Mama wa mwenye ualbino asimulia majaribu ya mkunga

26Mar 2020
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Mama wa mwenye ualbino asimulia majaribu ya mkunga
  • Asifu ushujaa wa mume ulivyombadili

STELLA Bulinda ni mama wa watoto wawili, wenye ualbino. Binafsi anaanza kwa shukurani kupitia imani ya imani ya Mungu, akieleza anawapenda sana wanawe.

Stella Bulinda, mkazi wa Bunju jijini Dar es Salaam, alopozungumza mafunzoni. PICHA: ROMANA MALLYA.

Mama huyo, mwaka 2017 alipojifungua mtoto wa kwanza wa kike, alitekwa na fikra za kukatishwa tamaa, kupitia kauli ya muuguzi aliyemhudumia baada tu ya kujifungua.

Ilikuwaje? Stella, mkazi wa Bunju jijini Dar es Salaam, aliyeolewa na mume anayemtaja kwa jina la Bulinda, alisimulia hayo hivi karibuni, katika mafunzo ya wanawake walio na watoto wenye ualbino, kwenye maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.

Ilikuwa Jumamosi ya Machi 7 ikiwa ni siku moja kabla ya kilele cha maadhimisho hayo, wanawake wenye watoto walio na vinasaba hivyo, walikutana katika viwanja wa Shirika la Kimataifa la Under The Same Sun (UTSS) jijini Dar es salaam, kujadili siku yao.

Anasema, mada kuu haikulenga zaidi kuzamakatika changamoto zao, ingawa kauli ya Stella iliangukia msingi wa ‘kila penye mafanikio, matatizo hayakosekani’ au kinyume chake.

ILIKUWAJE?

Stella anasimulia mwaka 2017 alipojifungua mtoto wa kwanza baada ya kuolewa, muuguzi alimtamikia kauli iliyobeba maudhui anayotafsiri ama ni kejeli na kashfa, kupitia swali: “Mtoto wako ni huyu umejifungua wa kike, kwenu kuna hawa?.”

Mzazi huyo anaeleza mapokeo ya hisia yake, akisema: “Kauli hii ilinipa shauku kutaka kumuona mtoto niliyejifungua ni wa aina gani na kwa haraka akilini mwangu nilijiuliza nimejifungua nini? kwa nini kauli hiyo ya muuguzi?

“Haraka nilimchukua mtoto, ndipo nilipobaini nimepata mtoto mwenye ualbino, ingawa sikutarajia kujifungua mtoto mwenye ualbino. Lakini kama ilivyo kwa mama yoyote duniani akijifungua, kauli kama ile aliyoitoa muuguzi ilinikatisha tamaa na kunivunja moyo.

“Kwa kweli kama mzazi na kitu ambacho sikutegemea, ilinishtua sana na niliumia sana kwa muda ule.Nilimchukua mtoto wangu, nikambeba na muuguzi alipoondoka nilichukua simu na kumpigia mume wangu ambaye wakati ule alikuwa nje.”

Stella anaendelea: “Kama ilivyo kwa mama yoyote duniani anapojifungua huwa na shauku la kumjulisha mzazi mwenza, ndivyo nilivyofanya. Nilimpigia simu mume wangu kumpa habari njema kuwa tumepata mtoto wa kike.”

Stella anasimulia kuwa mume wake alipopokea simu, alimtamkia:“Tumepata mtoto wa kike kama ulivyokuwa unahitaji na mtoto wetu ana ualbino.”

Mwanamke huyo anasema, tofauti na matarajio yake, mumewe alikuwa wa kwanza kumfanya ajione ni mwanamke pekee na mtoto waliompata ni baraka kutoka kwa Mungu.

Anaendeea kusimulia mkasa wa historia hiyo, akinukuu marejeo ya mume:“Hakuna shida mke wangu mpenzi, kila kitu ni mpango wa Mungu. Kwa hiyo, usimpangie Mungu, shukuru Mungu umejifungua salama na mpo salama na mtoto na umejifungua mtoto ambaye ni ‘special’ (wa kipekee).”

Stella ambaye ni mfanyabiashara, anasema ni kauli iliyompa faraja iliyomfungulia ukurasa mpya wa kiimani, ajione amebarikiwa, tofauti na wenzake wodini.

