Martha Mganga....

26Jan 2021
Gaudensia Mngumi
Dar es Salaam
Nipashe
Martha Mganga....
  • ‘Aliyeonja mauti’ na sasa anawaokoa wenye ualbino

BAADA ya kuzaliwa na ualbino na kuonekana kama mtu asiyekubalika ndani ya jamii Sista Martha Mganga, anaweka nadhiri ya kuwasaidia watu wanaozaliwa na hali ya ualbino, akifuatilia maisha yao kuanzia wanapozaliwa, kuwapa faraja walioteswa, kuwasaidia kupata elimu, huduma za afya na kulinda ustawi wao

Mama Martha (kushoto) na baadhi ya watoto anaowalea nyumbani kwake Njiro, wakianza safari ya kuelekea shuleni mapema mwezi huu, wakiwa na mafuta ya kuwakinga na mionzi ya jua, madaftari na vifaa vya shule tayari kwa masomo. PICHA: PEACE MAKER FOR ALBINISM

Anapozungumza na Nipashe hivi karibuni, Sista Martha Mganga, aliyeanzisha Taasisi ya Peace Maker for Albinism and Community, anafanya shughuli zake mkoani Arusha, anasema anawalea na kuwasaidia wenye ualbino baada ya kuweka ahadi kwa Mungu, anayesema alimnusuru na mauti na mateso mengi, akiamini alifanya hivyo ili amtumie kuwasaidia watakaozaliwa na hali hiyo.

Akikumbusha baadhi ya changamoto alizopita, anasema alizaliwa mapema miaka ya 1960 mkoani Arusha na wazazi wakata mkonge. Baba na mama walikuwa na rangi nyeusi, lakini walipata watoto watatu wenye ualbino na huo ukawa mwanzo wa maisha magumu ya huzuni na uchungu kwake na ndugu zake pamoja na wazazi, lakini mama aliyenyanyasika na kuteseka zaidi.

Anasema; “Mama ndiye aliyeelemewa na mzigo akihukumiwa kuwa na hatia kwa sababu yeye na mumewe hawana ualbino inakuwaje amepata watoto wanaoishi na ualbino? Anahukumiwa kuwa pengine siyo mwaminifu kwenye ndoa yake, anabebeshwa lawama na familia, ndugu na jamii inayomzunguka.”

Martha anasema alipokuwa na kujitambua alifahamu fika kuwa hakubaliki kwenye familia. Akienda shuleni wanafunzi wanamwogopa, mitaani inazingirwa na watu wenye imani potofu wanaosema kuwa yeye si binadamu wa kawaida ni mtu anayepotea kimaajabu.

Darasani anakutana na walimu wanaomfuka asikae mbele kwa fikra potofu, wasiotaka mwenye ualbino awakaribie. Hivyo, anasema licha ya kuwa na uoni hafifu anafukuzwa akae nyuma, anaadhibiwa, kufokewa na kudhalilishwa akiitwa mjinga.

“Yote hayo niliyaweka moyoni. Nikaangalia adha na manyanyaso anayopata mama yangu kwa ajili yetu. Anafukuzwa na baba, lakini bado anaendelea kutubeba na kututunza niliona hakuna sababu ya kuendelea kuishi. Nilipanga kumaliza maisha yangu na kuwaacha kwa amani hasa mama anayebeba lawama zote.” Anasema mwanaharakati huyo.

Mwanaharakati huyo alizaliwa na wazazi kutoka Dodoma waliohamia katika Kijiji cha Doli karibu na Usa Riva mkoani Arusha, lakini akakulia Kijiji cha Makiba kwenye kilimo cha mkonge ambako wazazi wake walikuwa wakifanyakazi kwenye mashamba ya zao hilo anasimulia jaribio la kujiua.

KUJIMALIZA

Anasema akiwa na miaka 21, alikata tamaa baada ya kuona maisha hayana maana. Aliamua kujimaliza kwa kujitupa mtoni usiku wa manane, wakati wa mafuriko ili apotee iwe kuliwa na mamba, kufukiwa mchangani au lolote ili kuachana na maudhi na maisha yaliyojaa kukejeliwa, kuchukiwa na kunyanyapaliwa.

“Nilitoroka nyumbani kijijini kwetu Makiba saa 12 jioni nilitembea usiku wote nikijua kuwa kama nitaondoka mchana wataniona na kunirudisha. Nilijitosa usiku nikaelekea ulipo Mto Nduruma.

Niliufikia baada ya kutembea muda mrefu porini nikiwa mwenyewe. Usiku wa manane nilifika mtoni. Nilisikia sauti ya maji ikivuma kwa nguvu ulikuwa umejaa na kufurika nilijitupa mtoni ili uwe mwisho wangu. Lakini haikuwezekana Mungu aliniokoa. Maji yalinipokea na kunirusha juu ardhi upande wa pili sehemu kavu nikiwa salama.

Nilisikia sauti ikiniambia usiogope bado ninakupenda. Nilikuwa salama na asubuhi watu walinikuta na kuniondoa. Huo ukawa mwanzo mpya wa maisha yangu.” Anasema Martha.

Aliingia mtoni kwa kukata tamaa kwa sababu hakukubalika popote kijijini, shuleni anakimbiwa na kuogopwa, lakini anapigwa na walimu na mama yake anateseka kwa vile hawezi kumuacha.

