Mahafali ya Kwanza Baraza la Wauguzi tangu 1953

25Feb 2021
Yasmine Protace
Kibaha
Nipashe
Mahafali ya Kwanza Baraza la Wauguzi tangu 1953

WAKUNGA na wauguzi wanafahamika kuwa watu muhimu katika sekta ya afya, kutokana na kazi wanazozifanya.

Wauguzi wahitimu katika mahafali yao, Kibaha mkoani Pwani. PICHA: MT ANDAO.

Kila hospitali au vituo vya afya, kuna watu wanaojulikana kama wakunga ambao ni mahususi kwa uzazi na wengine wauguzi kwa huduma ya umma.

Serikali inasema kazi yao ni kuhakikisha wanatoa huduma za afya kwa wageni waliofika tu ambao wamefika kupata huduma hiyo.

Ni kauli iliyowasilishwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Dorothy Gwajima, katika hotuba yake iliyosomwa na Mkurugenzi wa Idara ya Uuguzi na Ukunga, Ziada Sellah, kuwasajili wauguzi na wakunga wapya.

Akizungumza katika katika hafla ya kwanza ya kuwasajili wauguzi na wakunga wapya iliyofanyika kwenye Kituo Cha Maendeleo ya Uuguzi na Ukunga, mjini Kibaha, anasema ni wajibu wao kufanya kazi kwa weledi ili kuhakikisha jamii inanufaika na huduma hizo.

Ziada anasema wanataaluma hao wanapaswa kuzingatia viapo vya taaluma walizonazo na kutoa huduma kwa kujali utu, heshima na upendo kwa wagonjwa wanaowahudumia katika vituo vyao vya kazi.

"Tukio hili litasaidia kutoa msisitizo kwa wanataaluma kutambua wajibu wao katika utoaji wa huduma huku wakizingatia maadili ya taaluma zao.

“Kitendo hiki kilitakiwa kutekeleza kipindi kirefu kilichopita na ni vyema kikatekelezwa na taaluma zote za sekta ya afya nchini, ili kuwafanya wahitimu kuheshimu taaluma zao," anasema.

Katika kuboresha na kutekeleza majukumu ya Baraza la Wauguzi na Wakunga nchini, ziada amelitaka kuzingatia ubora wa stadi na maadili ya taaluma, ili kushuhudia mabadiliko makubwa ya ubora wa huduma za afya nchini.

"Tumeendelea kushuhudia changamoto nyingi za huduma zinazotolewa bila kuzingatia maadili ikiwa ni pamoja na kunyanyaswa wateja, natoa msisitizo tena kwa wanataaluma wote wa sekta ya afya zingatieni viapo vyenu," anasema Ziada.

Sellah amewahimiza viongozi katika ngazi za mikoa na hospitali za rufani, ambazo wamepewa mamlaka na Sheria ya Uuguzi na Ukunga ya Mwaka 2010, kuchukua hatua za awali, panapobainika kuna upungufu katika utoaji wa huduma.

"Tekelezeni majukumu yenu kwa haraka iwezekanavyo na kisha mtoe taarifa kwa Baraza la Uuguzi na Ukunga makao makuu kwa hatua zaidi.

“Wateja wanapenda kushuhudia haki inapatikana mapema, kuchelewa kuchukua hatua panapotokea upungufu kunaleta picha mbaya kwa wateja na kuleta taswira kuwa kuna kulindana au udhaifu katika usimamizi wa maamuzi,"anasema.

Ziada analipongeza baraza hilo kwa kuandaa tukio hilo na kuwahimiza liwe endelevu kwa wanataaluma kuelewa maana ya baraza na majukumu yake, pia akiwasisitiza kuhusu maadili ya taaluma yao.

Mwenyekiti wa Baraza la Uuguzi na Ukunga nchini,  Abner Mathube, anasema sheria iliyounda baraza hilo ilitungwa kwa lengo la kuhakikisha Watanzania wanapata huduma za uuguzi na ukunga zilizo salama.

Hivyo, baraza hilo limechukua hatua ya kuhakikisha linawasajili wataalamu wenye sifa za kitaaluma na kuwachukulia hatua za kisheria, wote wanaotoa huduma chini ya viwango vilivyowekwa.

Wakati huo huo Kaimu Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga, Happy Masenga, anasema baraza linahakikisha leseni ya kutoa huduma za kitaaluma za uuguzi inatolewa kwa waombaji waliopitia mafunzo yaliyokubalika, kutoka vyuo vinavyotambulika na kufaulu mitihani ya usajili inayoendeshwa na baraza.

Masenga anasema, tangu mwaka 2014, baraza hilo limekuwa likiendesha mitihani ya usajili na leseni, ili kupima umahiri wa wahitimu kwa lengo la kujiridhisha kama wanao uwezo wa kutoa huduma salama kwa wateja na hadi sasa wahitimu 30,715 wamekwishaifanya mitihani hiyo.

Ni mahafali yaliyoandaliwa na Baraza la Uuguzi na Ukunga nchini na yamefanyika kwa mara ya kwanza tangu baraza hilo kuanzishwa mwaka 1953.

Ndani ya hafla hiyo, kuna jumla ya wauguzi na wakunga 839 walihitimu masomo ya uuguzi na ukunga katika ngazi mbalimbali na kufaulu mitihani ya usajili na leseni iliyofanyika Novemba, 2020.

Habari Kubwa