka kadri uzalishaji utakavyokuwa unaongezeka.

Anaiomba serikali, kushirikiana na kampuni hiyo hasa katika kipindi hiki cha sera ya ujenzi wa viwanda nchini, kwani lengo la kiwanda hicho ni kuhakikisha kuwa siku za usoni Tanzania inapiga hatua kwa kutengeneza magari yake yenyewe badala ya kuunganisha kama ilivyo sasa.

Habari Kubwa