Mahindi ya njano na viazi lishe yabadilisha afya Kilosa na Gairo

06Jul 2017
Beatrice Philemon
Dar es salaam
Nipashe
Mahindi ya njano na viazi lishe yabadilisha afya Kilosa na Gairo

KILIMO cha aina yake kinacholeta mapinduzi ya lishe kimechachamaa katika wilaya za Gairo na Kilosa, kwa jumla ya wakulima 1907 kutoka vijiji 10.

Ni hatua ya aina yake inayoelezwa italeta mabadiliko yake hata kwa kuongeza kipato katika ngazi ya kaya. Yote ni zao la mafunzo waliopata kuhusu kilimo hicho.

Kwa nafasi ya pekee ya afya, inatarajiwa itachangia kupatikana virutubishi vingi vya kusaidia kupunguza utapiamlo katika jamii ambazo zina usugu na inachangia udumavu.

Viazi na Mahindi Lishe ni nini?

Si jamii yote ya Kitanzania inayoelezwa kuwa na uelewa mzuri kuhusu viazi lishe au mahindi lishe na nafasi yake katika afya ya mwanadamu, hususan watoto wadogo, kinamama na wajawazito.

Viazi lishe vimo katika kundi la viazi vitamu vyenye rangi ya njano ambavyo vina kiwango kikubwa cha lishe.

Pia, mahindi yamo katika aina ya mahindi ya njano, yenye virutubishi vingi kama vile wanga, vitamin B, protini, madini chuma na vinginevyo vya kujenga mwili.

Wenye mradi

Ofisa Lishe wa Ushirika wa Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (Sugeco), Jorenta Joseph, anasema baada ya kuona wakazi wa wilaya hizo wana upungufu wa Vitamini A na baadhi ya vijiji kuna utapiamlo mkubwa, Sugeco, iliamua kupeleka Mradi wa Kuboresha Lishe na Kuongeza Kipato kwa Ngazi ya Kaya katika wilaya ya Gairo na Kilosa.

Anasema lengo ni kuongeza vyakula vitavyosaidia kupunguza matatizo yatokanayo na upungufu wa Vitamini A na Protini katika jamii lengwa.

Mpaka sasa mradi huo upo katika vijiji 10 anavyovitaja kuwa ni; Zombo, Magubike, Kiegeya, Mtumbatu, Msolwa, Kisanga, Ulaya-kibaoni, Nyameni, Ngiloli na Ibuti.

Anasema mradi unatekelezwa na Sugeco na kusimamiwa na kampuni ya Farm Afrika-Tanzania na unafadhiliwa na Big Lottery.

Kupitia mradi huo, wakulima walifundishwa mbinu bora za kilimo ili kusaidia wakulima wadogo katika vijiji hivyo, kuongeza uzalishaji mazao ya chakula yenye virutubisho vingi na biashara, kwa ubora zaidi. Mazao yaliyoainishwa katika mradi ni viazi lishe, mahindi lishe, alizeti, ufuta na maharage.

“Mpaka sasa wakulima katika vijiji hivi wameanza kulima viazi lishe, mahindi lishe, ufuta, alizeti na maharage ili kuboresha lishe na kuongeza kipato kwa ngazi ya kaya,” anasema.
Matokeo yakoje?

Katika maeneo ambayo wakulima wameanza kuvuna mahindi lishe, hali ya watoto kiafya katika wilaya za Gairo na Kilosa, inaelezwa kuanza kuboreka baada ya Sugeco kutoa elimu inayohusu kilimo bora, kuhamasisha wakulima wa mazao yenye virutubishi vingi na kuanza kuyatumia mazao hayo.

Vilevile, asilimia kubwa ya wananchi katika vijiji hivyo, sasa ni walaji wakubwa wa viazi lishe na mahindi lishe, badala ya kubaki na biashara ya mazao pekee.

Jorenta anaeleza kuwa viazi lishe vina Vitamini A vinavyosaidia kuimarisha afya ya ngozi, macho, ubongo na kinga mwilini.

Mengine ni ukuaji mifupa na mfumo wa uzazi, unatenganisha na kutofautisha chembe hai, huku ikizingatiwa kwamba viazi lishe vichangie Vitamin B, C, E na K zinazosaidia kinga mwilini.

Manufaa mengine ni kupatikana wanga, na chanzo muhimu cha Vitamini A, B na C wenye kiwango kikubwa cha protini.

Jorenta anasema, ukosefu wa vitamini A unasababisha udumavu wa watoto wadogo na kukaribisha magonjwa nyemelezi kwa watoto, pia upofu muda wa usiku.

“Ili vitamin A ifyonzwe vizuri mwilini, ni lazima kuwapo kiwango kidogo cha mafuta, kwa sababu Vitamini A inayeyuka kwenye mafuta,” anasema.

