Majeruhi bodaboda waipa mtihani MOI

27Feb 2016
Moshi Lusonzo
Dar
Nipashe
Majeruhi bodaboda waipa mtihani MOI
  • *Idadi yao sasa ni 60% ya wagonjwa wote

IDADI ya majeruhi wanaofikishwa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) kutokana na ajali za pikipiki (maarufu bodaboda) imeendelea kuwa ya juu na kuipa changamoto kubwa taasisi hiyo, imefahamika.

Dereva bodaboda akiwa amepakia mshikaki (Picha kwa hisani ya Blogu ya Newztanzania).

Uchunguzi uliofanywa na Nipashe hivi karibuni na kuthibitishwa na Mkurugenzi wa MOI, Dk. Othman Kiloloma, umebaini kuwa asilimia 60 ya wagonjwa wote wanaofika kwenye taasisi hiyo kwa ajili ya kupata huduma huwa ni majeruhi wa ajali zinazohusisha bodaboda.

Majeruhi wa bodaboda wameongezeka MOI kwa asilimia tano kulinganisha na taarifa za awali zilizowahi kuchapishwa na gazeti hili Novemba 4, 2014, zikionyesha kuwa majeruhi wa bodaboda huwa ni asilimia 55 ya jumla ya wagonjwa wote wanaohudumiwa na taasisi hiyo.

Akizungumza na Nipashe, Dk Kiloloma alisema katika kipindi cha mwaka 2014 na 2015, asilimia 60 ya wagonjwa waliofikishwa kwenye taasisi yao walitokana na ajali za bodaboda.

Aliongeza kuwa idadi ya majeruhi kwa siku huwa kubwa zaidi katika baadhi ya siku za sikukuu ambapo kwa wastani hupokea wagonjwa 35 hadi 60 watokanao na ajali mbalimbali, nyingi kati ya hizo zikitokana na bodaboda.

Katika siku ambazo ajali za bodaboda hazijashamiri, idadi ya majeruhi wanaofikishwa MOI huwa ni kati ya watu watano hadi 35.

“Ajali za pikipiki zinachangia sana kuongezeka kwa idadi ya watu wanaojeruhiwa na hatimaye kuletwa hapa (MOI). Hata ukiingia katika wodi na kuzungumza na wagonjwa utapata ushahidi huo,” alisema Dk. Kiloloma.

Alisema licha ya ukweli huo, hakuna tofauti yoyote ya taratibu za kuhudumia wagonjwa kwani madaktari na wauguzi hutoa huduma bora kwa kiwango sawa kwa watu wote, bila kujali vyanzo vya matatizo yao.

Dk. Kiloloma aliongeza kuwa mara zote, madaktari na wauguzi huzingatia maadili ya kazi yao na kwamba hakuna ukweli wowote kuhusiana na madai kuwa majeruhi watokanao na ajali za bodaboda huishia kukatwa miguu.

“Sisi hatufanyi kazi juu ya sheria. Kazi yetu inategemea misingi na haki ya kila mtu. Kila aliyekatwa kiungo, ni lazima madaktari walijiridhisha kwamba hakuna njia nyingine ya kuokoa maisha ya mhusika,” alisema Dk. Kiloloma.

Alisema MOI hupokea idadi kubwa ya wagonjwa kutoka maeneo mbalimbali ya nchi na mara zote, madaktari na wauguzi hujitahidi kuwahudumia kwa kiwango sawa kwani taasisi yao (MOI) ni ya kitaifa.

Msemaji wa MOI, Almas Jumaa, alisema kila majeruhi huhudumiwa kwa kiwango sawa na hivyo, hakuna ukweli wowote pia kuhusiana na uvumi kwamba MOI ina wodi maalumu kwa ajili ya kuwalaza majeruhi wa ajali za bodaboda.

Alisema hata mtu akienda wodini, hawezi kujua ni mgonjwa yupi ametokana na ajali ya bodaboda, labda iwe hivyo baada ya kuwahoji mmoja hadi mwingine kwa sababu wagonjwa wote huwa pamoja bila kujali chanzo cha ajali iliyompata.

“Huwezi kujua kirahisi majeruhi gani ametokana na ajali kama pikipiki… wote wanalala wodi moja na kupata huduma sawa. Hii ni dhana potofu ambayo ni lazima ifutike katika vichwa vya watu,” alisema Jumaa.

MTIHANI MZITO
Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa ongezeko hilo la majeruhi watokanao na ajali za bodaboda ni miongoni mwa changamoto kubwa kwa madaktari, wauguzi na watumishi wengine wa MOI ambao hulazimika kufanya kazi ya ziada kuhakikisha kuwa wanatoa huduma bora.

