Majeruhi wa Bodaboda

19Jul 2019
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Majeruhi wa Bodaboda
  • *Gharama za matibabu mzigo usiobebeka
  • *Hutibiwa kwa sera ya msamaha
  • *Bingwa asema hufikia hata milioni 3/=

USAFIRI wa pikipiki nchini licha ya kurahisisha safari na kutoa ajira kwa vijana umeendelea kuwa changamoto.

Hiki ni chanzo cha vifo na majeruhi na huchangia kuwapo umaskini na uharibifu wa mali kwenye jamii mbalimbali kwa kuwa zinahusika sana na ajali za barabarani.

Kwa mujibu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, kwa mwaka 2017 kulikuwa na ajali za pikipiki 1,459 ambazo zilisababisha vifo 728 na majeruhi 1,090.

 

Aidha, kwa mwaka 2018 ajali za pikipiki zilipungua ambapo zilikuwa ajali 876 na kusababisha vifo vya watu  366 na majeruhi 994.

MZIGO WA TIBA

Waziri ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, anasema mzigo mkubwa wa matibabu ya majeruhi wa ajali hizo umekuwa ni mzito kwa serikali kwa kuwa wanatibiwa kupitia Sera ya Afya ya mwaka 2007 ambayo inatoa msamaha kwa wagonjwa wasio na uwezo.

Majeruhi wa ajali hizo ambaye amelazwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Petro Sang’a, anasema matibabu ya mivunjiko wa mifupa inayotokana na ajali ni changamoto hasa kwa watu wenye vipato vya chini.

 

Anasema matibabu ya mguu wake hadi sasa yamegharimu zaidi ya Sh. milioni 1.2 ambazo amechangiwa na ndugu na jamaa zake.

 

“Kutokana na gharama za matibabu kuwa kubwa ndugu na jamaa wamekuwa wakinichangia, na pia nimelazimika kukata Bima ya Afya ya Jamii iliyoboreshwa (CHF) ya Sh. 30,000 ambayo inanisaidia kwa matibabu madogo madogo,”anasema dereva huyo wa boda boda.

Sang’a alipata ajali mwezi Aprili mwaka huu ambapo mguu wake ulivunjika mara mbili, jambo lililosababisha kushindwa kufanya shughuli zake licha ya familia kumtegemea.

Akizungumza na Nipashe, anabainisha kuwa kwa takriban miezi mitatu yupo kitandani bado akiuguza majeraha hali ambayo imemrudisha nyuma kimaendeleo.

“Gharama nilizotumia na kuchangiwa na ndugu ningeweza kufanya mradi mwingine mdogo ambao familia ingekuwa ikipata kipato kama ningekuwa na bima kubwa ya afya yenye uwezo wa kubeba matibabu yote, kuna umuhimu kama serikali ikitunzishia bima ya afya ya aina hii,”anasema

Majeruhi mwingine Adri Sahagagili, anasema amepata ajali ya pikipiki ambayo imesababisha mguu  kuvunjika mara tatu hadi sasa matibabu yamekula zaidi  ya Sh.milioni 2.1 kutibu mguu wake.

“Ajali yangu nilipata mwezi Aprili, mwaka huu. Mimi nilikuwa naendesha pikipiki lakini taa zilikuwa si nzima  sikuweza kuliona gari lililokuwa limeharibika katikati ya barabara hivyo nikaligonga na kunisababishia kuvujika mguu,”anasema.MAONI YA DAKTARI

 

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Upasuaji, Ajali na Mifupa, Dk. Ernest Ibenzi, akizungumzia gharama anasema.

 

“Matibabu kwa wanaovunjika miguu, mikono na majeraha vichwani ni kati ya Sh.500,000 hadi 3,000, 000 na hutegemea na kiwango cha mvunjiko.”

Anasema kwa wasio na uwezo wa kumudu gharama hizo hutibiwa kwa utaratibu wa msamaha ambapo serikali hurejesha gharama zao kwenye hospitali husika.

“Serikali hutoa msamaha wa muda lakini huku mgonjwa akiendelea kutibiwa, huu msamaha si bure serikali hurejesha fedha hizi kwa kuzirudisha kwenye hospitali, anasema gharama hizo ni pamoja na vyuma wanavyowekewa waliovunjika miguu ambapo kwa mfupa wa paja chuma chake kinagharimu Sh. milioni 1.5.”

Dk.Ibenzi anasema kwa wale wanaotakiwa kubadilishiwa nyonga gharama yake hufikia kiasi cha Sh. milioni 2,000,000 hadi 3,000,000.

“Hawa majeruhi ambao mivunjiko sio mikubwa wanakaa hospitali kwa siku saba, lakini wale ambao wamevunjika sana wanakaa hadi miezi sita hospitali, mwenye shida ya kichwa anatibiwa hadi apate fahamu, kwa hiyo unaona ajali hizi zinasababisha kushindwa kuendelea na shughuli zao za kiuchumi,”anasema.Vile vile, mtaalam huyo anasema bei halisi ya miguu bandia ni kati ya Sh.milioni 1.5 hadi 3,000,000.

MAJERUHI 50

 

Mtaalamu bingwa huyo anasema kwa siku hospitali hiyo inapokea majeruhi wa ajali ikiwemo za pikipiki 50 ambapo kati yao zaidi ya 30 hulazwa.Mganga huyo anasema kila siku wanafanya upasuaji kwa majeruhi 12 hadi 17 wa ajali za barabarani.

Dk.Ibenzi anasema ni vyema madereva kuchukua tahadhari na kufuata sheria ya usalama wa barabarani kwa kuwa madhara ya mwendokasi ni makubwa kwenye afya zao.

“Kama huo mpango ambao Wizara ya Afya inatarajia kuuleta wa bima kwa watu wote utakuwa suluhisho kwenye gharama za matibabu ya ajali na pia magonjwa yasiyo ya kuambukiza yana gharama kubwa pia, ni vyema mpango huu ukianza watu wakate bima za afya,”anasema.

BIMA YA AFYA

Waziri ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, anasema tangu usafiri wa bodaboda kuruhusiwa kubeba abiria mwaka 2010 serikali imekuwa ikiingia gharama kubwa kutibu wagonjwa wa ajali huku asilimia kubwa wakitibiwa kwa fedha za umma.

 "Nipo kwenye mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Ndani, tunataka kupeleka muswada bungeni ambao utalazimisha kila anayeendesha bodaboda moja ya masharti lazima uwe na bima ya afya hii itaweza kusaidia wengi kuepuka ulemavu unaoweza kuzuilika na kupunguza mzigo wa serikali," anasema.SHIRIKA LA AFYA

Kwa mujibu wa Ripoti ya Shirika la Afya Duniani(WHO), iliyotolewa mwaka 2018, inaonyesha  kila mwaka takriban watu milioni 1.35 hufariki dunia kwa sababu ya ajali ya barabarani.

 

Kati ya watu zaidi ya milioni 20 na 50 wanapata majeruhi yasiyo ya mauti, na wengi wanapata ulemavu kutokana na majeraha yao.

Ripoti inasema majeraha ya ajali za barabarani husababisha hasara kubwa za kiuchumi kwa watu binafsi, familia zao, na mataifa kwa ujumla.Hasara hizi zinatokana na gharama ya matibabu pamoja na upotevu wa mali kwa wale waliofariki au walemavu na majeruhi yao huku nchi nyingi zikigharamika kutokana na ajali hizo kwenye ukuaji wa pato la taifa(GDP) kwa asilimia tatu.