Magufuli anapowamaliza wasioutaka Muungano

03May 2017
Gaudensia Mngumi
Dar es salaam
Nipashe
Magufuli anapowamaliza wasioutaka Muungano

MAADHIMISHO ya miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ya mwaka 2017, yamemaliza tumaini la kubadilisha muundo wa Muungano na ndoto za kuunda serikali tatu, kuufanya uwe shirikisho ama wa kimkataba.

Hii ni kwa sababu Rais Dk. John Magufuli, katika hotuba yake aliyotoa Dodoma Jumatano, iliyopita, ameweka wazi kuwa wenye nia za kuwa na sura nyingine ya Muungano hawatapewa nafasi hivyo, wauache ukae ulivyo.

Anaahidi kuwa ataulinda kwa nguvu zake zote na iwapo atatokea mjanja kutaka kuuvunja anaanza kuvunjika yeye kwanza, kabla hajatimiza azma hiyo.

Kwa hiyo, hatataka kusikia habari za Muungano wa mkataba, serikali tatu, shirikisho ama kuuvunja kama ambavyo wapo wanasiasa, wasomi na wanaosimamia maoni ya wananchi yaliyotolewa kwenye maandalizi ya rasimu ya katiba mpya.

Lengo la makala hii si kuzungumzia aliyosema Rais mjini Dodoma wiki iliyopita, bali kuangalia namna dunia ya leo inavyohitaji kuendeleza miungano na kuachana na hisia za ama kuuchukia au kuulaumu Muungano na Ushirikiano.

Hisia za kuwa na umoja ziko miongoni mwa wananchi wa madola makubwa ambayo yamekomaa kiuchumi, kisiasa na kiteknolojia.

Hata hivyo, dunia ya leo inajadili kuwa na mtangamano na ushirikiano wa kikanda, kwa mfano madola makubwa ya Ulaya kama Ujerumani, Ufaransa, Uholanzi na Hispania yanaendelea kujishikilia kwenye Umoja wa Ulaya (EU), licha ya kwamba yana uchumi mkubwa unaokidhi kujitegemea.

Pamoja na Uingereza kujitoa, hayajatetereka sana. Wachambuzi wa masuala ya siasa wanaona kuwa, tangu mwanzo Uingereza ilikuwa ni mshirika wa ‘mguu mmoja nje” na mwingine ‘ndani.’ Kwa mfano, licha ya EU kuunda sarafu ya EU mwanzoni mwa mwaka 2000, Waingereza hawakuwa tayari kuwa na sarafu moja, walibakia na Paundi yao.

Wakati hayo yanatokea, madola makubwa na yenye uchumi mkubwa ya Ujerumani na Ufaransa pamoja na Uholanzi, yaliachia sarafu zake kuingia kwenye Euro, ili kuudumisha umoja.

Inashangaza Watanzania kuupinga Muungano na kutaka kuwapo serikali tatu, mara uwe wa mikataba na wengine wakitaka iitishwe kura ya maoni kuamua uondoke ama ubakie.

Kwa kurejea tena kwa Waingereza, ambao wakati mwingine hutumiwa kama rejea ya kukataa Mungano na EU, waliendeleza ubabe hata kwenye masuala ya viza na uhamiaji kwa kukataa visa ya Schengen, inayotumika kuingia kwenye nchi za umoja huo.

Rais Dk. Magufuli anaona kuwa, dunia ya zama hizi siyo ya kutaka kubomoa au kutengana. Ndiyo maana, katika jitihada za kushirikiana, Tanzania ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC), pia imo kwenye ushirikiano wa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

KUUNGANISHWA KIHISTORIA
Ni wazi kuwa, panapokuwapo muungano uwe wa EU au wa Tanganyika na Zanzibar, kuna mambo ambayo historia inayaunganisha.

Kwa mfano, Ulaya inaunganishwa na kumbukumbu za vita vikuu vya dunia na hasa Vita vya Pili vya Dunia vilivyoangusha dola la Mjerumani na Uingereza kutwaa enzi.

Wanaungana ili kulinda na kuepuka uhasama, wanataka kudumisha amani na kuendeleza mshikamano miongoni mwao. Ni ukweli kwa vile tangu vita hivyo, hakujawepo na mapigano na uhasama miongoni mwa mataifa ya Ulaya.

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, unaunganishwa na mizizi ya kihistoria; utumwa, ukandamizaji na unyonyaji wa mabeberu.

Mbegu za ushirikiano zimepandwa kihistoria. Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume wanaunganishwa kwenye kitovu cha machungu ya ubeberu wa kiarabu, utumwa na ukandamizaji, uliowafanya kuanzisha vyama vya ASP na TANU, kutetea maslahi ya weusi waliochukuliwa ni watu wa ‘daraja la tatu.’

Muungano ulilenga kuwa nguvu za kuyalinda mapinduzi machanga ya Zanzibar, yaliyohitaji dola lenye msuli kijeshi na usalama wa taifa, kudhibiti chokochoko za wanaopinga serikali ya Wazanzibari (Waafrika badala ya Waarabu).

