Maisha ya sinema zama hizo na kumbi zilizotamba mijini

27Nov 2021
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Maisha ya sinema zama hizo na kumbi zilizotamba mijini

MIONGO kadhaa nyuma, kulikuwa na kumbi za sinema kila kona jijini Dar es Salaam na miji mingineo zilizotamba, hadi mwishoni mwa miaka ya 1990, wakati huo starehe hiyo ilikuwa kwenye chati.

Ni kwa sababu hakukuwa na televisheni, video, CD wala flash, hivyo ili kuangalia sinema ilikuwa ni lazima mtu atoke nyumbani, yeye peke yake au na familia yake aende sehemu maalum ambayo ilikuwa ikitumika kuonyesha filamu mbalimbali za mastaa ambao walivuma kipindi hicho.

Ukiwa sebuleni kwako, unaangalia filamu na watoto wake sasa hivi, halafu ukirudisha nyuma kumbukumbu kuwa zile picha ambazo unaziangalia leo sebuleni miaka ya nyuma ulilazimika kupanda basi kuzifuata, tena wakati mwingine kulanguliwa tiketi, au kufanya 'booking' wiki moja au mbili kabla, unabaki kucheka kimoyomoyo peke yake.

Unaweza ukadhani umekaa nchi mbili tofauti.

Tukianza na vijana waliozaliwa au kuishi Dar es Salaam wakati huo watakumbuka jinsi kulivyokuwa na kumbi mbalimbali za sinema zilizotamba.

Watoto, vijana na hata watu wazima wa wakati huo, wakitaka burudani ya kuangalia filamu, wakati huo zikiitwa 'picha', ni lazima waende kwenye kumbi ambazo ni maalum kwa kuonyesha sinema mbalimbali za Kizungu, Kichina na Kihindi.

Kumbi zilizotamba jijini Dar es Salaam ni Cameo, Odeon, New Chox, Avalon, Emress, Empire, Star Light, bila kusahau Drive Inn Cinema.

Wenyewe watoto wa mjini waliuita 'Drai'. Huu ndiyo ukumbi maarufu zaidi wa sinema jijini Dar es Salaam kwa sababu haukuhitaji kuwa na kiingilio ili kwenda kutazama picha.

Ni uwezo wako wa kutembea tu kutoka unakoishi hadi hapo. Kwa vijana wa sasa, Drive Inn Cinema ni maeneo ya Msasani, ambapo kwa sasa kuna Ubalozi za Marekani.

'Drai' ilijengwa tofauti na kumbi zingine zote, nadhani nchini Tanzania  kama siyo Afrika.

Wakati kumbi zingine zilijengwa kama majumba mengine ya starehe ambayo ni lazima ukate tiketi na kuingia ndani, 'Drai' ilijengwa kama vile uwanja wa mpira, tena vile vya mikoani, au Uwanja wa Uhuru. Na hata ukubwa wake unafanana na viwanja hivyo.

Lakini kulikuwa na ukuta mkubwa pembeni juu, kama vile jukwaa hivi ambalo lilitumika kuonyeshea sinema hizo. Wakati huo hata ukiwa maeneo ya Kinondoni, au Makumbusho na Kijitonyama, ukuta ule au 'bodi' la sinema, lilikuwa kinaonekana vizuri tu.

Kulikuwa na watu wa aina mbili waliokuwa wakitazama sinema maeneo ya Drive Inn.

Ulijengwa maalum kwa watu kwenda na magari na familia zao, ambapo walikuwa wakiingia ndani ya uwanja huo kupitia magetini na humo ndani kulikuwa na maeneo maalum ya kukaa watu na familia zao, pamoja na sehemu za kupaki magari yao. Na ndiyo maana ukaitwa 'Drive Inn'.

Aina nyingine ni wenzangu na mimi. Hawa nadhani ndiyo walikuwa wengi zaidi kuliko waliokuwa wanaingia na kulipa kwa pesa.

