Majibu yanayowahamisha wafugaji kutoka ‘kusaka nyoka’ hadi sayansi

20Nov 2020
Na Mwandishi Wetu
Morogoro
Nipashe
Majibu yanayowahamisha wafugaji kutoka ‘kusaka nyoka’ hadi sayansi
  • Wafugaji wapishana na umaskini mlangoni

LEO hii wakiulizwa wafugaji wanaoishi katika maeneo yanayozungukwa na Shamba la Mifugo la Serikali la Ngerengere mkoani Morogoro, jibu lao linaangukia katika ‘kukombolewa kiuchumi’ kutokana na kuchangia maendeleo yao katika ufugaji.

Wana kauli ya pamoja kwamba, kuwapo shamba hilo, kumewaondolea vikwazo mbalimbali, ikiwamo walivyokuwa wakihama maeneo yao.

Sasa wanabaki katika eneo lilelile, wakiwa wanawezesha kuendelea na ufugaji wakitumia mbinu za kisasa.

SAUTI YAO

Kifuto Kimanga, mkazi na mfugaji wa Kiwege, anaeleza kwa muda mrefu alikuwa akifanya ufugaji wa kuhama na ulimsababisha yeye na familia yake kutokuwa na makazi maalum.

Kimanga anasema, kila siku walihangaika na kutumia muda mrefu poroni wakihangaikia kusaka na kupiga kambi katika maeneo ya kulishia mifugo na kuna wakati, waliingia kwenye migogoro na watumiaji wengine ardhi, baada ya mifugo yao kufanya uharibifu na hasa mashambani.

Anaeleza kutokana na uwapo wa shamba hilo lililoko chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, anasema sasa ameamua kuacha adha ya kuhama na kuamua kutafuta eneo la kudumu kwa ajili ya makazi na ufugaji wa kisasa, huku akiweka wazi mkombozi wake kifikra ni shamba la Ngerengere, lililompatia mbegu bora za mifugo wa kisasa.

“Uwapo wa shamba la LMU Ngerengere umewasaidia wafugaji kupata mbegu bora za mifugo kama ng’ombe, mbuzi na nguruwe kwa bei nzuri na mifugo hiyo inakuwa haraka, nyama nyingi na maziwa mengi,” anasisitiza Kifuto.

Pia, anabainisha kwamba kuwapo shamba hilo, kunawaunganisha na msaada wa kitabibu kwa mifugo yao, kutoka kwa wataalamu wa mifugo waliopo katika shamba hilo, inayoambatana na utunzaji bora wa mifugo iliyopo.

Aidha, anadokeza mafanikio aliyopata kutokana na ufugaji bora na wa kisasa, kwani mwaka 2013 alijenga nyumba kubwa ya kisasa yenye uwezo wa kuhifadhi wakazi 24, inayokidhi haja zao na kupeleka watoto shule nzuri na za kisasa.

Kadhalika, anasema ameendelea kufaidika na mifugo hiyo kwa kuzalisha mbuzi kwa wingi na wanawauza kwa bei inayompa faida, tofauti na waliwanunua mbuzi kwenye shamba la LMU Ngerengere, huku akiorodhesha bei nafuu ya ununzi na mauzo ya mifugo kama mbuzi Kifuto anajivunia kuwa na mbuzi wakubwa, wanaokua kwa haraka, wana nyama nyingi, makuzi yao yakipitia kauni muhimu za matunzo, ikiwamo chanjo, dawa za minyoo na lishe.

Esther Kilinga, mfugaji wa Kiwege, anaeleza kwamba amejipatia madume kutoka shambani hapo na kwa sasa ana ng’ombe 200, mradi uliofanikisha kujenga nyumba ya kisasa ya makazi na za wageni zinazowaingizia kipato na kuendesha maisha ya kila siku.

Kwa mujibu wa Kilinga, ni kiwango cha kipato kinchowawezesha hata kuchangia ujenzi wa nyumba ya ibada na kuwasomesha watoto kwa namna bora, katika shule anayoiita ‘ya kisasa.’

Pia, mradi huo wa kuuza maziwa, unaendana na samli iliyo hai kwa wanakijiji Ngerengere na maeneo jirani, hatua inayowanufaisha na kuchangia pato la taifa. Mfugaji mdogo na mkazi wa Ngerengere, Athumani Ramadhani, anajitambulisha alianza ufugaji mwaka 2018 akiwa na ng’ombe watatu, lakini sasa amefikisha 10.

Katika manufaa, hayuko mbali na wenzake na kuainisha faida alizozipata kujenga nyumba ya kisasa, kukidhi mahitaji ya familia yake ambayo hapo awali hali ya maisha ilikuwa mbaya.

