Makatazo na athari zake katika fikra,mawasiliano na mafarakano kijamii

11Jun 2019
Michael Eneza
Nipashe
Makatazo na athari zake katika fikra,mawasiliano na mafarakano kijamii

MOJA ya maeneo magumu katika historia ya fikra na hata maisha ya jamii kwa kawaida ni kuoanisha kile mtu anachojua na kile anachosema, au anachoweza kusema, hali ambayo mara nyingi inafanya iwe vigumu kutofautisha ukweli na uongo.

Jamii iliyostaarabika katika mawasiliano. PICHA: MTANDAO.

Kwa vile utamaduni na ustaarabu kimsingi umejengwa katika msingi wa kutofautisha maeneo hayo mawili katika hisia, mazungumzo au dhamira, kuwapo kwa mazingira mapana ambako siyo rahisi kusema kile ambacho mtu anafikiria ni tatizo, kwani inafanya mawasiliano au ubadilishanaji hisia kuwa mgumu, kuanzia mwanzo hadi mwisho.

Majadiliano kwa mfano katika redio za FM ni kielelezo cha mustakabali kama huo.

Mtaalamu mmoja wa Kiswahili anaulizwa katika majadiliano ya redio ya kujiliwaza na kutafakari vipindi vya asubuhi kuhusu neno ‘uhuni,’ na anakomalia kutoa maelezo kuwa mhuni ni mtu mwenye umri wa kuoa lakini hajaoa.

Kwa msikilizaji wa kawaida, au tuseme msikilizaji aliyeenda shule, hayo ni maelezo ya mzee wa kijijini labda wa umri wa miaka 65 kama siyo zaidi, ambaye anaona ni kioja mtu mwenye umri hata ingekuwa wa miaka 30 kuwa bado hajaoa, na mbaya zaidi, hana mipango ya kuoa.

Inaelekea maelezo hayo ya kuchukua neno ‘uhuni’ kuwa ni kutokuoa yalilenga wanaume, na kwa jumla neno hilo linatumika zaidi kwa wanaume, ambayo ni sahihi kiasi tu.

Yako maeneo mengi tu ambako hata mwanamke anaweza kuwa mhuni, kwa maana ya mtu asiyeaminika, asiyekuwa na ahadi au kuweza kutumainiwa kutenda kwa mujibu wa kile alichosema, na siyo udanganyifu hata kwa jambo ambalo anayemsikiliza anajua fika liko hivi au vile.

Kimsingi ni tabia hiyo ya kutokuwajibika katika masuala ambayo yanagusa watu wengine ambako dhana ya ‘uhuni’ imejichimbia, na siyo kuwa na maisha ya ndoa au hapana, au kuwa na maisha thabiti ya ndoa.

Hisia ya kuelekeza neno hilo katika uwepo wa ndoa ni uhafidhina, ambako kuingia katika maisha ya ndoa kwa wakazi wa maeneo ya pwani kijadi ni kama jando kwa makabila mengine hasa ya wafugaji, ambako jando ndiyo inatoa heshima kwa kijana awe na sifa ya kuoa. Pwani anaoa tu.

Yako maeneo mengine ambako uhafidhina unaoendana na makatazo ya kitamaduni kwa jamii za pwani yanafikia mahali yanatawala lugha, iwe ni kwa kuunda neno moja kutumika kwa hisia au dhana fulani kwa lengo la ‘kupaka rangi’ ili ipendeze au isipendeze, au kufanya uhusiano wa dhana hiyo na neno husika kuwa wa msingi sana.

Moja kati ya maneno kama hayo ni matumizi ya dhana ya ‘tendo la ndoa’ ambayo ni vigumu kusema ilianza wapi, kwani kwa waliokuwapo zamani hapakuwa na mfumo huo wa maneno ila kugusia kwa mfano ‘unyumba,’ lugha ya adabu ya kuzungumzia mahusiano ya watu wanaokaa pamoja.

Na kwa jumla inatazamiwa kuwa wanakuwa katika ndoa.

Sasa kuinua matazamio hayo iwe ni mfumo halisi wa fikra inakuwa kidogo inaleta matatizo kwani inafikia mahali ambapo mtaalamu wa Kiswahili aliyeingiza neno ‘tendo la ndoa’ hakuwa anazingatia kuwa anazungumza lugha na siyo anatoa mawaidha katika nyumba ya ibada, ambapo kusingekuwa na ukinzani kuhusu usahihi wa msamiati kama huo.

Ila kuna upande mwingine wa kushangaza, kuwa hao hao (inaweza kutazamiwa) waliotunga msamiati wa kuzuia uwezekano wa unyumba au uhusiano wa kimapenzi nje ya ndoa, kwa kuchukulia kuwa ile dhana tu ya kushirikiana kimapenzi inajumuishwa na ndoa, walitunga maneno mengine kukinaisha mazungumzo ya ushirika kama huo nje ye ndoa. Inaelekea ‘walitohoa’ (kukopa, kutwaa maneno) kutoka lugha nyingine za pwani, kwa mfano neno ‘ngono’ ambalo si rahisi kujua limetoka wapi, na ni moja ya misamiati ya takriban miaka 20 au zaidi.