Walikuwa wakikaa nje ya uwanja au ukumbi huo, lakini walikuwa na uwezo wa kuangalia sinema vizuri tu. Tatizo lilikuwa moja. Watu waliokuwa nje ambao wote hakuwa wanalipa, yaani bure kabisa, walikuwa hawasikii sauti. Sauti ziliishia ndani kwa wale walioingia na magari yao.

Iliaminika kuwa waliokuwa wakiingia ndani mle na magari yao ni watu wenye uwezo tu, mabalozi, wakurugenzi, mameneja, wafanyabiashara wakubwa na watu wengine tu wenye pesa zao.

Sasa wale watoto wa vijana wa uswahilini, Kinondoni, Mwananyamala, Magomeni, Msasani, Mburahati, Kigogo, na wakati mwingine watu wazima, walikuwa wakijazana nje na kuangalia picha na ilikuwa kuanzia saa 12, wakati mwingine hadi saa nne usiku au tano.

Tabu nyingine ilikuwa ni mbu, kwa sababu ilikuwa nje na pembeni kulikuwa na majani mengi, kulikuwa na mbu wengi kiasi cha watu kusema 'Drai tiketi ni mbu,' wakiwa na maana sehemu ile haikuwa na kiingilio, lakini lazima uvumilie mbu.

Kuna baadhi ya watu ambao walikuwa wakiangalia sinema hizo kibubu-bubu nje ya 'Drai', lakini wakirejea nyumbani wanakuwa wasimuliaji wazuri na watafsiri kwa wenzao. Cha ajabu ni kwamba licha tu ya kutojua lugha ya Kiingereza au Kihindi, lakini hata sauti walikuwa hawasikii, lakini kwa kusimulia picha ilivyokuwa utadhani wao ndiyo watunzi wa huyo sinema.

Halafu kwa asilimia kubwa, watoto na vijana wa wakati huo walipendelea sana picha za kibabe.

Ni sehemu ambayo ilivuta wafanyabiashara wengi wa vyakula vidogo vidogo, kama 'ice cream',  vinywaji na vitafunwa. Hata ule mtaa wa 'Maandazi Road' ulikuwa maarufu kwa sababu wengi walikwenda kununua maandazi maeneo hayo kwa ajili ya kutafuna wakati wanaangalia picha 'Drai'.

Mastaa waliokuwa wakitamba ni baba lao Bruce Lee, Angela Mao, Wang Yu, Sonny Chiba, Jim Kelly, Jackie Chan na wengine, huku kwa upande wa picha za kihindi kukiwa na Amitabh Bhachchan, Govinda, Mithun Chakraborty, Dharmendra, bila kumsahau Amrish Puri maarufu mama mzee Ashanti au Mugambo, kubwa la maadui.

Sinema zilizokuwa zikitamba wakati huo ni zile zote ambazo staa alikuwa Bruce Lee, War Bus, American Ninja, na nyingine nyingi, huku za kihindi ni 'Loha', 'Nasseb', 'Disco Dancer', 'Dance Dance', 'Andha Kanoon,'Hatya' na nyingine nyingi.

Kuna picha inaitwa Snake in the Monkey Shadow, iliyochezwa na Jackie Chan. Hii ilisababisha wengi kuiga staili yake ya kupigana mitaani ya kunyanyua mguu mmoja na mikono kuweka kama nyoka kobra anavyotaka kugonga mtu. Picha za Bruce Lee zilisababisha mtu akitaka kupigana avue shati.

Kumbi zingine ambazo zilikuwa zikionyesha picha hizo Sapna na Shaan zilizokuwa Morogoro, Metropole na Elite ambazo zilikuwa Arusha, huku Mwanza kulikuwa na kumbi kama Tovol Hall na Leberty Hall.

Mkoano Tanga, kumbi maarufu zilikuwa ni Majestic, Regal na Novelt, Geita wao walikuwa na ukumbi wa Mamlaka ya Pamba na Singida kulikuwa na Furaha Cinema. 

Kwa maoni tuma 0716 350534.

  

Habari Kubwa