Athumani anashukuru kuwapo shamba la LMU Ngerengere limewasaidia wafugaji kupata mbegu bora za mifugo inayowasaidia kuzalisha kwa wingi na kufundishwa kanuni za ufugaji bora na tiba kwa mifugo yao na kupata lita nane za maziwa kwa ng’ombe mmoja kwa siku. 

Ana ombi kwaa serikali isaidie kuwajengea josho wafugaji majumbani, kwani namna ya kuhudumia mifugo huko sasa ni ngumu, kwa kuwa dawa haziwafikii vizuri na kuna wakati mifugo inakwepa dawa, hata juhudi za kufanikisha uogeshaji zinaangamia.

Kwa kutambua mchango wa Sekta ya Mifugo serikalini, iliamua kuwekeza katika mashamba ili kuyapa uwezo wa kuzalisha mifugo bora itakayosaidia kukuza kipato cha taifa na wananchi kwa ujumla.

Ngerengere, ni miongoni mwa mashamba matano ya serikali yaliyo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.

MENEJA SHAMBA

Meneja wa Shamba la Ngerengere, Saita Ole Kimosa, anasema lilianzishwa mwaka 1975 kama shamba la ng'ombe wa maziwa ambalo kabla lilifahamika kama ‘Dairy Farm Company’ lililokuwa chini ya watu binafsi na baadaye kufilisika, ndipo likabadilishwa jina na kuitwa LMU mwaka 2004 chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Anaeleza, lengo la kuanzishwa shamba hilo ni kuzalisha mifugo bora yenye tija na kuuziwa wananchi kwa bei ambayo ni rafiki na kujiingizia kipato na kusaidia wananchi kupata mbegu bora za mifugo.

Ole Kimosa anasema, hadi kufika Mei ya mwaka huu, 2020 lilikuwa maganyiko wa mifugo: ng’ombe 771, mbuzi 234 na nguruwe 201, uzalishaji ukiwa na tija. Anataja aina ya mifugo iliyopo ni ng'ombe jamii za kisasa: Borani, Friesian na Chotara na kwa mbuzi, alitaja aina ya kutoa Afrika ya Kusini. Pia, nguruwe na mifugo mingine ya kisasa ipo.

Ole Kimosa, anataja mafanikio ya shamba, kwamba lina jumla ya mifugo takribani 1,206 na kuna mifugo mingi iliyozalishwa na kusambazwa, kwa kuwauzia wafugaji wadogo kwa bei ambayo ni rafiki katika Mkoa wa Morogoro na jirani Dar es Salaam.

Anafafanua kuwapo mifugo ya aina tatu, ambayo ni ng’ombe, mbuzi na nguruwe inayouzwa kwa wanachi kwa bei rafiki, ili kuwasaidia wananchi kupata mbegu bora za mifugo.

WAFUGAJI KUNUFAIKA

Ole Kimosa anasema, hadi sasa wamewapatia wafugaji mitamba bora kwa bei nafuu, baadhi ya wameathiriwa ndani ya shamba la hilo la serikali, wanawauzia maziwa wananchi wanaozunguka shamba hilo na kuwapa maksai kwa ajili ya kulima.

Pia, anaeleza wafugaji wananufaika kwa mifugo yao kutibiwa na wanapata ushauri kutoka kwa wataalamu shambani, wakihamasishwa kutenga mifugo yao na kuibebesha mimba pamoja na kuuziwa madume bora, ili kuboresha ngombe wa asili na kuwauzia chotara.

Meneja huyo anafafanua kuwa, katika kipindi cha kiangazi, kuna lambo linalofahamika kama Mkobora ambalo limetengwa kwa ajili ya wananchi kunywesha mifugo yao, ili kusaidia ng’ombe na mifugo mingine isife kwa kukosa maji.

Anataja ugumu anaopata ni kuwapo miundombinu mibovu na iliyochakaapamoja uchakavu wa vitendea kazi, vyote vinafanya washindwe kutimiza baadhi ya majukumu yao ya kila siku na kutoka eneo moja kwenda lingine, kutokana na ubovu au kutokuwapo kabisa usafiri.

Meneja anaongeza, katika kipindi cha doria wananchi hukasirishwa na kuna wakati wanaamua kuchoma moto baadhi ya maeneo ya shamba.

Vivyo hivyo, inaendana na uvamizi mdogo wa wafugaji kuingiza mifugo na kulisha ndani ya mashamba ya watu na kisha wanatoka.

Kilichopo, anadokeza wanatarajia kila mwaka kufanya uzalishaji mkubwa wa mifugo, wauze na kupata fedha kwa ajili ya kurekebisha miundombinu ya shamba na kutatua changamoto zilizo ndani ya uwezo wao.

 

Habari Kubwa