Makocha wa4 waliokalia kuti kavu EPL kwa sasa

02Dec 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Makocha wa4 waliokalia kuti kavu EPL kwa sasa

MSIMU wa Ligi Kuu England unazidi kushika kasi, huku hadi sasa mechi 13 zimechezwa na timu zipo kwenye nafasi zao (kabla ya mechi za juzi Jumamosi na jana Jumapili).

Liverpool na Manchester City walitarajiwa kuwa kwenye mbio moja, lakini tofauti na matarajio ya wengi kikosi cha Jurgen Klopp kimewaacha vijana wa pale Etihad kwa tofauti ya pointi nane, na nafasi ya pili wakiwa Leicester City wanaonolewa na kocha, Brendan Rodgers.

Leicester pamoja na Sheffield United, wamefanya kile kisichotarajiwa na wengi na kujikuta wakiwa na kiwango cha kuvutia zaidi.

Leicester kwa sasa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo baada ya mechi 13.

Manchester United na Arsenal, klabu kubwa mbili zilizokuwa na mafanikio chini ya makocha, Sir Alex Ferguson na Arsene Wenger, sasa zimeachwa nje kabisa ya nne bora.

Tottenham Hotspur, nayo imekuwa kwenye wakati mgumu kwa mwanzo mbaya na baadae wakaamua kuachana na kocha, Mauricio Pochettino na nafasi yake ikichukuliwa na Jose Mourinho.

Katika soka, timu ikiwa na matokeo mabaya, kocha ndio mtu wa kwanza kubeba msalaba, sasa wakati tayari makocha kadhaa wameshatimuliwa akiwamo Unai Emery wa Arsenal, hapa tunawaangalia makocha wanne waliokalia kuti kavu kwenye Ligi Kuu England maarufu EPL.

 

4. Ralph Hasenhuttl - Southampton

Tangu alivyochukua mikoa kutoka kwa Mark Hughes, Desemba mwaka jana, Ralph Hasenhuttl, ameshindwa kuiweka Southampton kwenye ramani nzuri. Sasa klabu hiyo imejikuta yenyewe kwenye hatari ya kushuka daraja, ikiwa imepata pointi tisa tu katika mechi 13.

Southampton haijashinda mchezo wowote kati ya mechi tano zilizopita kwenye Ligi Kuu, ikiwamo kichapo cha mabao 9-0 kutoka kwa Leicester City wakiwa nyumbani na sasa kocha huyo raia wa Austria yupo kwenye hatari ya kufukuzwa.

Tangu hapo, kikosi hicho kimepambana na kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Arsenal kwenye Uwanja wa Emirates, lakini Hasenhuttl anaweza kuwa kocha anayefuatia kufukuzwa kwenye ligi hiyo, kama matokeo yataendelea kuwa hivyo, huku Southampton wakiwa kwenye hatari ya kushuka daraja.

 

3. Manuel Pellegrini - West Ham United

Ingawa West Ham walianza vizuri msimu na walipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Manchester United Oktoba mwaka huu. Tangu hapo kikosi hicho cha kocha, Manuel Pellegrini kimeshindwa kushinda mchezo wowote kwenye Ligi Kuu na kujikuta kikiwa na matokeo mabaya kila wiki.

West Ham iliimarisha kikosi chake kwa kutumia fedha nyingi kuwasajili Pablo Fornals na Sebastien Haller kipindi cha majira ya joto, lakini wameshindwa kufikia kile walichokiacha msimu uliopita na sasa bila shaka nafasi ya Pellegrini klabuni hapo ipo shakani.

Wagonga nyundo hao wa jiji la London kwa sasa wamejikuta wakiwa juu kwa pointi tatu tu kutoka mstari wa kushuka daraja wakiwa nafasi ya 16 kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Pellegrini ni mshindi wa taji la Ligi Kuu England akiwa na Manchester City, lakini West Ham wanaweza kuachana nae ndani ya wiki chache zijazo, kama matokeo ya klabu hiyo hayatabadilika.

 

2. Marco Silva - Everton

Nafasi ya Marco Silva pale Everton ipo shakani hasa katika wiki za hivi karibuni, wakati Toffees hao wakijikuta wenyewe wakiwa nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi baada ya mechi 13. Klabu hiyo ya pale Merseyside ilifanya kazi nzuri kwenye dirisha la usajili ikiwa moja ya timu 6 zilizotumia kiasi cha pauni milioni 100 kwenye usajili, wakiwa kwenye harakati za kufuzu kwenye Ligi ya Europa.

Ni Norwich City na Watford pekee ndio zilizopoteza mechi nyingi zaidi kuliko Everton msimu huu.

Katika wiki za hivi karibuni, mashabiki na wachambuzi wa soka, wamepaza sauti zao kutaka kocha huyo raia wa Ureno kuondoka klabuni hapo. Muda unaonekana kwenda kwa kasi zaidi kwa kocha huyo wa zamani wa Hull City na kama matokeo yataendelea kuwa mabaya, kuna uwezekano mkubwa nafasi ya Silva akapewa mtu mwingine ndani ya siku chache zijazo.

 

1 Ole Gunnar Solskjaer - United

 

Manchester United imeanza msimu wa Ligi Kuu vibaya zaidi, licha ya kuwa moja ya klabu iliyotumia fedha nyingi kwenye usajili wa kipindi cha majira ya joto na sasa kocha, Ole Gunnar Solskjaer anaoneka wazi kwamba amekalia kuti kavu. Raia huyo wa Norway alionekana kuwa kwenye nafasi nzuri wakati alipochukua mikoba ya Jose Mourinho, lakini tangu alipopewa mkataba wa kudumu, matokeo ya timu hiyo yamekuwa sio ya kuridhisha.

United walikuwa na nafasi nzuri katikati ya wiki iliyopita, wakati walipotoka nyuma ya mabao mawili dhidi ya Sheffield United na kuongoza 3-0 pale kwenye dimba la Bramall Lane. Lakini Blades hao wakafanikiwa kulazimisha sare ya 3-3 wakati Oliver McBurnie alipofunga dakika ya mwisho. Kwa kiasi kikubwa matokeo ya United yamekuwa sio ya kuvutia, huku pia wakitoka kuchapwa mabao 2-1 kwenye Ligi ya Europa Alhamisi iliyopita.

Kocha Mauricio Pochettino kwa muda mrefu amekuwa akihusishwa na mpango wa kuchukua nafasi katika kikosi cha Manchester United na tangu raia huyo wa Argentina afukuzwe pale Tottenham Hotspurs wiki iliyopita, kibarua cha Solskjaer kinaweza kuwa kwenye wakati mgumu zaidi kwa wiki zinazokuja.

Kwa sasa United inashika nafasi ya tisa ikipitwa pointi 9 nyuma ya Chelsea iliyopo nafasi ya nne.

Habari Kubwa