Makocha 9 wanaoweza kumrithi Setién Barca

06Jul 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Makocha 9 wanaoweza kumrithi Setién Barca

HUKU msimu ukielekea ukingoni, muda huu sio mzuri kwa Kocha wa Barcelona, Quique Setién.

Barcelona imeanguka tangu kurudi tena kwa La Liga, imeiruhusu Real Madrid kuwa juu kwenye mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Hispania. Soka lao halivutii na wachezaji wanaonekana kutokuwa kwenye viwango vyao na inaonekana mambo ni mabaya na Setien anaweza kufukuzwa mara tu baada ya msimu huu kufika mwisho.

Hapa tunawaangalia makocha 9 ambao wanapewa nafasi ya kuchukua mikoba yake.

1. MAURICIO POCHETTINO

Mauricio Pochettino pengine ndio mtu ambaye anaweza kuwa kwenye nafasi kubwa zaidi ya kupewa mikoba hiyo, kwani hana kibarua chochote kwa sasa.

Anaweza kuwa mtu mzuri zaidi kwa nafasi hiyo, ingawa alishawahi kusema kwamba anaweza asiende pale Camp Nou kwa sababu alishawanoa wapinzani wao wakubwa wa Barcelona pale Katalunya, Espanyol.

2. EUSEBIO SACRISTAN

Eusebio Sacristán alishinda mataji manne ya LaLiga kama mchezaji akiwa na Barcelona kabla ya kutumia miaka minne kufundisha kikosi B kati ya mwaka 2011 na 2015.

Pia alikuwa sehemu ya benchi la ufundi chini ya Frank Rijkaard pale Camp Nou. Kama Barça wanamtaka mtu anayeielewa vizuri klabu hiyo, Eusebio ndio mtu anayefaa kwa kazi hiyo.

Hata hivyo, tatizo la Eusebio hajawahi kuwa na mafanikio nje ya Barcelona. Alifanya kazi pale Real Sociedad na kwa sasa hana kazi tangu kipindi cha majira ya joto kilichopita, wakati timu yake ya Girona iliposhuka daraja.

Hajawa na rekodi ya kuvutia nje ya Barcelona, hivyo kazi hii inaweza kuwa kubwa zaidi kwake.

3. XAVI HERNANDEZ

Xavi anataka kurudi Barcelona? Ndio.

Wao Barcelona wanamtaka arudi? Ndio, walijaribu kumtaka kabla ya Setien.

Lakini ni ukweli uliowazi kwamba, Xavi hawezi kwenda pale Barcelona chini ya bodi ya wakurugenzi wa sasa na rais aliyepo.

4. ROBERTO MARTINEZ

Alionekana ndio mrithi wa Ernesto Valverde kabla ya ujio wa Setién, na jina la Roberto Martínez bado linazungumzwa katika viunga vya Barcelona kama ndio kocha ajaye.

Bado ana mkataba na Timu ya Taifa ya Ubelgiji, lakini Martínez anaweza kuwa mtu sahihi zaidi kwa kikosi hicho. Yeye ni kocha mzuri, lakini rekodi zake hazionyeshi kama ndoto ya Barça.

Muda wake pale Everton ulimalizika kwa aina yake, na ingawa kikosi chake cha Ubelgiji kinafanya vizuri, anaweza kufikiriwa kutua Katalunya.

5. MASSIMILIANO ALLEGRI

Kocha wa zamani wa Juventus, Massimiliano Allegri inaaminiwa kwamba alikataa nafasi ya kujiunga na Barcelona, lakini uvumi haujakoma kumhusisha na kazi hiyo.

Akiwa ameshinda mataji matano ya Ligi Kuu Italia, Serie A, kwa jina lake, Allegri anaonekana ni mtu anayefaa kuchukua mikoba pale Barcelona, lakini staili yake inaonekana kutofiti pale kwenye dimba la Camp Nou.

Kikosi chake cha Juventus kilikuwa kinacheza soka la taratibu kitu ambacho ni kinyume na Barcelona. Anaweza kupewa mikoba hiyo kwa kufuata mfumo wa uchezaji wa kikosi hicho.

6. LUIS ENRIQUE

Akiwa ameshinda mataji matatu katika mwaka wake wa kwanza na mataji mawili mwaka uliofuata, Luis Enrique bado ana nafasi kubwa ya kuchukua mikoba ya Barcelona.

Mtazamo wake na aina ya uchezaji wa timu yake, ulileta kitu fulani cha kuvutia kwa kikosi hicho na bado Enrique kazi yake inathaminiwa pale Katalunya kwa kipindi cha miaka mitatu aliyokaa.

Kwa sasa ni kocha wa Timu ya Taifa ya Hispania, lakini Enrique hajawahi kuacha kuonyesha mapenzi yake kwa kikosi cha Barcelona, hivyo ana nafasi ya kurudi kwenye klabu hiyo na kuachia majukumu ya kulinoa taifa hilo.

7. RONALD KOEMAN

Ni gwiji wa Barcelona na Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Uholanzi, Ronald Koeman na anapendwa zaidi na mashabiki wa pale Camp Nou, hivyo uwezekano wa kutua pale ni mkubwa zaidi kwa siku za usoni.

Koeman anaelewa njia zote za mfumo ulioasisiwa na Johan Cruyff na mara zote yupo tayari kujaribu kuendelea kuufanyia kazi. Kumiliki mpira na kuamini vijana ndio sehemu ya mfumo huo.

Muda wake pale Everton haukuwa mzuri, lakini amejenga heshima kubwa akiwa na Uholanzi. Na kuna uwezekano wa kupewa nafasi ya ukocha katika kikosi hicho.

8. MARCELO GALLARDO

Marcelo Gallardo bado hajajijaribu yeye mwenyewe barani Ulaya, lakini rekodi yake na kikosi cha River Plate cha kule Argentina ni ya kuvutia.

Kutokana na staili yake amekuwa mmoja wa makocha vijana maarufu sana na anajulikana pia pale Camp Nou, anapenda soka la kushambulia mwanzo mwisho na ameiwezesha timu yake kucheza soka la kuvutia zaidi.

Tatizo moja tu ni kwamba, hajawahi kuinoa timu yoyote barani Ulaya zaidi ya kuwa kule Amerika Kusini. César Luis Menotti na Gerardo Martino walishindwa kutamba walipojaribu kwenda Ulaya – je, Gallardo ataweza?

9. FRANCISCO GARCIA PIMIENTA

Inaonekana kama Barcelona wanasubiri tu muda wa kumpandisha kocha wa timu ya akiba, Francisco García Pimienta kwenye kikosi cha kwanza.

Anaonekana mmoja wa makocha wanaoufahamu vizuri mfumo wa timu pale Camp Nou, kwani Pimienta amekaa miaka 14 kwenye akademi ya klabu hiyo. Anajua namna ya kuwalea vijana wenye vipaji, na anauwezekano mkubwa akapandishwa kwenye kikosi cha wakubwa.

Kiukweli wengi wanamfananisha na Pep Guardiola, kwamba anafanana kwa vitu vingi na hasa ikichukuliwa kwamba naye alitokea kwenye kikosi B na kuja kutamba sana katika timu ya wakubwa. Wanaweza kutumia mfano huo kumpa mikoba ili kuiwezesha Barcelona kurudi kwenye nafasi yake.

Habari Kubwa