Umoja wa EU ni chipukizi linalokomaa zaidi kwa sababu ya kifo cha Jamhuri za Umoja wa Kisovieti zilizokuwa zinaongozwa na Urusi ambazo zilianguka kuanzia 1994. EU kihistoria inafahamu kilichoiua Urusi, hivyo madola hayo yanajizatiti kuongeza dhamira ya kudumisha umoja wa muungano wa Ulaya.

KUBOMOA NI HISIA ZA SIASA

Wanachama wa EU wanafahamu umuhimu wa umoja tena wakiangalia Urusi ilivyoparaganyika. Ni wazi EU inadumu kwa sababu ya misimamo ya viongozi wanaotaka iendelee mmojawapo ni Kansela wa Ujerumani Angela Markel.

Kadhalika, Rais Dk. Magufuli na Dk Ali Mohamed Shein, wakifuata nyayo za wastaafu Jakaya Kikwete, Benjamin Mkapa na Ali Hassani Mwinyi, kwa Tanzania Bara na Amani Abeid Karume, Dk. Salmin Amour, Idris Abdul Wakili, Ali Hassan Mwinyi na Aboud Jumbe Mwinyi, hawako tayari kuchezea Muungano. Wanayafahamu mazuri ya Muungano na utamu wa kuwa ndani ya ushirika.

Ni kazi ya wanasiasa kulinda na kupambana na fikra mchanganyiko zikiwamo za kisiasa, Kiuchumi, kisaikolojia, kijiografia zinazoelekeza ama kuvunja Muungano kwa sababu wanafahamu kinasababisha watu kuukataa au kuukosoa.

KUVUNJA UMOJA NI LAANA?

Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kuonyesha laana inayotokana na ubaguzi na kuvunja umoja, akitoa mfano wa sumu ya ubaguzi inayoambatana na kujitambulisha kwa ukabila na utaifa licha ya kuwa wote ni Watanzania.

Anaonya kuwa, iwapo kuna hisia za kujiondoa kwenye Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zitaanza kusikika kelele za “Sisi Wazanzibari, Sisi Wazanzibara, Sisi Wapemba …. Na kauli nyingine za kujitenga. Yote haya hayajengi.”

Ukiangalia, Sudan ya Kusini ni taifa lililojiondoa kutoka Sudan ya Khartoum, lakini kinachotokea leo naweza kukifananisha na laana ya kujitenga, kuongezeka maafa kama vifo, vinavyotokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe, wakimbizi na umaskini miongoni mwa raia wa Sudan Kusini ndicho kinachojiri.

Viongozi Salva Kiir Mayardit na Makamu wake Riek Machar, hawaelewani na huenda watu wanalalamikia hatua ya kujiondoa kwenye taifa la Sudan.

Sudan Kusini haina utulivu tena inakuwa sehemu ya mataifa yenye vurumai barani Afrika kama ilivyo Libya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Japo kuna wanaounga mkono kujitenga kwa mataifa hayo kutokana na chuki, ubaguzi wa rangi, dini na kunyimwa fursa za kuongoza serikali kwa watu weusi wanaoishi upande wa kusini, kujiondoa kwenye utawala wa Khartoum na kuunda serikali ya Juba kumeleta maafa makubwa kwa raia wa Sudan Kusini.

Ndiyo maana changamoto kama hizi zinawafanya marais wa Tanzania na Zanzibar kuamua kuulinda Muungano na sasa Rais Magufuli anasema atakayetaka kuuvunja anavunjika kwanza.

Wakati Rais anawaonya wenye kiu na ndoto za kuvuruga Muungano wasitamani kufanya hayo, ni wazi kuwa haiwezekani kuuacha ubaki kama msahafu.
Watanzania wapewe jukwaa la kuujadili ili kuuboresha, kuukosoa, kuufanya wa wananchi zaidi badala ya viongozi waasisi au wanasiasa.

Zinahitajika juhudi za kuufuatilia mwenendo wa Muungano, kuibua changamoto, kushauri na kuleta mambo mapya yanayoleta tija kiuchumi, kisiasa na kiteknolojia.

ANGALIZO
Ni wakati wa kuimarisha Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano ili iwe taasisi inayoshughulikia Muungano kikamilifu. Ianzishe utaratibu wa kutumia utaalamu na ubobezi kutoka kwa viongozi watangulizi kuanzia Marais wastaafu wa Bara na Zanzibar, mawaziri viongozi na wakuu, wanasheria wa serikali,wabunge, magavana wa benki wasomi kushauri jinsi ya kuboresha taasisi hii.

Ofisi hii ya Makamu wa Rais kwa kutumia wataalamu na wana siasa hawa ishughulikie changamoto kubwa za Muungano, iitoe ufumbuzi na iwe ni jukwaa la kupokea maoni ushauri na miongozi ya kuboresha ushirikiano huu.

Muungano usiwe wa kisiasa zaidi ulinde maslahi ya pande zote, kiuchumi, uongeze furaha kwa Watanzania na usichukuliwe kama kitu cha kulazimishana.