Mapendekezo wadau NEC yanapoibua mjadala zaidi

25Aug 2021
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Mapendekezo wadau NEC yanapoibua mjadala zaidi
  • *Ni matamanio ya uchaguzi na haki

BAADA ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuiagiza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kupitia sheria za uchaguzi na kushirikisha wadau kwenye mchakato wa mapendekezo hayo, wachambuzi wa siasa wanasema suluhu ni katiba mpya itakayoleta tume huru ya uchaguzi.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji mstaafu Semestocles Kaijage (kulia), akisoma taarifa kwa Rais Samia Suluhu Hassan, katika hafla ya kukabidhi Ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020. PICHA: MTANDAO

Mjumbe wa Baraza Kuu la CUF, Taifa, Abdul Kambaya, anasema pamoja na Rais kuruhusu mjadala na mapendekezo ya wadau, suluhisho la yote ni kuwa na katiba na tume huru.

Rais Samia alitoa maagizo hayo, hivi karibuni, wakati akipokea taarifa ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, 2020 iliyowasilishwa kwake na NEC.

Kambaya akirejea maelekezo hayo anasema: "Uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, dunia iliahidiwa kwamba utakuwa huru na haki. Lakini tunajua kilichotokea, hivyo hata suala hili linaweza kutatuliwa na tume huru inayotokana na katiba mpya.”

Anaeleza kuwa tume huru inayotokana na katiba mpya, ni mwiba wa kasoro zote, kwa kuwa haitaegemea upande wowote, na kwamba itaondoa malalamiko yanayojitokeza kila uchaguzi.

"Kumbuka hata uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019, Watanzania waliahidiwa kwamba utakuwa huru, lakini figisu zilikuwa nyingi kuanzia wagombea kuchukua fomu hadi kuzirejesha," anakumbusha Kambaya.

Wasimamizi walifunga ofisi na kusababisha wagombea wa upinzani kukwama kuwasilisha fomu kwa wakati au kukosa fomu za kuomba kuwania nafasi za uongozi wa serikali za mitaa, anaongeza.

"Uwepo wa tume huru ya uchaguzi ndiyo suluhisho la yote hayo, kwani pamoja na ahadi za serikali kuruhusu mjadala wa mapendekezo ya wadau, hata wakurugenzi wa halmashauri wakiondolewa katika usimamizi wa uchaguzi, bado tume iliyopo viongozi wake wanateuliwa na Ikulu, hivyo tatizo liko pale pale," anasisitiza.

Anasema uzoefu unaonyesha kuwa imekuwa ni kawaida kuvuruga uchaguzi kwa madai ya kulinda maslahi ya wachache na kuzusha malalamiko ambayo kama kungekuwa na tume huru yasingekuwapo.

Wakati ikiwasilisha mapendekezo ya wadau kuboresha uchaguzi mkuu wa 2025, inataja uwezekano wa kuunganisha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura 343 na Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa Sura 292 kuwa ni miongoni mwa yaliyopendekezwa.

Aidha, mengine ni kutaka uchaguzi wa serikali za mitaa kusimamiwa na mamlaka moja.

Pamoja na hayo, mapendelezo mengine ni umuhimu wa NEC kuwa na wafanyakazi kwenye ngazi ya halmashauri badala ya kuwatumia wakurugenzi wa halmashauri.

Aidha, ilipendekezwa serikali kutoa fedha kwa ajili ya asasi za kiraia zinazotoa elimu ya mpigakura.

Rais Samia, anakumbusha kuwa katika uchaguzi huo, yapo matatizo yaliyojitokeza na ndiyo moja ya sababu ya kuandaliwa kwa ripoti hiyo na kuwekwa hadharani ili kutoa fursa kwa wadau wa uchaguzi na wananchi kuichambua na kutoa mapendekezo yao.

Anasema, jambo la muhimu ni wadau kujadili kwa kina, kwa kuwa kila suala linaloanzishwa lina msingi wake, kwamba, ili uchaguzi ukidhi malengo, ni lazima usimamiwe kikamilifu , lakini kinyume chake unaweza ukawa chanzo cha fujo na vurugu kama ambavyo imekuwa ikishuhudiwa katika baadhi ya nchi..