Pamoja na matatizo hayo ya kupiga pasi fikra na misamiati ili iendane na kinachotazamiwa na wazee katika jamii fulani, bado ni wazi kuwa ipo juhudi ya kuondoa kabisa matumizi ya maneno yasiyo na staha yasisikike hadharani, na kukiuka kanuni hiyo ni moja ya sababu za ugomvi wa kila siku kati ya chombo cha kudhibiti sanaa, mawasiliano na vijana wanaolenga mashabiki, kugusa hisia zao.

Wanajitahidi kuvuka mipaka wakitazamia kuwa wataeleweka vyema kwa njia moja au nyingine, mara nyingine waponee chupuchupu na mara nyingine inabidi wakumbushwe kuwa kuna mipaka inabidi iangaliwe, ili fedheha isitawale anga ya mawasiliano na kusababisha taharuki.

Tatizo la mawasiliano na makatazo ni kubwa kwa sababu utamaduni kote duniani umejengwa katika misingi miwili ya Torati au Jadi kila mahali, kwani torati ilitolewa kwa watu maalum na wengine walipewa mafunuo au amri zinazoendana na torati hiyo maalum, na mara nyingine hata majina ya watoa amri yanafanana.

Kwa mfano mmoja wa watoa amri muhimu wa Israeli ya kale ni Mfalme Sulemani ambaye aliandika vitabu viwili/vitatu vya busara, hasa Mithali na Mhubiri, na jina lake likiandikwa kwa Kiingereza, Solomon, linashabihiana na mtungaji sheria muhimu wa Uyunani, Solon.

Alipata sifa kiasi ambacho dhana nzima ya kunukuu ilijengeka katika utamaduni wa Kilatini (eneo la pwani ya Kaskazini ya bahari ya Mediterranean) kuwa ni kukumbusha alichokisema Solon katika suala fulani, kwani Kifaransa, ‘selon…’ ni ‘kwa mujibu wa.’

Katika Kiarabu mtoa sheria muhimu, Muhammad bin Abdullah SAW anatambuliwa katika mtiririko kama huo, kuwa pale alipotoa maelekezo kama yeye, na siyo ufunuo (unaotoka kwa malaika) inaitwa ‘sunna,’ ambayo ni njia nyingine ya kutamka neno ‘selon,’ au inatoka kwa Solon.

Jitihada ya kuficha kile kinachozungumziwa ni sehemu ya utamaduni wa kumlinda anayesikiliza, ambao upande wake wa pili ni kutamka maneno yenye dhamira ya kumuumiza mhusika.

Hapa pia kuna mwingiliano wa kushangaza kidogo wa lugha, katika neno ‘kutukana’ ambalo ukiangalia kwa haraka unadhania kuwa kinachotajwa hapo ni kutumia lugha chafu dhidi ya mtu au watu kadhaa, kumbe kuna maana nyingine imejificha, kuwa aliyetamka maneno hayo amekana undugu na wale aliowalenga.

Ni kuwakana kuwa ni ndugu zake, na kwa maana hiyo hawaoni kama wenye heshima au wanaostahili heshima mbele yake, hivyo ‘ametukana’ haina maana tu kuwa ametoa matusi ila ‘hana undugu na sisi’ yaani amewakana kama ndugu, ambalo ni jambo la hatari, linaloshangaza.

Ina maana kuwa kuanzia dakika hiyo alipokana undugu wake na wahusika, mtu akiinua upanga akiwa mlengwa wa maneno yale walio karibu wasingefanya lolote.

Makatazo kimsingi yalilenga mahusiano au tabia katika mazingira ambako jamii ndiyo inasimamia sheria, kwa mfano kupiga mawe mwizi, mgoni n.k. utamaduni ambao sasa haukubaliki, kuwa kuchukua hatua ya kutoa hukumu na kuitekeleza ni kujichukulia sheria mkononi, kwani ni Mahakama, si jamii, iliyo na uwezo wa kuamua kama kuna kosa limetendeka.

Hata katika mazingira hayo, makatazo ya kihisia na lugha yaliyojengwa katika jamii za zamani zinazokataza mahusiano ya aina fulani (uhuru wa unyunba, maadili) bado yapo na yanasisitizwa na wataalamu, wakati ambapo jamii imebadilika.

Wanawake wanapokuwa sasa wanajilisha wenyewe, makatazo hayo hayafai kitu kwani msingi wake ni kuilinda ‘mali’ ya mtu fulani ‘isiibwe…’

Habari Kubwa