Maprofesa Mbilinyi, Ngowi walipotathmini maudhui ya bajeti inayowafaa

12Apr 2019
Theodatus Muchunguzi
Dar es Salaam
Nipashe
Maprofesa Mbilinyi, Ngowi walipotathmini maudhui ya bajeti inayowafaa
  • Watetezi jinsia walia walichokubaliana hakijatekelezwa

WAKATI bajeti ya Taifa ya mwaka 2019/20 inatarajiwa kuwasilishwa bungeni Juni 16, makundi kadhaa katika jamii hususan ya watetezi wa usawa wa kijinsia, yameanza kuichambua na kuifanyia tathmini, kuona kama itakuwa yenye kukidhi mahitaji ya makundi yote hususan ya wanyonge.

Prof. Marjorie Mbilinyi.

Tunapozungumzia wanyonge inamaanisha kuwa ni makundi ya pembezoni, wenye mahitaji maalum kama wanawake, watoto, wenye ulemavu na watu wanaoishi maeneo ya pembezoni; kwa lugha nyingine maskini.

Kutokana na hali hii, ni mategemeo ya wengi kwamba ili kuondoa changamoto zinazowagusa wanyonge wengi, bajeti hiyo ya Sh. trilioni 33.1 hainabudi kuandaliwa kwa kulenga kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo.

Tunategemea bajeti itakayoandaliwa, kuwasilishwa bungeni na kujadaliwa itasimamia haki za binadamu kwa kuwajali wanawake na kupunguza kama si kuondoa vifo vya wajawazito na watoto wachanga. Ni bajeti itakayowagusa watu wanaoishi na ulemavu, mabinti, watoto wachanga na wazee. Tunategemea itatoa fedha na ruzuku zitakazojibu changamoto hizo. Aidha, itajenga mabweni ili mabinti wawe na haki ya kusoma na kulindwa dhidi ya wabakaji.

Mdahalo wa TGNP

Wiki iliyopita nilihudhuria jumuiko jijini Dar es Salaam ambalo jopo na wasomi na watatezi wa usawa wa kijinsia walichambua na kufanya tathmini kuhusu bajeti jumuishi, ambayo inazingatia usawa wa kijinsia.

Katika mdahalo huo ulioandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), ziliainishwa changamoto mbalimbali zinazoendelea kuwa vikwazo kwa makundi ya wanyonge, jambo linalodhihirisha kuwa bado bajeti ya Taifa inayoandaliwa kila mwaka haijawa jumuisho; kwa maana ya kutokidhi mahitaji ya wanyonge.

Kwa mtazamo wake, Prof. Marjorie Mbilinyi, mambo yote muhimu yaliyobainishwa katika mpango wa maendeleo endelevu yanapaswa kuingizwa katika bajeti yenye mlengo wa kijinsia kwa lengo la kubomoa mfumo dume na kuleta udawa wa kijinsia.

Prof. Mbilinyi anaona kuwa inahitajika bajeti ambayo itakomboa nguvu kazi ya wanawake na wasichana, akisema wasichana wadogo wamegeuka kuwa wafanyakazi wa ndani wa kutunza watoto bila kuwa na elimu, uzoefu. Hivyo, anaeleza kuwa njia ya kuwakomboa wasichana na wanawake ni kuwapa elimu.

“Tutatumiaje rasilimali zetu kujenga mabweni kwa ajili ya wasichana, ili wasikatishwe masomo kwa kubakwa na baadaye kunyimwa fursa ya kuendelea na masomo,” anasema na kuongeza:

“Tubomoe child labour (kazi za utotoni), ndoa za utotoni na kuweka mfumo rasmi wa uchumi ili kila mtu abaki na heshima ya kuutunza mwili wake.”

Swamwely Mkatwa, mchambuzi wa sera kutoka asasi ya Actionaid, anasema kodi ndicho chanzo kikuu cha mapato, hivyo fedha zitokanazo na kodi hizo zipelekwe kutoa huduma kwa mujibu wa mlengo wa kijinsia na kodi hiyo ugawiwe sawa.

Mkatwa anaona kwamba ili kuhakikisha kuwa kodi ya wananchi inanufaisha watu wote na kwamba serikali iwajibishwe kwa sababu kodi ni ya wananchi, hivyo iangalie mlengo wa kijinsia.

Kwa upande wake Prof. Honest Ngowi, anaiona bajeti shirikishi kuwa ni inayoangalia katika matumizi kama makundi yote yanalengwa; kwa maana kila mmoja anapata anachotarajia kupata.

“Tunapaswa kuangalia mapato kwanza kwa mfano, kama watu wote wanaostahili kulipa kodi wanalipa, bila hivyo tukikopa tutarajue mzigo wa madeni (deni la taifa) litakua, huduma zitakosekana,” anaeleza na kuhoji:

“Je, sera zetu za bajeti tunazifanya kuwa shirikishi. Je, tunashirikisha katika kiongeza keki ya taifa na katika kuigawana?”

Lilian Liundi, Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, anabainisha kwamba ulifanyika utafiti ambao ulibainisha ngawo wa rasilimali haukidhi mlengo wa kijinsia, hivyo ukafanyika uhamasishaji kwa kushirikiana na serikali na wafadhili kuhusiana na bajeti yenye mlengo wa kijinsia mwaka 2008, ambao sera, mipango na programu zilizingatiwa serikalini.

