Manyika: Kazama Mapinduzi Cup, kaibuka tena

09Jan 2017
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Manyika: Kazama Mapinduzi Cup, kaibuka tena

INAWEZEKANA michuano ya Kombe la Mapinduzi, ikaja kuwa na historia ya aina yake kwenye maisha ya kipa wa Simba, Manyika Peter.

Hatoweza kusimulia maisha yake ya soka bila kutaja michuano hii.

Alhamisi usiku alisimama langoni kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu kupita.

Ilikuwa ni mechi dhidi ya mabingwa watetezi wa michuano hiyo, URA kutoka nchini Uganda.

Mtoto huyo wa kipa wa zamani wa klabu ya Yanga na timu ya Taifa, Taifa Stars alisimama imara na kumaliza dakika zote 90 bila kufungwa.

Kilichompa sifa kwenye mechi hiyo na mashabiki wa Simba kukubali kuwa ameanza kurejea tena kwenye kiwango chake, ni kuokoa mashuti mawili kwa ustadi akikabiliana ana kwa ana na mastraika hatari wa URA.

Kwa muda mrefu kipa huyo hajaonekana langoni, huku msimu mzima uliopita akimezwa na kipa aliyetupiwa virago, raia wa Ivory Coast, Vicent Angban.

Ujio wa kipa Mghana, Daniel Agyei ulionyesha kuwa ndiyo mwisho wa maisha ya kipa huyo ndani ya klabu ya Simba.

Baadhi walishauri Manyika aondoke, ili Angban abaki kuwa msaidizi wa Agyei, jambo ambalo halikukubalika na viongozi wa klabu hiyo, ikawa kinyume chake.

Kwa mechi moja aliyocheza na kama ataendelea na kiwango kile, atakuwa ndiye msaidizi sahihi wa Agyei na Simba sidhani kama itaingia tena sokoni kusaka kipa mpya mwishoni mwa msimu.

Ikumbuwe kabla ya yote haya, Manyika ndiye alikuwa kipa namba moja kuanzia msimu wa 2014/15.

Nini kilimsibu kupoteza namba?

Kwa mujibu wa baba yake mzazi, Peter Manyika ni kwamba kijana wake hakusikiliza ushauri wake na kuwa na mambo mengi nje ya uwanja, zaidi ya umri wake.

Hili ndilo lililosababisha kushuka kwa kiwango chake kwa muda mfupi tu na kupoteza namba kwenye kikosi cha Simba.

Hata hivyo, alisema anashukuru hivi karibuni kijana wake alimfuata na kumuomba msamaha, naye akamrudisha kwenye kituo chake na kwa muda mfupi tu, tayari ameonekana kurejea kwenye kiwango.

Kipa huyo alipoteza namba pia kwenye Kombe la Mapinduzi mwaka jana.

Makosa yake ya kushindwa kuokoa mpira wa shuti hafifu la Shiza Kichuya wa Mtibwa Sugar wakati huo na kumruhusu Ibrahim Rajab Jeba kufunga dakika ya mwisho ya kipindi cha kwanza, yaliifanya Simba kuaga rasmi michuano hiyo kwa kufungwa bao 1-0 mechi ya nusu fainali.

Akaanza kutoaminika kwa wanachama, mashabiki na benchi la ufundi. Hatimaye akapoteza namba.

Kilele cha mafanikio yake

Mwaka 2015 ilikuwa ni kilele cha mafanikio cha kipa Manyika.

Awali alipangwa kwenye mechi ya Simba na Yanga msimu wa 2014/15 kwa mara ya kwanza na timu hizo kutoka sare ya bila kufungana. Kabla ya hapo alikuwa ni kipa wa kikosi cha pili cha Simba.

Alipata bahati hiyo kwa sababu tu, Ivo Mapunda kipa namba moja na Hussein Sharrif 'Casillas' wote walikuwa majeruhi.

Wengi walidhania kuwa alibahatisha. Michuano ya Kombe la Mapinduzi mwaka 2015 ndiyo iliyomtambulisha. Alidaka mechi zote na kuisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa.

Kwenye mechi ya fainali alitoka dakika za mwishoni na kumuachia Mapunda aliyeingia kwa ajili ya kudaka penalti, Simba ikashinda mabao 4-3 kwa matuta dhidi ya Mtibwa Sugar.

Baada ya hapo akawa kipa namba moja wa Simba kwenye mechi mbalimbali, ikiwamo Ligi Kuu.

Kombe la Mapinduzi lilimtoa, likamzamisha na sasa linaonekana kumuibua tena.

Habari Kubwa