Matokeo chanya

Jorenta anasema kuwa, majani ya viazi lishe ni chanzo kikuu cha madini ya chuma, yanayosaidia uzalishaji wa chembe nyekundu za damu na kuchangia kupunguza vifo na hasa kwa wajawazito.

“Ninafurahi sasa hivi katika baadhi ya vijiji kama vile kijiji cha Zombe, wananchi wameanza kutumia majani ya viazi lishe na mahindi lishe, kula ugali na kunywa uji,” anasema na kuongeza:

“Matokeo ya mazao hayo wameyaona, kwa sababu wanasema macho yao yameanza kuona baada ya kuanza kula majani ya viazi lishe na mahindi lishe.”

Anasema, awali dhana iliyojengeka ni kwamba mahindi ya njano yapo kwa ajili watu masikini, kumbe si sahihi.

“Mpaka sasa kuna baadhi ya wakulima wamevuna mahindi lishe kuanzia gunia sita mpaka saba kutoka kwenye ukubwa wa robo ekari,” anasema.

Mwakilishi huyo anataja faida za mahindi lishe ni kuwa na virutubishi vingi kama vile wanga, vitamini A, B, protini, madini chuma na vingine muhimu kwa afya.

Anasema mfumo wa uzalishaji mazao hayo, ni kwamba kila kijiji kina wakulima 120 wanaolima viazi lishe, ili kuongeza upatikanaji katika ngazi ya kaya na ni kundi lililokwishapewa mbegu za mahindi lishe (mahindi ya njano).

Mafunzo yanavyoendeshwa

Mradi ulianza kupitia mafunzo elekezi kwenye vituo vinane kwenye maeneo ya mradi, ikitumia wahudumu kutoka vinane vya afya wanaoelimisha umuhimu wa viazi lishe na mahindi lishe.

Kimsingi, ili Vitamini A ifyonzwe, mwili unahitaji kuwa na mafuta na hicho ndicho msingi wa kuhamasisha kilimo cha zao la ufuta.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ngiloli katika Kata ya Chigela, Adam Magawa, anafafanua: “Mradi huu tuliupokea vizuri sana katika kijiji chetu. Kabla ya kulima mahindi lishe na viazi lishe, nilienda Sugeco mwaka 2016 kupata mafunzo juu ya kilimo bora cha mazao haya na baada ya hapo, nilirudi kijijini, nikaanza kuwaelimisha wananchi kupitia mikutano yetu ya maendeleo ya vijiji na mimi kuanza kulima.

“Katika kijiji chetu, mradi huu umefanya vizuri kwa asilimia 98, kwa kushirikiana na Sugeco na maofisa kilimo.

“Wakulima walifuata mbinu zote za kilimo walizofundishwa na ushauri waliopewa na hivi sasa, baadhi ya wakulima wanatarajia kuvuna mahindi kuanzia gunia saba hadi nane, kwenye robo eka ya mahindi ya lishe.”

Magawa anasema, kwa sasa watu wengi wameupenda mradi huo na wanazalisha mazao hayo kwa mafanikio makubwa, huku wakiiomba Sugeco iwatafutie soko, kwa sababu matarajio ni uzalishaji kuwa mkubwa.

“Tunahitaji soko kwa sababu asilimia 78 ya wananchi wanatarajia kujikita katika kilimo cha mahindi lishe na viazi lishe, kwa sababu mradi umefungua njia kwao na kusaidia wakulima kujikita katika kilimo cha kisasa,” anasema.

“Mbegu za viazi lishe tulizopata toka Sugeco aina ya ‘Kabode na Jewelis 1219’ zinavumilia ukame, zinazaa kwa wingi,” anasema.
Kutoka kwa mkulima

Fenehas Mohamed, ni mkulima mwenye familia ya watoto watano. Anasema alipata mbegu ya mahindi lishe kutoka Sugeco na alianza kulima mahindi hayo katika wastani wa ukubwa wa robo ekari, kwa matarajio ya kuvuna magunia kati ya tano na sita.

Mkulima huyo anasema, baada ya kuanza kutumia unga wa mahindi lishe, sasa hivi uzito wake binafsi na wa watoto wake zimeongezeka.

Mbali na hilo, anaeleza furaha yake kwamba hata ufanisi wa mwanafunzi darasani upo juu, tofauti na awali kabla ya kuanza kutumia mahindi hayo.

“Sasa hivi natumia mahindi lishe kwa uji na chakula na hivi sasa wananchi wamehamasika na wanakuja kwangu kutafuta mbegu na mwakani natarajia kulima ekari mbili za kilimo cha mahindi lishe,”anasema.

Ombi lake ni kwamba Sugeco inapaswa iendelee kuwasaidia wakulima, kwa sababu majibu yake yameonekana katika kilimo cha msimu uliopo na wakulima wengi wamevutiwa.