Kwa mujibu wa Liundi, ni masikitiko kwamba baadaye serikali ilionekana kutochukua hatua kosonga mbele kwa mfano, akitoa mfano ilipofika mwaka 2010, mambo ya jinsia yalibakia kwenye wizara moja (Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto), badala ya kuwa ndani ya wizara nyingi kwa ni suala mtambuka.

Anasema, ni hali iliyosababisha baadhi ya nchi jirani za Rwanda na Uganda zilizokuja kujifunza nchini, kwenda kwa kasi na kuiacha nyuma Tanzania katika suala la bajeti, yenye mlengo wa kijinsia.

Anaongeza kuwa mwaka 2015-2016 yalionekana mageuzi kutokana na serikali kuongeza masuala ya jinsia katika bajeti, ingawa utekelezaji wake haujawa wa kuridhisha.

Licha ya Wizara ya Fedha na Mipango kuandaa kitini cha bajeti ya kijinsia (gender bajeti manual), lakini Liundi anasema kilibaki katika karatasi.

Licha ya changamoto hiyo, bado Liundi anaeleza matumaini ya kupatikana bajeti yenye mlengo wa jinsia. Anasema, kwa sasa kuna hali chanya kutokana na Tamisemi (Ofisi ya Waziri MKuu Tawala za Mikoa Serikali ya Mitaa), kwa kuungana mkono na TGNP na Shirika la Chakula Duniani (WFP), ambalo liko chini ya Umoja Mataifa.

Anafafanua kiwapo msukumo mkubwa, ikiwamo kuandaliwa kwa kitini cha bajeti ya kijinsia, ili kuanza kutumika katika ngazi ya wilaya.

Mwelekeo wa bajeti

Kuhusu mwelekeo wa bajeti ijayo ya mwaka 2019/20, Prof. Ngowi anatathmini kwamba haitakuwa tofauti na zile za miaka miwili iliyopita, ambazo zilijiekeleza katika miundombinu na miradi mikubwa.

Anasema, kwa kiasi kikubwa itakuwa ya uchaguzi, kwa kuwa mwaka huu, kuna uchaguzi wa serikali za mitaa na mwakani ni uchaguzi mkuu. Anaeleza mtazamo wake:

“Ni fursa, ni wakati wa kudai zaidi. Wakati wa uchaguzi wanasiasa hujipendekeza kwa wananchi, hivyo kuwapo kodi ndogo, chache kwa lengo la kuwafurahisha wananchi.”

Kwa upande mwingine, Prof. Ngowi na Mkwata wana mawazo yanayofanana, kwamba ili kuwapo bajeti ya kutosha inayoweza kukidhi mahitaji ya wengi wakiwamo wanyonge, kuna haja kwa serikali kupanua wigo wa makusanyo ya mapato kwa kuacha kodi za mazoea kama vinywaji na sigara, badala yake ijielekeze katika kampuni kubwa, sambamba na kufuta misamaha ya kodi ambayo ni mzigo kwa wananchi.

Jicho la Tamisemi

Dennis Londo, kutoka Tamisemi, anaeleza kuwa serikali ina dhamira ya dhati kuhakikisha rasilimali zinaelekezwa katika utoaji huduma kwa watu wote.

Anafafanua kuwa, kwa sasa serikali inachukua hatua kadhaa kuzirekebisha athari zilizosababishwa na masharti ya nchi wafadhili, hususan ya kuwataka wananchi kuchangia huduma za jamii ambazo zilikuwa zikitolewa bure na serikali.

Londo anatoa mfano wa elimu bila ya malipo kwa shule za msingi na sekondari, imepunguza athari ya watoto wa kike waliokuwa wakishindwa kwenda shule, badala yake waliajiriwa kufanya kazi za ndani, majumbani.

Anasema kutokana na hatua hiyo katika sura chanya kwa waathiriwa, kwamba hivi sasa kuna malalamiko kuwa wasichana wa kufanya kazi za ndani wameadimika, hali inayotoa ujumbe kwamba wengi wako bado wako shuleni.

Kadhalika, anataja kushuka kodi za viwanja na majengo kutaiwezesha serikali kupata kidogo, lakini pia wananchi wananufaika kwa kutoa kiasi kidogo cha fedha.

Mengi yalizungumzwa katika mdahalo huo, lakini jambo la msingi ni kufanyika ufuatiliaji ili kuhakikisha yanapewa kipaumbele katika mipango na utekelezaji wa bajeti.

Kuna baadhi ya halmashauri zimeanza angalao kutenga bajeti kwa ajili ya taulo za kike kwa ajili ya wanafunzi. Pia hatua ya serikali ya kufuta kodi kwa taulo za kike katika bajeti ya mwaka huu (2018/2019).

Kwa mwaka ujao wa fedha 2019/2020 bila shaka serikali itakuwa imeyazingatia mahitaji ya msingi ya makundi ya wanyonge kama uwezeshaji (mikopo), miundombinu (mabweni), kuongeza bajeti ya kilimo ambacho ni tegemeo kubwa kwa wanawake pamoja na barabara katika maeneo ya kuingia kwenye masoko.

Habari Kubwa