Mambo hayo! Nigeria Mahari mtindo wa kodi

15Nov 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Mambo hayo! Nigeria Mahari mtindo wa kodi

NI takribani miezi minne sasa hakuna ndoa iliyofungwa katika kijiji kimoja la jimbo la Kano, nchini Nigeria tangu chifu wa eneo hilo kuanzisha malipo ya kodi ya harusi.

Jamii ya Nigeria ikifurahia harusi. PICHA: Bbc

Ado Sa'id, ni chifu wa kijiji cha Kera, Kaskazini Magharibi mwa nchi hiyo, amewataka mabwana harusi kulipa kodi ya kiasi cha dola 377 (sawa na Sh. 878, 400).

Hiyo ni mbadala wa utamaduni uliopo wa kulipa samani, vyombo vya jikoni na vitu vingine vya thamani, kwa familia ya bibi harusi watakapofunga ndoa.

Kiongozi huyo anasema kuwa, kulipa kodi ni rahisi zaidi kuliko mahari na itawafanya watu wengi kufunga ndoa kirahisi na utekelezaji wake, utaanza baada ya kushauriana na wanakijij, jambo ambalo lilipingwa vikali.

Wanakijiji wanadai utaratibu wa zamani ulikuwa mzuri na waliweza kununua zawadi wanavyotaka.

Mwanakijiji, Isah Kera, anasema sheria mpya inawalazimisha wapenzi kwenda kufunga ndoa sehemu nyingine, ili kukwepa kodi hiyo na mwenzake, Sani Kera, anasema ana watoto watano ambao wako tayari kuoa, lakini mipango yao imebidi ihairishwe.

Wakati Nigeria wanalalamikia kodi kwenye harusi, vijana wa kwingineko Afrika, wanalalamikia gharama kubwa ya mahari katika jamii zao.

Nchini Uganda, utamaduni huo ni wa kawaida kwa jamii zilizopo katika maeneo ya mashinani, pia hutolewa katika maeneo ya mijini. Mahari nchini humu hufuata msingi ambao umekuwapo kutoa kitu ili upewe mke.

Lakini sasa, kuna mtindo wa baadhi ya familia kuandikishana mikataba na bwana harusi kama ithibati ya kulipa mahari anayoitishwa.

Inaaminika, iwapo mke anamtoroka mumewe, familia yake inawajibika kulipa mahari.

Mwaka 2010, mahakama nchini humo iliamua utoaji mahari ni halali, lakini majaji walipiga marufuku mtindo wa kurudishwa wakati ndoa inapovunjika.

Nchini Kenya, sheria haishurutishi ulipwaji mahari, lakini ni jambo linalofahamika rasmi katika jamii.

Baadhi ya jamii, kwa mfano za wafugaji husisitiza mahari ya mifugo na jamii nyinginezo pesa taslimu na hata madini hupokewa kama mahari.

Utamaduni wa kutoa mahari upo katika nchi nyingi, ikiwamo barani Asia, pia Mashariki ya Kati

Maana ya mahari

Kiwango kinachotolewa kumposa binti, hutofautiana kuanzia zawadi ndogo tu za kuendeleza utamaduni huo hadi maelfu na mamilioni ya shilingi.

Tangu jadi, utoaji mahari umekuwa utamaduni unaoheshimiwa na kuenziwa pakubwa hata miongoni mwa jamii za watu waliosoma na kuishi maisha ya kisasa.

Kwa kawaida mahari ni kama mkataba wa makubaliano kabla ya ndoa ambapo mali kama ng'ombe, ngamia, mbuzi au hata pesa taslimu hulipwa na bwana harusi kwa familia ya bibi harusi ili apewe mke.

Iwapo mume hatotimiza mahari iliyokubaliwa kwa muda uliotolewa, kuna jamii ambazo zinamrudisha mke nyumbani mpaka mume akamilishe kulipa mahari.

BBC

Habari Kubwa