Anabainisha kuwa, mapendekezo yaliyotolewa na wadau ni ya msingi, na kwamba cha umuhimu ni kuyajadili kwa kina.
Maelekezo ya Rais Samia, yanafanana na yale yaliyowahi kutolewa baada ya mchakato wa katiba mpya kukwama 2014, ya kuelekeza baadhi ya sheria za uchaguzi kuangaliwa upya ili kuufanya uwe huru, haki na unaokubalika.

Baadhi ya mapendekezo hayo ni kuangalia kuwapo kwa tume huru inayosimamia uchaguzi huo, aidha kuzitazama upya asilimia za ushindi kuwa mshindi apate zaidi ya asilimia 50 ya kura zote zilizopigwa, lakini pia kuruhusu matokeo ya urais kupinga mahakamani na kuwapa nafasi wagombea huru.

NI MWANZO MZURI

Wakiendelea kutoa maoni yao, baadhi ya wachambuzi wanaeleza kile wanachokitarajia na kwamba ni mwanzo mzuri.

Mchambuzi wa siasa Maggid Mjengwa, anasema, kuwapo kwa mapendekezo ya wadau na pia maoni ya Rais kuruhusu mjadala wa mabadiliko kwenye sheria za uchaguzi ni mwanzo mzuri kwa kuwa inaonyesha ni jinsi gani Rais alivyo tayari kufanya mabadiliko kwa manufaa ya Watanzania wote bila kujali maslahi ya vyama.

"Kwa mfano mapendekezo ya wadau kwamba NEC iwe na watumishi kwenye ngazi ya halmashauri ni muhimu, kutokana na kwamba kumekuwapo na sintofahamu kila unapofanyika uchaguzi," anasema Mjengwa.

Wakurugenzi wa halmashauri wanalaumiwa kwa kuwaengua baadhi ya wagombea kwenye uchaguzi hata kwa jambo dogo ambalo wangetumia busara kulimaliza.

"Rais ametolea mfano masuala ya kiufundi, kama kukosea kuandika jina la mgombea au chama na kwamba yasitumike kumnyima haki ya kushiriki uchaguzi," anasema.

Anasema iwapo mapendekezo hayo yatafanyiwa kazi, imani ya wananchi kwa tume itaongezeka na kupunguza hofu inayotokana na yale ambayo yamekuwa wakidaiwa kufanywa na baadhi ya wakurugenzi wa halmashauri.

"Hata Tume ya Jaji Warioba kwenye rasimu ya katiba, iligusia suala la NEC kuwa na watumishi ngazi ya chini ili kuondoa kasoro zinazojitokeza kila unapofanyika uchaguzi na nyingine kuhusishwa na  hofu ya wasimamizi wakiwaogopa waliowateua," anasema.

AIBU ZITAPUNGUA

Mwenyekiti wa Taasisi Utawala Bora na Maendeleo Tanzania (CEGODETA), Thomas Ngawaiya, anasema, aibu za mara kwa mara kwenye uchaguzi zinaweza kupungua iwapo kuna usimamizi imara.

"Kumekuwapo na mambo ya aibu kwenye uchaguzi ambayo husababishwa na baadhi ya wasimamizi kama kuwanyima mawakala nakala za viapo vya kusimamia uchaguzi au kuwaengua wagombea kwa sababu zinazolalamikiwa na kuonekana hazina mashiko," anasema Ngawaiya.

Anasema, wao kama watu wa utawala bora, wanaamini kwamba, tume huru yenye watumishi ngazi zote itapunguza kasoro zisizo za lazima ambazo baadhi husababishwa na wasimamizi watumishi wa serikali.

KUONDOKA MAKADA

Ngawaiya anasema, chanzo kikubwa cha kasoro kinatokana na kwamba baadhi ya wasimamizi ni makada wa chama, hivyo inawawia vigumu kuruhusu wagombea wa upinzani kushinda.

"Niseme tu kwamba, figisu kama kukosea kuandika majina yao au vyama vyao, ni aibu na udhaifu wa kutaka ushindi wa mezani badala ya kupambana majukwaani, " anasema.

Mwenyekiti huyo anasema, si vyema kuwanyuma wapigakura mgombea wanayemtaka kwa lengo la kufurahisha ngazi ya uteuzi, kwa kuwa husababisha kupata viongozi ambao si chaguo lao.