“Usafiri wa bodaboda hauepukiki. Ni wa gharama nafuu na unarahisha usafiri katika barabara zetu ambazo nyingine huwa na foleni kubwa za magari… hata hivyo, umakini mkubwa unahitajika kwa sababu ajali za vyombo hivyo husababisha majeruhi wengi zaidi kwa hapa MOI,” mmoja wa wauguzi wa MOI aliiambia Nipashe na kuongeza:

“Ukienda wodini na kuzungumza na wagonjwa, utabaini kuwa wengi wao wamefikishwa hapa baada ya kupata ajali zinazohusiana na bodaboda. Kama siyo madereva wenyewe, basi utakuta ni abiria wao. Ni vizuri kukawa na jitihada zaidi za kupunguza ajali hizi.”

Muuguzi Kiongozi wa MOI, Uwezo Nkomola, aliiambia Nipashe wiki iliyopita kuwa kwa kawaida, kanuni ya kazi yao huwataka kila muuguzi ahudumie wagonjwa sita au saba kwa siku, lakini wao hutoa huduma kwa wagonjwa kati ya 15 hadi 25, hiyo ikiwa ni sawa na wastani wa kuwahudumia majeruhi wa bodaboda kati ya 9 hadi 15 (asilimia 60 ya makadirio ya wagonjwa wanaofika MOI).

Dk. Kiloloma, alisema mgonjwa mmoja wa ajali ya pikipikipi hupaswa huduma ya upasuaji kuanzia Sh. 500,000 kwa ajili ya gharama ya vyuma vya kuunganisha mifupa, lakini hutozwa Sh. 250,000 tu.

Alisema chuma kimoja huuzwa kati ya dola 200 (Sh. 450,000) kwa mogonjwa mmoja, ukiacha gharama za vifaa tiba vingine na dawa.

Hata hivyo, Dk. Kiloloma alisema nusu ya wagonjwa hao wanashindwa kulipa gharama hizo, badala yake hospitali hubeba mzigo huo kwa asilimia mia moja.

Mkurugenzi huyo alisema wagonjwa wengi wanaohusishwa na ajali za pikipiki huumia zaidi maeneo ya kichwani, kuvunjika mikono, paja, miguu na hivyo matibabu yao kuwa ya gharama kubwa.

Aidha, Nipashe iliripoti wiki iliyopita kuwa baadhi ya gharama za matibabu yanayohusisha upasuaji katika taasisi hiyo hubebwa na MOI kwa sababu vifaa na gharama halisi za huduma zao huwa ni za juu kulinganisha na fedha wanazowatoza wananchi.

Mkurugenzi wa MOI, Dk. Kiloloma, alitaja mfano wa gharama za upasuaji wa nyonga, akisema kuwa wao huwatoza wagonjwa Sh. milioni 10, lakini katika hospitali binafsi huwa ni takribani dola 15,000 (Sh. milioni 32).

Kadhalika, Dk. Kiloloma alisema kifaa kimoja cha kuunganisha paja hukinunua kwa dola za Marekani 500 (zaidi ya Sh.
milioni moja), lakini wao hutoa huduma hiyo kwa kuwatoza wagonjwa Sh. 350,000 tu na kati ya fedha hizo, Sh. 250,000 huwa ni kwa ajili ya upasuaji na Sh. 100,000 kwa ajili ya kifaa hicho walichokinunua kwa dola 500. Gharama hiyo ni ya chini ukilinganisha na gharama za huduma kama hiyo katika hospitali nyingine binafsi ambazo hutoza kuanzia Sh. milioni mbili.

“Kwa idadi hii ya majeruhi wa bodaboda, ni wazi kwamba sehemu kubwa ya rasilimali za MOI hutumika kuwashughulikia majeruhi wa ajali hizi (za bodaboda). Kungekuwa na namna nzuri zaidi ya kupunguza ajali hizi pengine gharama za sasa za uendeshaji zingepungua,” mmoja wa wauguzi wa MOI aliiambia Nipashe.

KAMANDA MPINGA
Mwaka 2013, aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Perreira Silima, aliliambia Bunge kuwa ajali za bodaboda zilisababisha vifo vya watu 5,100 kuanzia mwaka 2007 hadi 2014.

Mkuu wa kikosi cha Usalama wa Barabarani, Kamishna Mohamed Mpinga, alisema takwimu zilizowahi kutolewa hivi karibuni na Kamati ya Usalama Barabarani mkoa wa Dar es Salaam zilionyesha kuwa kuanzia mwaka 2011 hadi Juni 2015, ajali 10, 351 za pikipiki zilitokea kwenye jiji hilo na kusababisha vifo vya watu 514 huku majeruhi wakiwa 10,079.

Alisema mwaka 2015, katika jiji la Dar es Salaam, kuliripotiwa ajali 1,132, huku Wilaya ya Temeke ikiongoza kwa kuwa na matukio 564 na kusababisha vifo 33 na majeruhi 517. Wilaya ya Ilala inafuatia kwa kuwa na ajali 450 huku vifo vikiwa 33 na majeruhi 215, Kindondoni ikiwa na ajali 118, vifo vikiwa vya watu 26 na majeruhi 71.

