Malawi yavunja rekodi ya Kenya

01Jul 2020
Mashaka Mgeta
Dar es Salaam
Nipashe
Malawi yavunja rekodi ya Kenya
  • *Yapata Rais anayependa kuimba hata akiwa bafuni

KENYA iliweka historia kwa mahakama nchini humo kutengua matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2017, lakini sasa Malawi imeipiku kwa kuwa nchi ya kwanza Afrika kufuta matokeo ya uchaguzi wa urais na kuandaa duru ya pili na upinzani kuibuka na ushindi.

Mwaka 2017, upinzani Kenya ulichukua hatua hiyo iliyofanyika Malawi, kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais yaliyotenguliwa na mahakama, lakini kinara wa upinzani nchini humo, Raila Odinga wa ODM alisusia duru ya pili na kusababisha ‘ushindi wa kishindo’ kwa Rais Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee.

Hali kama hiyo ya kususia uchaguzi, ilijitokeza katika uchaguzi wa 2015 visiwani Zanzibar ambapo aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi visiwani humo, Jecha Salum Jecha aliufuta uchaguzi na kuitisha uchaguzi wa marudio ambao chama kikuu cha upinzani visiwani humo, Civic United Front (CUF) kiliususia.

Wachambuzi wa kisiasa wanasema matokeo ya uchaguzi kutokana na kutowajibika kwa tume limeendelea kuwa tatizo sugu barani Afrika na kuwa katika nchi nyingi.

Mahakama na tume za uchaguzi ni vyombo vinavyoongozwa na wateuliwa wa marais waliopo madarakani na hivyo kuwa kishawishi cha kuelemea upande wa waliowateuwa.

Gambia inatajwa kuwa miongoni mwa nchi chache kwa kuwa na tume yenye uadilifu, ikitolewa mfano kuwa mwaka 2017, ilimtangaza kiongozi wa upinzani Adama Barrow kuwa mshindi halali dhidi ya rais aliyekuwa madarakani kwa muda mrefu Yahya Jammeh.

Tukio kama hilo la mabadiliko ya kidemokrasia katika kanda ya kusini mwa Afrika, liliwahi pia kujitokeza Zambia ambapo rais wa kwanza Kenneth Kaunda, alikubali kushindwa na mpinzani wake Frederick Chiluba.

NI HISTORIA MALAWI

Katika uchaguzi mkuu uliofanyika Juni 23, mwaka huu, aliyekuwa mgombea urais kupitia chama cha Malawi Congress Party (MCP), Lazarus Chakwera, alishinda kwa kupata asilimia 58.57 dhidi ya rais aliyekuwa madarakani, Dk.Peter Mutharika aliyepata kura 1,751,377 na nafasi ya tatu kuchukuliwa na Peter Dominico Kuwani aliyeambulia kura 32,456 huku waliojitokeza kupiga kura wakitajwa kuwa ni asilimia 64.81.

Kiongozi huyo amekuwa akijihusisha na kamati ya masuala ya umma yenye misingi ya kidini na mashirika ya kutetea haki za kiraia, akiwa kama mtetezi wa masuala ya uongozi bora.

Rais huyo mpya wa Malawi anayezungumza Kiingezera cha lafudhi ya Kimarekani anasema anapenda kusoma na muziki wa kiasili, wa kigeni na nyimbo za Injili.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, anapenda kuimba sana hata akiwa peke yake bafuni akioga.

Kwa ujumla uchaguzi huo wa duru la pili ulifanyika baada ya mahakama nchini humo kuyafuta matokeo ya uchaguzi wa awali yaliyompa ushindi Mutharika.

Katika uchaguzi huo, Mutharika alitangazwa kupata ushindi mwembamba wa kura 159,000 – sawa na asilimia 38.6 ya kura zilizopigwa huku Chakwera akifuatia kwa nafasi ya pili akiwa na asilimia 35.4.

Chakwera na mgombea aliyekuwa katika nafasi ya tatu waliyapinga matokeo hayo kwa madai kwamba uchaguzi huo haukuwa huru na haki.

Miongoni mwa hoja zao ni kwamba nakala za kuhesabu kura zilifutwa na kuongezewa idadi ya kura kwa kutumia wino wa kusahihisha makosa.

Kupingwa kwa matokeo hayo kulizua maandamano na ghasia kati ya wafuasi wa upinzani na polisi nchini humo.

Ingawa maelfu ya raia wa Malawi walishangilia kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa awali, Mutharika akautaja uamuzi huo kama “mabadiliko yanayoadhimisha mwanzo wa mwisho wa demokrasia nchini humo.”