“Huwezi amini, wakati naondoka wodini nikiwa na mtoto na mume wangu, nakumbuka ilikuwa siku ya pili baada ya kujifungua. Nilijiona ni mwanamke aliyebahatika kupata mtoto wa pekee.

“Wakati ninaondoka wodini, wanawake wenzangu walikuwa wananishangaa, wauguzi wananishangaa, sijui walitegemea tofauti. Nilijawa amani moyoni na uso wenye tabasamu. Hii yote ilitokana na maneno ya mume aliyonieleza, nilipompa habari njema ya kujifungua salama,” anasema.

Stella anasema baada ya kufika nyumbani, mtu wa pili ambaye alimtia moyo ni baba wa kiroho (kiongozi wa kiimani ), aliyewaita na mume wake azungumze nao.

“Nakumbuka maneno yake aliniambia Stella, mshukuru Mungu umetoka salama. Halafu mtoto ni zawadi kutoka kwa Mungu na Mungu amekupa kwa sababu anajua unaweza kumlea na kumtunza. Wewe ni wa pekee amekupa mtoto wa pekee.

Anakiri kauli hiyo ya pili, iliwanya wote wawili kutembea ‘kifua mbele’ na kuzidisha upendo zaidi kwa mtoto wao, huku wakati wote wakimuombea akue na kufikia kutimiza ndoto zake.

Stella anasimulia kwambna, wakati akiendelea na malezi ya mtoto wake wa kwanza, mwaka uliofuata 2018, alibarikiwa kujifungua mtoto wa pili wa kiume, naye alikuwa mwenye ualbino.

“Nakumbuka wakati najifungua mume wangu alikuwa safarini. Nilimpigia simu kumtaarifu kuwa nimejifungua salama na mtoto tuliyempata ni wa kiume na amefanana na mtoto wetu wa kwanza.

“ Kama kawaida ya mume wangu, alipokea taarifa hii kama ilivyokuwa ya mtoto wetu wa kwanza,” anasema.

JAMII INAVYOMCHUKULIA

Stella anasema, kwa kawaida ni vugumu majirani kuzungumza chochote, lakini siyo wote walioelewa hali hiyo.

Aanaendelea:“Kukwambia moja kwa moja mpaka sasa sijawaona watu wa namna hii, ila kuna baadhi ya watu naona wanapungua katika maisha yangu.

“Ila kupungua kwao katika maisha yangu, haikunikatisha tamaa, kwa sababu kuna watu wananishika na kuwa bega kwa bega name. Wa kwanza ni mume wangu mpenzi tumeshikana pamoja.

“Mwingine ni mama yangu na watumishi ambao walitumwa na Mungu kwa ajili ya familia yangu wamekuwa nasi bega kwa bega.”

NENO LAKE

Stella ana wito kwa jamii kuwa wanapaswa kuwa na uelewea mzuri, pindi wanapojifungua mtoto mwenye ualbino, kwani daima hakuna ubaya, bali ina upekee kama iivyokuwa kwake.

Pia, anatahadharisha tabia ya wanaume wanaokimbia familia mara wapatapo mtoto mwenye ualbino, hata marukio ya mwanamke kumtelekeza mtoto.

“Mshukuru Mungu na umwambie ‘ninakuangalia wewe kwa sababu wewe ndiye uliyenipa mtoto huyu mwenye ualibino na kwa sababu unajua ninao uwezo wa kumlea, kumlinda na kufanikisha ndoto zake,” anasema, akisisitiza mzazi kumuwajibikia kila mtoto.

Moja ya eneo muhimu anazozitaja ni kuwawezesha watoto kujitambua, wapewe ulinzi na haki yao ya kupata elimu na kuelimika, ili wawe na tafsiri sahihi ya ualbino na maisha yao.

“Tukifanya hivyo hatutaongelea mauaji, hatutaongelea unyanyapaa, hatutaongelea baba au mama kukimbia familia, tutalisaidia kundi hili kutembea zaidi kifua mbele mijini na vijijini, iwe mchana au usiku,” anasema.

“Binafsi katika mafunzo haya, nimejifunza zaidi upendo na ushirikiano siyo tu kwa watoto wenye ualbino, bali pia kwa jamii kwa ujumla. Ninalishukuru Shirika la Under The Same Sun kwa kuandaa mafunzo haya ambayo naamini tulivyokuja ni tofauti na tutakavyoondoka,” anasema.

Habari Kubwa