Makocha 5 waliokalia kuti kavu msimu huu

18Jan 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Makocha 5 waliokalia kuti kavu msimu huu

MAKOCHA kadhaa wanaweza kupoteza kazi zao kwa kipindi ambacho hakitabiriki kwenye mchezo wa mpira wa miguu.
Mara zote timu inapofanya vibaya kuliko matarajio ya wengi, makocha ndio wanabeba mzio wa lawama.

Huku kukiwa kumebakiwa na nusu ya pili ya msimu huu wa ligi za soka Ulaya, makocha kadhaa kwenye klabu kubwa, wanaonekana ni kama wamekalia kuti kavu, kwani wanaweza kupoteza ajira yao wakati wowote.

Makala haya inawaangalia makocha watano ambao wanaweza kupoteza kazi zao kabla ya mwishoni mwa msimu huu...

#5. Ronald Koeman (Barcelona)

Ronald Koeman aliteuliwa kuwa kocha wa Barcelona kipindi cha majira ya joto mwaka 2020, huku klabu ikiwa na matarajio makubwa kutoka kwake.

Koeman amekumbana na mambo mengi pale Barcelona ndani ya uwanja na nje ya uwanjani. Hata hivyo, bado wapo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa LaLiga, wakipitwa pointi nne na vinara Atletico Madrid, wakiwa wamecheza mechi tatu zaidi ya kikosi hicho cha kocha Diego Simeone.

Hata kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, Barcelona wapo kwenye droo ngumu hatua ya 16, wakikabiliana na Paris Saint-Germain kama ilivyokuwa msimu wa 2016-17.

Zaidi ni kwamba, kwa sasa Barcelona wapo kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu wa rais. Na mmoja wa wagombe amebainisha wazi kabisa kwamba kipaumbele chake cha kwanza akishinda ni kufumua benchi la ufundi, kitu ambacho kinaonekana wazi kwamba, ajira ya Koeman ipo shakani.

#4. Antonio Conte (Inter Milan)

Antonio Conte ni kocha ambaye yupo kwenye presha kubwa baada ya kushindwa tena kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Inter Milan.

Katika kundi ambalo pia ilikuwapo Real Madrid, Shakhtar Donetsk na Borussia Moenchengladbach, Inter Milan ilimaliza nafasi ya nne. Hiyo maana yake ni kwamba, Nerazzurri hao hawatacheza Ulaya msimu huu.

Inter Milan kwa sasa wapo nafasi ya pili kwenye msimamo wa Serie A, pointi tatu nyuma ya vinara AC Milan ambao ni wapinzani wao wa jiji moja.

Conte alikwaruzana na maofisa wa Inter kabla ya kuanza kwa msimu huu na ilionekana wazi kwamba angetupiwa virago. Hata hivyo, msimu huu kama atashindwa kubeba taji la Serie A kuna uwezekano mkubwa wa kupoteza kazi yake.

#3. Andrea Pirlo (Juventus)

Wakati Andrea Pirlo alipoteuliwa kuwa kocha wa Juventus, mjadala mkubwa uliibuka. Bianconeri walimfukuza Maurizio Sarri licha ya kushinda taji la Scudetto.

Tofauti na matarajio yao baada ya kumfukuza Sarri, Juventus haijawa kwenye kiwango bora. Ingawa Juventus ina michezo miwili mkononi, wamepitwa pointi 10 na vinara wa Serie A, AC Milan.

Hata kama Juventus wakishindwa kutwaa taji la Serie A msimu huu, kama Pirlo atawaongoza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, anaweza kubaki klabuni hapo. Tofauti na hapo nafasi yake bado ipo shakani.

#2. Frank Lampard (Chelsea)

Frank Lampard tayari yupo kwenye presha kubwa pale Chelsea. Blues hao wapo nafasi ya saba kwenye Ligi Kuu, wakiwa na pointi 29 kutokana na mechi 18.

Lampard amekuwa na asilimia mbaya zaidi ya kushinda kuliko kocha yeyote aliyepita pale Chelsea tangu zama za Roman Abramovich. Hivyo, licha ya kuwa gwiji wa klabu hiyo, uvumilivu unaweza kuwashinda wamiliki wake.

Msimu uliopita Chelsea ilitumia pauni milioni 250 kwa ajili ya kutengeneza kikosi kipya, lakini hadi sasa matokeo dimbani si ya kuridhisha.

Kiungo huyo wa zamani wa Chelsea bado hajaweza kukitengeneza vizuri kikosi hicho licha ya usajili wa Timo Werner na Kai Havertz.

#1. Pep Guardiola (Manchester City)

Pep Guardiola hajasaini mkataba mpya wa kuendelea kukaa pale Manchester City.

Hata hivyo, raia huyo wa Hispania nafasi yake inaweza kuwa shakani mwishoni mwa msimu huu. Msimu uliopita, City ilimaliza kwa kupitwa pointi 18 na Liverpool kwenye Ligi Kuu. Pia walipoteza kwa Lyon katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Msimu huu, pia wapo kwenye mbio za ubingwa. Lakini kiwango cha timu si cha kuridhisha sana.

Hajawahi kuiongoza City zaidi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, bado hajawahi kushinda taji la Ligi ya Mabingwa katika kikosi alichokinoa kikiwa bila Lionel Messi.

Kama Manchester City watamaliza msimu huu bila taji lolote, ni wazi kwamba nafasi ya Pep Guardiola kuendelea na kazi yake ya ukocha pale kwenye dimba la Etihad itakuwa ngumu.

Habari Kubwa