Magufuli na harakati za ukombozi wa pili

09Oct 2019
Reubeni Lumbagala
Dodoma
Nipashe
Magufuli na harakati za ukombozi wa pili

DESEMBA 9, 1961, Tanzania ilipata uhuru wake kutoka katika mikono ya wakoloni.

Rais John Magufuli, picha mtandao

Huu ulikuwa ni ukombozi wa kwanza wa kisasa ambao ulileta furaha na matumaini mapya kwa Watanganyika walioishi kwa miaka mingi katika utumwa na manyanyaso kutoka kwa wakoloni.

Baada ya Tanzania kutoka katika minyororo ya ukoloni na kupata ukombozi wa kwanza, jitihada za kuleta ukombozi wa kiuchumi (ukombozi wa pili) zilichukua nafasi yake.

Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Jemadari wa vita vya uchumi Rais John Magufuli imepania kwa vitendo kuhakikisha mapambano ya ukombozi wa pili wa kiuchumi yanafanikiwa kwani ndiyo malengo na dira ya nchi katika kuleta ustawi na ukuaji wa maendeleo ya kweli.

DIRA YA MAENDELEO YA UCHUMI WA VIWANDA

Rais Magufuli amesimama imara katika kuhakikisha dira ya maendeleo ya nchi yetu ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 inafanikiwa.

Ndiyo maana serikali ikaweka mazingira mazuri kwa ajili ya wawekezaji wa ndani na wa nje ya nchi kuwekeza nchini kwa kujenga na kuendeleza viwanda vikubwa, vya kati na vidogo ili kufikia dira hii. Ujenzi wa viwanda zaidi ya 3000 kote nchini umefanyika ambapo vijana wengi wamepata ajira za kudumu na za muda, hali iliyoboresha maisha ya vijana hao.

Wakulima na wafugaji wadogo na wakubwa wameweza kupata masoko kwa ajili ya kuuza mazao yao ambayo hutumika kama malighafi za kulisha viwanda hivyo.

Hii imesaidia kukuza sekta ya kilimo na mifugo kwa kiwango kikubwa.

Pia, serikali imeweza kukusanya kodi kupitia viwanda hivi, hali inayochagiza ongezeko la mapato ya nchi na hivyo mapato hayo kutumika katika ukuzaji wa sekta nyingine kama elimu, nishati, afya, maji, miundombinu, mawasiliano, kilimo nk.

Mwelekeo wa kuifikisha Tanzania katika nchi ya viwanda na ya uchumi wa kati unaenda vizuri, na hakika tutafika kama nchi,

UBORESHAJI MIUNDOMBINU YA USAFIRISHAJI

Ukombozi wa pili wa kiuchumi unakwenda sambamba na ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya barabara, reli, madaraja na vivuko.

Kumekuwa na kasi kubwa ya ujenzi wa miundombinu hii kote nchini ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Wakulima, wafanyabiashara na wajasiriamali wamewekewa mazingira rafiki kwa ajili ya usafirishaji wa mazao na bidhaa zao ili kupunguza gharama kubwa za usafirishaji.

Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) na Wakala wa Barabara za vijijini (Tarura) wanafanya kazi kubwa katika usimamizi wa ujenzi na uboreshaji wa barabara.

Aidha, ujenzi wa reli ya mwendo kasi (SGR) unaendelea ambapo wananchi wa mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro wataweza kusafiri kwa urahisi na kuokoa muda wa safari.

Pia, reli katika mikoa ya Tanga-Kilimanjaro imekamilika ambapo wafanyabiashara wanaweza kusafirisha bidhaa zao kwa bei nafuu.

Ujenzi wa meli katika mikoa ya kanda ya ziwa na maeneo mengine ya nchi yetu unaendelea ili kuwarahisishia wananchi usafiri huo.

Usafiri wa anga nao umeboreshwa kwa kiwango kikubwa, ambapo serikali imeboresha na kujenga viwanja vingi vya ndege katika mikoa mbalimbali.

Aidha, serikali imenunua ndege kwa ajili ya kuwahudumia abiria wa ndani na wa nje ya nchi katika safari zao za kikazi, kibiashara, kiutalii na za kimapumziko.

Mapato yanayopatikana katika usafiri wa anga unachangia ukuaji wa uchumi na hatimaye kuchagiza ukombozi wa pili.

MRADI WA UMEME WA JULIUS NYERERE

Kutokana na ongezeko la mahitaji ya nishati ya umeme katika kuendesha shughuli mbalimbali za kijamii na za kiuchumi, Rais Magufuli aliamua kutimiza ndoto za Mwalimu Nyerere za kujenga Bwawa kubwa kwa ajili ya kufua umeme wa maji katika Mto Rufiji.

Mradi huu utagharimu dola za Marekani bilioni 2.9 sawa na shilingi trilioni 6.5 za Kitanzania na kufanikisha uzalishaji wa Megawati 2115.

Megawati 2115 ni kiasi kikubwa kuliko kinachotumika sasa kwa nchi nzima.

Umeme huu utamaliza kabisa mahitaji ya nishati ya umeme. Kama hiyo haitoshi, kukamilika kwa mradi huu kutaiwezesha Tanzania kuuza umeme kwa Watanzania kwa bei nafuu na kuziuzia nchi nyingine.

Hivyo basi, mradi huu ni utekelezaji wa dira ya maendeleo ya kuhakikisha shughuli za kiuchumi hasa za viwandani na huduma nyingine za kijamii kama afya na elimu zinapata nishati ya umeme ili kuongeza uzalishaji.

KUONGEZA MAKUSANYO NA MATUMIZI BORA YA MAPATO

Ili kufikia maendeleo na ukombozi wa kiuchumi, ni lazima kodi ikusanywe kutoka kwa wananchi.

Tangu serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, kumekuwa na ongezeko la makusanyo ya kodi kutoka sh. bilioni 800 hadi trilioni 1.43.

Mafanikio haya yametokana na nia njema ya Rais Magufuli katika kuhakikisha kodi inakusanywa na kutumika katika uwekezaji wa miradi mikubwa na midogo ya maendeleo kwa ajili ya ustawi wa wananchi na nchi kwa ujumla wake.

Kutokana na mafanikio ya makusanyo ya kodi, serikali imeongeza uwezo wake wa utekelezaji wa shughuli za kimaendeleo.

Ukombozi wa pili wa kiuchumi ndiyo ajenda ambayo wananchi wanaitaka kuisikia na kuona serikali yao ikiisimamia kwa vitendo kwani ni katika ukombozi huu ndipo yalipo maendeleo ya kweli ambayo yanawagusa wananchi moja kwa moja. Tafakari.

Mwandishi ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma.

Maoni: (+255) 764 666349

Habari Kubwa