Hata hivyo, Mpinga alisema inawezekana takwimu hiyo ikawa si sahihi kutokana na watu wengi kwenda moja kwa moja hospitali kupata matibabu bila kupitia katika vituo vya polisi.

“Kipindi cha nyuma ilikuwa rahisi kujua idadi za ajali za pikipiki kutokana na utaratibu wa kupata fomu ya PF 3, lakini sasa suala hilo halipo kwani watu wengi wanakwenda hospitali kupata matibabu bila kutoa ripoti,” alisema Kamanda Mpinga.

SABABU ZA AJALI
Kamanda Mpinga alisema madereva wengi wa pikipiki wanaendesha vyombo vyao bila kufuata sheria za barabarani na ulevi wa kupindukia.

Alisema moja ya sharti la kuendesha pikipiki katika njia kuu, lazima dereva kuwasha taa ili iwe rahisi kuonekana, lakini wengi hawafuati hilo na hivyo kugongwa na magari mara kwa mara.

“Sababu nyingine ni kwamba, pikipiki haikutengenezwa kwa kubeba abiria, lakini ikibidi kufanya hivyo, lazima mtu avae kofia. Lakini abiria wengi hawataki kuvaa kwa kuhofia magonjwa ya ngozi na inapotokea ajali, ni wao (abiria) wanaokuwa katika hatari ya kuumia,’ aliongeza.

Kuhusu madereva wa pikipiki, alisema Chuo cha Ufundi Stadi (Veta), huendesha programu ya mafunzo kwa madereva wa pikipiki, lakini kinachosikitisha ni kwamba wengi hawapendi kwenda kujifunza.

MTAALAMU WA USAFIRISHAJI
Mtaalamu wa masuala ya usafirishaji, Injinia Hans Mwaipopo, aliwahi kuiambia Nipashe kuwa vyanzo vya ajali ni vitatu ambavyo ni binadamu anayechangia kwa asilimia 76, chombo anachotumia asilimia 16 na mazingira asilimia nane.
Alisema binadamu anachangi kwa asilimia hiyo kutokana na ukosefu wa elimu ya usalama barabarani kwa vile wengi hawajui sheria zinazowaongoza wawapo barabarani.

Mwaipopo alisema pia tabia ya kupuuza sheria kwa wanaofahamu huchangia ongezeko la ajali; kuporomoka kwa maadili kwani sasa ni rahisi mtu kupata cheti kwamba amesomea na kukionyesha hata kama hajawahi kusomea udereva.

Aidha, Mwaipopo aliongeza kuwa lipo pia tatizo la watu kupewa vyombo vya moto bila kujihakikishia kuwa ni wazima kiakili kwani upo uwezekano kwa watu wenye matatizo ya akili kuendesha vyombo vya moto kama pikipiki na hivyo kuhatarisha maisha ya watu wasio na hatia.

Mtaalamu huyo alisema katika nchi nyingi zilizoendelea, kabla ya mtu kukabidhiwa leseni anapimwa akili na hilo pia linapaswa kuzingatiwa ili kupunguza ajali.

Mwaipopo alisema sheria namba 30 ya 1973 na marekebisho yake inasema dereva mwenye leseni halali anatakiwa kuwa na sifa kuu tatu, ambazo ni pamoja na kusomea udereva katika chuo kilichosajiliwa na chenye walimu na macho yake yawe yanaona vizuri. Sifa nyingine ni kutokuwa na ulemavu unaoweza kuathiri chombo cha moto anachoendesha, kuwa na akili timamu, awe na afya njema na asiwe na maradhi yenye kuathiri chombo anachoendesha kama ugonjwa wa moyo, sukari na kifafa.

"Leo hii wapo madereva wana matatizo ya kifafa. Tukifanya ukaguzi, tutabaini kwamba wapo wengi wana matatizo ya macho, kifafa, moyo na sukari lakini wanaendesha vyombo vya moto. Hii ni hatari," alisema.

Alisema chombo kinachangia kwa asilimia 16 kwa maana ya matumizi mabaya, ikiwa ni pamoja na chombo kwisha muda wake wa matumizi, lakini bado kinaendelea kubaki barabarani huku mazingira yakichangia kwa asilimia nane, hiyo ikitokana na miundombinu mibovu na kukosekana kwa alama muhimu katika barabara na pia barabara kulazimishwa kona pasipostahili na nyingi kujengwa chini ya kiwango.

Alisema changamoto iliyop kwa watu wa bodaboda, ni tabia ya wengi wao kufundishana wao kwa wao. Hawajifunzi sheria za usalama barabarani na hivyo hujiona wenye haki kuliko watumiaji wengine.

Habari Kubwa