Mamlaka habari zatafsiri kinachonaswa na ‘CCTV’ unyanyasaji jinsia

26Nov 2021
Jenifer Gilla
Dar es Salaam
Nipashe
Mamlaka habari zatafsiri kinachonaswa na ‘CCTV’ unyanyasaji jinsia
  • Wasomi wao wakokotoa ya utafiti

SEHEMU ya kwanza ya makala hii imeripoti unyanyasaji kijinsia ndani ya vyombo vya habari, kukiwapo ushuhuda walioguswa moja kwa moja, pia wasimamizi wao wakianika uhalisia.

Nipashe sasa inahamia wadau wakuu wa sekta wanavyozungumzia mustakabli, ikianza na utafiti wa shirika la WAN-IFRA Women in News kuhusu unyanyasaji kijinsia katika vyombo vya habari.

Hapo unaonyesha nusu ya wanawake katika vyumba vya habari Afrika wanafanyiwa unyanyasaji kijinsia, lakini wanaoripoti wachache wakikatishwa tamaa na hatua nyepesi zinazochukuliwa, ikiwamo kuishia kuonywa.

Mratibu wa WAN-INFRA/women Tanzania Dk. Joyce Bazira, anasema kuwapo sera katika vyombo vya habari kutawapa ujasiri wanahabari kutoa taarifa wanaponyanyaswa kijinsia.

“ Wapo waandishi wanaotamani kuripoti matukio ya unyanyasaji, lakini wanahofia kukosa ajira zao kwa kuwa hakuna sera zinazowalinda ndani. Hivyo, ni muhimu vyombo hivyo vikafikiria kutengeneza sera za ndani” anasema.

Dk. Bazira, mkongwe katika vyumba vya habari, mshiriki utafiti na mtoaji elimu kuhusu unyanyasaji kupitia asasi kama vile WAN-IFRA / Women in News na Chama cha Wanadishi wa Habari Wanawake (TAMWA), anashauri sera hiyo iambatane na mambo kadhaa.

Anayataja kuwa ni elimu, uhamasishaji jamii na undani wake, kuondoa utamaduni uliojengeka kwamba “ni jambo la kawaida, halipaswi kusemwa na jamii.”

Msomi huyo anafafanua: “Kuna watu wanafanyiwa unyanyasaji wa kijinsia bila ya kujua wakidhani ni jambo la kawaida. Mfano, unamsalimia mwanamume kwa kumpa mkono, halafu anakutekenya kwenye kiganja. Ule ni unyanyasaji, lakini wengi wanachukulia kama ni hali ya kawaida.”

Pia, anataja wanaume wanaonyanyasa pasipo kujitambua wanakosea, kwa sababu ya kukosa elimu sahihi, akitoa mfano anapomkonyeza mwanamke asiye mke wake.

Mwanahabari wa kujitegemea, Christina Stephen, anaungana na Dk.Bazira, akisema wanaogopa kuripoti matukio ya unyanyasaji wa kijinsia ili kulinda maslahi yao.

“Unakuta aliyekufanyia kitendo cha unyanyasaji ni bosi wako na ndiye anaamua habari hii itoke ukurasa gani. Ukienda kumshtaki, anaweza kukuwekea chuki na kukukomoa,” anasema Christina, akitaja mbadala unaochukuliwa na anayeonewa ni kuvumilia.

Mwandishi wa habari wa Gazeti la Mwananchi na Mkuu wa Kitengo cha Takwimu, Halili Letea anasema utamaduni na malezi waliojengewa wanawake kuwa baadhi ya mambo hayapaswi kuripotiwa, yanawachangia wasitoe taarifa wanaponyanyaswa, yabaki kuwa siri.

“Hii inawapa mwanya viongozi wa kiume kuendeleza haya matendo machafu, kwa hivyo sera ni muhimu katika vyombo vya habari,” anasema.

Letea anatoa ushahidi wa mwanahabari wa kike jasiri, aliyetoa taarifa za kunyanyasika kingono na bosi wake kwa kushikwa faragha ya umbo, hata ofisi yao ikaamua kuongeza idadi ya kamera kunasa vyema matukio aina hiyo ili yachukuliwe hatua.

Mwandishi wa habari wa gazeti moja la jijini Dar es Salaam, Rachel Imanuel (sio jina lake kamili) anakiri kupitia unyanyasi kingono kazini na hakutoa taarifa kwa kuhofia kuweka ajira yake rehani.

“Sasa ukishamshitaki bosi itakuwaje? Wakati hakuna sheria ya ndani . Hata sisi waandishi wa habari wa kujitegemea, unaweza kupoteza ajira dakika moja tu. Kukiwa na sheria ya kupinga unyanyasaji katika vyumba vya habari, itatupa nguvu hata sisi kutoa taarifa,” anasema Rachel.

FEMNET

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Wanawake, (FEMNET), Memory Kachambwa, anasema kukosekana sera ya kushughulikia unyanyasaji kijinsia kazini, kunasababisha vitendo hivyo kuwa endelevu.

Kachambwa anaeleza unyayasaji wa kijinsia kazini ni zao la kukosekana usawa wa mamlaka na dalili zake ni mazingira kama vile malipo ya chini kwa wanawake na wasichana kazini.

“Wanawake wakinyanyasika wanakosa ari ya kufanya kazi, hali inayowafanya kuacha kazi na kuhatarisha uwezeshaji wao wa kiuchumi.

“Hii ina athari kubwa katika shirika zima na inaweza kusababisha kudorora kwa ustawi wa shirika, hivyo sera ya ndani ni muhimu kulinda maslahi ya wanawake hawa,” anasema Kachambwa.

Mkuu huyo wa FEMNET anazisisitiza nchi za Kiafrika kuidhinisha mkataba wa 190 wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) ili kukomesha unyanyasaji kazini akianika kati ya nchi saba duniani zilizoridhia mkataba huo tatu ni za Afrika; Namibia, Somalia na Mauritius.

WAN-IFRA /Women in News

Mkurugenzi wa shirika WAN –IFRA, kwa nchi za Afrika, Jane Godia, anasisitiza haja ya kuwapo sera yenye viwango, miongozo na taratibu za kushughulikia kesi za unyanyasaji kijinsia endapo zitatokea, ikiwa na ufafanuzi wa hatua za kinidhamu kupopatikana hatia.

“Sera hii itawafungua macho waandishi wa habari wajue kuwa hawastahili kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji na ni muhimu sera hii ikumbushwe mara kwa mara kwa wahusika kupunguza au kuondoa kabisa unyanyasaji wa kijinsia,” anasema.

Mbobezi huyo wa zaidi ya miaka 20, pia mhariri, mkufunzi kwa wanahabari, anasema unyanyasaji huo unatokea kwa jinsia zote, lakini wanawake ni waaathirika wakubwa kutoka kwa mabosi.

Tathimini ya muundo na utendaji katika vyombo vya habari dhidi ya uhamasishaji wa usawa kijinsia na kupinga udhalilishaji wanahabari wanawake iliyofanywa na TAMWA unaeleza kuwa 25% ya wanawake wanahabari wamenyanyasika kijinsia kwa kurubuniwa kimapenzi; 17.2% kwa picha za mtandaoni; 15.2% shambulio la mwili; 12.4% kulazimishwa ngono na 4.8% walibakwa.

Habari Kubwa