Licha ya kutenguliwa kwa matokeo ya awali, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini humo, Jane Ansah alijiuzulu kufuatia miezi kadhaa ya shinikizo la waandamanaji waliomkosoa kwa jinsi alivyosimamia uchaguzi huo.

Ushindi wa Chakwera dhidi ya Mutharika licha ya kuungwa mkono na wapinzani wengine, unakirejesha madarakani chama kilichoasisiwa na Dk Banda cha Malawi Congress MCP kwa mara ya kwanza, miaka 26 baada ya kuondoshwa madarakani.

Baada ya matokeo ya awali kuonyesha kwamba kimeshindwa, kilichokuwa chama tawala cha Democratic Progressive Party (DPP) kilitoa wito wa kurudiwa kwa uchaguzi huo kwa madai ya kukumbwa na udanganyifu na vitisho.

DPP ikaitaka tume ya uchaguzi nchini humo kutupilia mbali matokeo hayo na kutaka kufanyika kwa uchaguzi wa tatu.

Katibu wa chama hicho Francis Mphepo, anasema, "tungependa kuangazia matukio kadhaa ambayo huenda yakatia dosari uaminifu na uadilifu wa matokeo ya ya uchaguzi wa urais."

Chama hicho kiliorodhesha vituo ambavyo kilidai wasimamizi wake walitolewa nje na kusema zaidi ya kura milioni 1.5 zilichakachuliwa.

"Hakuna shaka yoyote kwamba vitendo vya udanganyifu vitaathiri matokeo kwa namna moja au nyengine,"Mphepo anakaririwa na vyombo vya habari akisema.

BAIBAI IKULU

Siku nne baada ya kufanyika kwa uchaguzi huo, Mutharika hakuwa na namna nyingine zaidi ya kuanza kuizoea hali ya kuondoka ikulu, pale aliposema ingawa hakubaliani na matokeo lakini Malawi na Wamalawi walipaswa kusonga mbele.

Chakwera ameapishwa kuwa rais mpya wa Malawi kupitia hafla iliyofanyika jijini Lilongwe.

Mwandishi wa BBC Kusini mwa Afrika, Andrew Harding, anasema si jambo la kawaida kwa mahakama za nchi za Afrika kufuta matokeo ya urais, ingawa suala hilo linawavutia watu wengi pale mahakama inapoingilia kati na kubadilisha matokeo katika eneo ambalo wizi wa kura ni suala la nyeti.

Baada ya matokeo rasmi kutangazwa Chakwera anautaja ushindi huo kuwa ni ishara thabiti ya demokrasia na haki, huku akiweka wazi namna roho yake ilivyojawa na furaha.

MAANA YA USHINDI

Matokeo ya uchaguzi huo yametafsiriwa kwa namna tofauti na wachambuzi wa masuala ya siasa, wengi wao wakielezea sababu kuwa ni hatua ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na mahakama nchini humo, kujitenga na ushawishi wa ikulu au watawala.

Baada ya kufutwa kwa matokeo ya awali, Mutharika alikata rufani katika mahakama ya rufani kupinga uamuzi huo, lakini akashindwa.

MUTHARIKA AFUNGUKA

Kama ilivyokuwa kwa wapinzani katika matokeo ya uchaguzi wa awali, Mutharika naye akautaja uchaguzi wa duru la pili kwamba ni mbaya zaidi uliowahi kushuhudiwa nchini humo.”Ni uchaguzi ambao haki haikutendeka.”

Akizungumza baada ya kupiga kura kusini mwa Malawi, Mutharika alidai na kukaririwa na Shirika la Habari la Reuters, kwamba kulikuwa na ghasia katika maeneo ya upinzani.

''Inasikitisha. Katibu Mkuu wetu amepigwa, wanaosababisha ghasia hawana la kufanya,'' alinukuliwa akisema na kisha kuhoji, “ni vipi sasa kwamba uchaguzi huu utakuwa wa haki na huru?''

KUUNGANISHA TAIFA

Vyombo kadhaa vya habari vimekariri vyanzo tofauti vukielezea kwamba pamoja na mambo mengine, Rais Chakwera anakabiliwa na changamoto ya kuwaunganisha Wamalawi kufuatia mgawanyiko uliojitokeza, na kumaliza ghasia zilizoshuhudiwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Hali hiyo inawiana pia na kudhibiti vitendo vya ufisadi, kupunguza umaskini na ukosefu wa ajira, mambo ambayo yalikuwa ni miongoni mwa masuala ya msingi katika uchaguzi huo.

Shirika la habari la AFP, limesema kuwa Rais huyo anapenda kuimba sana hata akiwa peke yake bafuni akioga.

Habari Kubwa