Makipa mashujaa wa penalti Ligi Kuu 2020/22

25Oct 2021
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Makipa mashujaa wa penalti Ligi Kuu 2020/22

KABLA ya mechi za Jumapili za Ligi Kuu, jumla ya penalti tano zilikuwa zimepatikana, huku moja tu ikiwekwa wavuni.
Shiza Kichuya wa Namungo FC, ndiye mchezaji pekee aliyefunga penalti mpaka sasa kwenye Ligi Kuu hadi kufikia Jumamosi.

Kipa Aboutwalib Mshelly wa Mtibwa Sugar, mmoja kati ya makipa wanne waliookoa penalti kwenye mechi za Ligi Kuu hadi kufikia juzi.

Alifanya hivyo kwenye Uwanja wa Ilulu, alipoweka wavuni mkwaju wa penalti, akiisawazishia Namungo FC, iliyokuwa inaongozwa kwa bao moja dhidi ya KMC.

Bao hilo liifanya timu hizo kufungana 1-1, hivyo penalti nne zilizobaki zilikoswa na wachezaji John Bocco wa Simba, Eliud Ambukile wa Mbeya City, Boban Zirintusa wa Mtibwa Sugar na Raymond Masota wa Geita Gold.

Penalti zote hizi ziliokolewa kwa ustadi na makipa, hapa tunakuletea magolikipa waliookoa penalti hizo, jinsi walivyookoa na mechi walizocheza, haya sasa...

#1. James Ssetuba - Biashara United

Kipa huyo raia wa Uganda, aligeuka shujaa alipookoa penalti ya nahodha wa Simba, John Bocco kwa kuruka upande wa kulia na kuupangua. Ilikuwa ni dakika ya tatu ya nyongeza kwenye moja ya mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu kati ya Biashara United na Simba, ukichezwa Uwanja wa Karume, Musoma mkoani Mara.

Baada ya Pape Sakho kuangushwa ndani ya eneo la hatari, ilionekana kama Simba ingeweza kupata bao kwenye mechi hiyo iliyochezwa Septemba 28, mwaka huu, lakini kipa huyo alifuta matumaini hayo, timu hizo zikatoka sare ya bila kufungana.

#2. Hamad Juma - Mbeya Kwanza

Kipa wa Mbeya Kwanza, Hamad Juma alicheza penalti ya Ambukile dakika ya tatu ya mchezo wa Ligi Kuu, timu hiyo ikicheza dhidi ya ndugu zao Mbeya City, Oktoba 3, mwaka huu kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya. Ni mechi ambayo iliisha kwa sare ya mabao 2-2. Kama Mbeya City ingefunga mkwaju huo ingeweza kuibuka na ushindi.

Kipa huyo aliruka upande wa kulia alikopiga mpigaji na kupangua mchomo huo, akiwaweka salama Mbeya Kwanza, pia kuwabakisha mchezoni.

#3. Khomein Aboubakar - Geita Gold

Kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari Nyankumbu, Geita, kipa Khomein Aboubakar wa Geita Gold aliokoa penalti iliyopigwa na Boban Ziruntusa wa Mtibwa Sugar, Oktoba 16 kwenye mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ilikuwa ni dakika ya 28, Mtibwa Sugar ilipopata penalti, lakini mpigaji ambaye alipiga upande wa kushoto, alishuhudia kipa huyo naye akiruka huko huko na kuupangua. Ni mechi ambayo iliisha kwa sare ya bao 1-1.

#4. Aboutwalib Mshelly - Mtibwa Sugar

Ni mechi ile ile ya Geita Gold dhidi ya Mtibwa Sugar. Ni mechi ambayo imeingia kwenye rekodi ya kupatikana kwa penalti mbili kwenye mchezo mmoja msimu huu, kila timu ikipata penalti moja. Lakini zote zilishindwa kuzitumia.

Ilikuwa ni dakika moja kabla ya mechi kumalizika, wenyeji Geita Gold walipopata mkwaju wa penalti. Wakati huo mechi ilikuwa sare ya bao 1-1. Kazi ilikuwa ni kuukwamisha wavuni, ili iondoke na ushindi wa bao 1-0.

Shughuli hiyo aliachiwa Raymond Masota. Mshelly alimuotea mpigaji na kuruka upande wa kulia, akiucheza kwa ustadi wa hali ya juu, akiwanyima wenyeji bao dakika za mwisho, akiwafanya mashabiki wa Geita Gold waliojazana kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari ya Nyamkumbu, wakiwamo wanafunzi wa shule hiyo waliokuwa wamevalia sare, kuondoka vichwa chini.

Habari Kubwa