PAMBAZUKO JIPYA

Baada ya kunusurika aliahidi kuwasaidia wenye ualbino na kuanzia mwaka 1986 akiwa na miaka 23 alianza kazi ya kuwasaidia watoto na jamii ya wenye ualbino: “Nilimwambia Mungu umenikoa, umenilinda, kama utanitunza nisife katika umri mdogo, ukanipa nguvu na uwezo nitawatunza wanaoishi na ualbino. Nitawafariji, nitawahudumia na kuwasaidia kuvuka kwenye changamoto wanazopitia ambazo najua haziwezi kukosekana.”

Anasema akiwa Arusha alianzisha huduma ya kuwasaidia wenye ualbino, wakiwamo wagonjwa, kuwatafuta na kuishi nao kwenye chumba chake, kuwalisha chakula, kuwatibu, kuwasaka na kuwahifadhi watoto waliotelekezwa na kuwasaidia kupata shule za kusoma iwe bweni au popote juhudi zilifanywa kwa kuomba uhisani si kwa kulipia.

“Niliwatia moyo, nikawasaidia kuelewa kuwa wapo kwa kusudi la Mungu, si kwa mapenzi mtu wala jamii,” anasema na kuongeza kuwa alikuwa hana kipato, lakini alikuwa mtumishi wa Kanisa la Anglikani akifanyakazi kanisani.

Kuanzia mwaka 2015 amekuwa akiwahudumia wenye ualbino takribani 160 zaidi ni wanafunzi wanaotoka mikoa mbalimbali wanaopatiwa matibabu, kusomeshwa, kupewa vifaa vya shule na makazi na asasi ya Peace Maker for Albinisim and Community, inawahifadhi wenye ualbino 35 kwenye makazi yao mkoani Arusha wakiishi pamoja na Martha eneo la Njiro.

UJUMBE WA MALEZI

Martha anatoa ujumbe kwa wote, akirejea maisha yake asema unapomlea mtoto mwenye ualbino daima mtie moyo. Usimdhalilishe wala kumnyanyapaa. Si vyema kumwambia huwezi kufanya jambo fulani, una kasoro hii au ile kutokana na ngozi yake.

Anasema wazazi, walezi na jamii isifanye hivyo kwa kuwa mwenye ualbino ni binadamu wa kawaida.

Anatoa mfano wanafunzi wakiwa shuleni wanapojifunza mathalani mapishi, wapo walimu wanawaambia wenye ualbino wasipike kwa sababu ya joto kali wanaweza kuunga na ni hatari kwa ngozi yao.

“Haipendezi. Mwambie ajifunze mtie moyo, kama ni kuoka mikate mpe jiko mbadala asifanyekazi kwenye tanuru na joto kali. Akae sehemu yenye hewa. Tafuta maarifa ya kumwelimisha, kumpa ujuzi na stadi za maisha si kumkataza kwa kigezo cha ngozi yake.”

Anataja mfano mwingine wa kushona, wapo walimu kwenye vyuo vya mafunzo wanawakataa wenye ualbino kwa kigezo kuwa wana uoni hafifu na hawawezi, anasema ni kuwakosea.: “Mpe vifaa saidizi kama miwani na vikuza herufi na maumbo ili aone, siyo kumnyanyapaa. La msingi ni kumtia moyo.

Anashauri kuepuka ubaguzi na unyanyapaa wowote iwe nyumbani au shuleni wa kuonyesha kuwa mwenye ulemavu akiwa anayeishi na ualbino wana upungufu. Anasema watoto waelimishwe kuwa wote wako sawa tofauti ni ngozi pekee, kuwa yao inakosa rangi ya asili.

KUFAHAMISHWA ATHARI

Martha anasema wenye ualbino wanahitaji kutumia dawa au mafuta maalumu ya kulinda ngozi na athari za jua kali, ni vyema kuwaeleza watoto umuhimu wa mafuta hayo na athari za kuyaacha wakati wa malezi. Kuhusu mavazi ni vyema kuwaambia kuhusu kuvaa mavazi ya kufunika mwili, kofia na miwani kulinda macho na uso. Yote yafanywe pamoja na kubainisha athari za kuyapuuza.

MILA POTOFU

“Wenye ualbino wanaathiriwa na mila potofu. Utasikia hawafi wanatoweka au kupotea kimaajabu. Wengine wanaamini wakijamiaana nao magonjwa yao yataondoka na kuna wanaowinda viungo vyao kwa imani ya kupata utajiri na kuwaeleza kuhusu madai ya kuwadhuru ili kupata viungo vyao. Ni vyema kuwaeleza usiwafiche.”

Mlezi huyu wa wanaoishi na ualbino anasema katika malezi ni vyema kuwaeleza watoto kwa hatua kuwa wanahitaji vifaa saidizi ili kumudu maisha. Mfano miwani kusoma, kukaa mbele karibu na ubao, kutumia vikuza herufi na maumbo wakati wa kusoma na pia miavuli wanapotembea kwenye jua kali.

JUHUDI KITAIFA

Martha anasema yaliyompata maishani hasa utotoni yamemwamsha kufanya juhudi za kipekee kusaidia wenye ualbino kwa mfano kufundisha wakunga, wauguzi na madaktari katika mikoa mingi mijini na vijijini kufahamu chanzo cha ualbino na namna ya kuwafariji wazazi wanaojifungua watoto wenye ualbino.

ITAENDELEA…

Habari Kubwa