Marekani, China walipotia saini kuweka sawa mauzo biashara zao

17Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Marekani, China walipotia saini kuweka sawa mauzo biashara zao

MATAIFA ya Marekani na China yametia saini makubaliano yanayolenga kumaliza vita vya kibiashara, ambavyo vinaelezwa kuathiri masoko na uchumi wa dunia.

Marais, Donald Trump wa Marekani na Xi Jinping wa China. PICHA ZOTE: MTANDAO.

China na Marekani zimekuwa katika vita ya kibiashara tangu Rais Donald Trump aingie madarakani na kuanzisha sera ya ‘Marekani Kwanza’ inayolenga kulinda bidhaa za nchi hiyo.

Rais Trump akizungumzia makubaliano mjini Washington, anasema makubaliano hayo ni mapinduzi makubwa kwa uchumi wa nchi yake ya Marekani, huku viongozi wa China wametaja makubaliano hiyo kama ushindi kwa pande zote na utasaidia kuimarisha uhusiano wa pande mbili.

China imeahidi kuongeza bidhaa zinazouzwa Marekani zenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 200 ikiwa ni ongezeko la kiwango ilichoweka mwaka 2017, kisha kuimarisha sheria za haki miliki.

Aidha, Marekani imekubali kupunguza kwa asilimia 50 ya kodi mpya dhidi ya bidhaa za China zinazoingizwa Marekani.

YALIVYO MAKUBALIANO

Katika mazungumzo hayo, mafahari hao wa uchumi wa dunia, wamekubaliana kuimarisha ununuzi wa bidhaa za kilimo kwa thamani ya Dola za Marekani bilioni 32, uzalishaji kwa Dola bilioni 78, nishati Dola bilioni 52 na huduma nyinginezo bilioni 38.

Pia, China imekubali kuchukua hatua zaidi dhidi ya bidhaa ghushi na kufanya iwe rahisi kwa kampuni kuchukua hatua za kisheria dhidi ya uchukuaji taarifa muhimu za kibiashara.

Marekani imekubali kuacha asilimia 25 ya kodi kwa bidhaa zinazoingizwa kutoka China zenye thamani ya bilioni 360, ikiwa imeweka kodi mpya kwa bidhaa za Marekani zenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 100 na inatarajiwa kuendelezwa kiwango hicho cha kodi.

YANAAKISI DUNIA?

Makamu Rais wa China Liu He, alitia saini makubaliano kwa niaba ya China, anasema makubaliano hayo yalibebwa na kuwapo usawa na kuheshimiana kwa pande zote mbili hizo za dunia.

Pia katika hutoba yake alitamka kuleta mfumo wa kiuchumi wa nchi yake, kwamba hautakuwa na madhara katika uchumi wa dunia wa sasa.

"China ina mfumo wa kisiasa na wa kiuchumi ambao unaendana na maslahi ya taifa," anasema.

"Hii haimaanishi kwamba China na Marekani haziwezi kushirikiana. Badala yake, nchi hizi mbili zinashirikishana maslahi mengi ya kibiashara," anasisitiza.

Makamu huyo wa Rais, anaongeza:"Ni matumaini yetu kwamba pande zote mbili zitashirikiana na kutimiza waliokubaliana na kudumisha makubaliano kwa dhati."

Ni aina ya makubaliano yaliyopigiwa makofi kimataifa, kwamba mwanzo wa kumalizika vita baridi vya kibiashara duniani.

Rais Trump anasema, ni mazingira yanayotokea katika hali ya kulinda kazi za kampuni za Wamarekani, kutokana na kile anachokitathmini kama “ushindani usiyo wa haki wa kibiashara.”

Hali hiyo isiyo ya kawaida, Rais kutia saini mkataba wa pande mbili kunachagiza umuhimu wa mkataba huo kuonekana ushindi kwa Marekani, huku kiwango cha kodi kikifanyiwa marekebisho na maridhiano madogo ya kibiashara yakifikiwa.

Aidha, malalamiko ya Marekani kuhusu kinachoitwa “tabia ya China kuanzisha mtazamo wake, utoaji ruzuku za kibiashara hadi wizi wa kimtandao” bado haijashuhidiwa katika mwafaka huo.

Pia kumekuwapo dai la Rais Trump, ambaye nchini mwake nazi ‘hazijapoa’ kwake, kutaka kuandikwa tena sheria za kibiashara duniani hazijafanikiwa.

AFRIKA KULIKONI?

Marekani imekuwa ikipoteza ushawishi barani Afrika, lakini kuna dalili nchi hiyo inataka kubadili hali hiyo, iendelee kulikamata bara hilo.

Mjumbe wa Masuala ya Afrika wa Marekani, Tibor Nagy anatamka: ''Ikamate kwa muda mrefu, wakati wawekezaji walipokuwa wakibisha milango na Waafrika wakimfungulia mtu pekee aliyekuwapo, Mchina.

Marekani imekuwa chanzo kikubwa cha uwekezaji wa moja kwa moja barani Afrika, lakini mchango wake umekuwa ukipungua.

Inaelezwa, ushindani kutoka nchi nyingine umeongezeka katika kipindi cha muongo mmoja uliopita bna katika utawala wake, Rais Trump anaelezwa kuinyima amani Afrika kisiasa kwamba ‘sehemu ambayo marafiki zake wanakwenda kujaribu kutajirika.’

China nayo mwaka 2018, ilitangaza uwekezaji wa thamani ya Dola za Kimarekani bilioni 60 kwa ajili ya miradi ya miundombinu Afrika.

Lina Benabdallah, mtaalamu wa uhusiano ya China na Afrika katika Chuo cha Wake Forest, Marekani, anasema biashara kati ya Marekani na mataifa ya Afrika imeshuka kwa sababu ya ongezeko la uhitaji wa China, Russia na Uturuki.

Kampuni za China, zimechangia maendeleo makubwa katika ujenzi wa miundombinu mipya na iliyosahaulika kwa muda mrefu katika baadhi ya mataifa ya Afrika.

Mtaalamu huyo anasema, Marekani imekuwa ikiishtumu China kwamba inahimiza mataifa ya Afrika kujitegemea na ilitumia mikataba ya kifisadi na kuhatarisha rasilmali asili za mataifa hayo.

Pia, anadai imewahi kuutaja uwekezaji wa China kwa Afrika kama wenye uwezo wa kuimarisha miundombinu Afrika, lakini unaongeza madeni na nafasi kidogo za ajira.

Kwa ujumla kibiashaara, inaelezwa Marekani ina wakati mgumu kujihusisha na uchumi wa nchi hizo unaochipukia na wakati huohuo kukabiliana na kasi ya ukuaji uchumi wa China.

.Kwa msaada wa taarifa za kimataifa

Habari Kubwa