Marufuku soko la pembe China kuokoa asilimia 70 ndovu Afrika

05Jan 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Marufuku soko la pembe China kuokoa asilimia 70 ndovu Afrika

CHINA imetangaza marufuku biashara ya pembe za ndovu nchini humo, utekelezaji unaotorajiwa kuanza miezi mitatu ijayo. Ni taarifa nzito kwa kila pande husika duniani, iwe kwa mtazamo hasi au chanya.

Kimsingi, ni taarifa inayotangaza kufunguka mpango wenye tija katika harakati za kuwalinda tembo Afrika, ambao hivi sasa wanaelezwa wako hatarini kutoweka.

Kuchukuliwa hatua hiyo ni pigo kubwa kwa majangili wa Afrika na hata kuwagusa wengine katika biashara hiyo.

Uzito wa taarifa hiyo unaendana na uhalisia kwamba, China ndiye mnunuzi wa zaidi ya theluthi mbili ya meno ya tembo duniani.

Pia, ni matumaini yenye sura pana katika kuachana na kilio cha utekelezaji marufuku yenye miaka 41 sasa. Tamko lingine kama hilo lilitolewa mwaka 1947.

Watakwimu mbalimbali watetezi wa mazingira nao wana vilio vyao, kama vile wanaodai kila baada ya saa moja wanauawa tembo si chini ya wanne.

Katika mtazamo huohuo, wapo wenye takwimu zinazoonyesha hadi sasa zaidi ya nusu ya tembo duniani wameuawa na wengine wakitaja si chini ya 100,000 kutoka barani Afrika.

Kwenye eneo hilo, kuna malalamiko kwamba utakuwa mtihani mkubwa kurejesha idadi ya tembo waliokuwepo, huku hofu ikihamia upande wa pili kuhusu kutoweka viumbe hao.

Wakati sokoni pembe zinauzwa kwa bei ya Sh. milioni 2.4 kwa kilo zikipewa majina mbalimbali ya kufananishwa na madini, bidhaa hiyo inanadiwa katika masoko zaidi ya 140.

HATUA YA CHINA
Serikali ya China imesema biashara ya nyara hizo na usindikaji wake, isipokuwa minada ya pembe za ndovu zilizopatikana kutoka vyanzo halali, itapigwa marufuku kufikia mwishoni mwa mwezi Machi, mwaka huu.

Hatua hiyo inadaiwa kuwa, ni utekelezaji unaoridhia msukumo wa miaka mingi kutoka kila pande za dunia, hasa kutoka kwa watetezi wa ulinzi wa wanyamapori, juu ya kuwapo tishio la kuwamaliza tembo wa Afrika.

Wanamazingira wanasema, hatua hiyo ya kupiga marufuku biashara ya nyara hizo kwenye soko la China linalokadiriwa kununua asilimia 70 ya pembe zote zinazouzwa duniani, inatoa shinikizo kwa nchi jirani ya Hong Kong na taifa la Uingereza, ichukue hatua ya kuziba mianya inayochochea biashara hiyo.

“Hii ni habari njema ya kulihitimisha kabisa soko hili kubwa la pembe za ndovu duniani,” anasema Mkurugenzi wa Shirika la Uhifadhi wa Wanyamapori barani Asia, Aili King na anaongeza:

“Hatua hii ni ya manufaa kwa tembo wa Afrika. Tunatoa wito kwa nchi nyingine zilizohalalisha soko la pembe za ndovu ndani ya mataifa yao, mfano wa China kwa kuyafunga masoko ya biashara za nyara hiyo.”

Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Uhifadhi Wanyamapori na Mazingira (WWF) wa China, Lo Sze Ping anasema: “Kwa kulifunga hili soko kubwa la nyara hizi, kutawazuia raia walioko nchini na nje ya nchi yetu kujihusisha na ununuzi wa pembe za ndovu na hivyo kuwa vigumu kwa walanguzi kuuza hifadhi zao walizozificha.”

Baraza la Dola la China, limesema pembe za ndovu kutoka Afrika, huuzwa kwa bei ya Dola za Marekani 1,100 kwa kilo moja, ambayo ni sawa na Sh. milioni 2.4 za Kitanzania na sasa haitafanyika kila baada ya Machi 31, mwaka huu.

“Ili kuwalinda vyema tembo na kushughulikia kwa ukamilifu biashara haramu ya nyara hizo, China itasimamisha taratibu usindikaji na uuzaji wa pembe za ndovu kibiashara,” ilisema taarifa ya baraza hilo.

Nalo Shirika la Habari la China (Xinhua) linasema marufuku hiyo itaathiri kampuni 34 za usindikaji na majukwaa 143 yanayojishughulisha na biashara hiyo.

Kupigwa marufuku biashara ya pembe za tembo, ni kutekeleza ahadi iliyotolewa na serikali, kupanua wigo wa marufuku ya uingizaji nyara hiyo iliyowekwa mapema kabla ya mwaka 1975.

Hata hivyo, umetolewa msamaha kwa minada ya pembe za ndovu zilizoingizwa nchini humo siku nyingi, ingawaje kuna tahadhari itaendeshwa chini ya kilichotajwa ‘usimamizi mkali.’

Kuna hofu ruhusa hiyo, inaweza kufungua mlango wa mianya kwa biashara hiyo haramu.

Takwimu zinaonyesha kuwepo matukio kati ya 800 hadi 900 za magendo ya nyara hugundulika kila mwaka nchini China.

Mamlaka ya kodi ya China, inasema zaidi ya nusu ya biashara halali za pembe za ndovu, vyanzo vya kupatikana bidhaa zake zinazohusishwa na biashara haramu ya pembe za ndovu.

Inakadiriwa tembo 100,000 waliuawa kutokana na ujangili katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.

Aidha, takwimu zinaonyesha katika kipindi hicho, tembo 111,000 wamepungua hadi kufikia 415, 000. Waliobaki ni sawa na asilimia 373 ya waliokuwepo awali.

Mwaka jana, kampeni hiyo nchini ilikataliwa China, hata pale ilipokuja na hoja kwamba inaweza kuokoa tembo wa Afrika.

SAUTI YA WANAMAZINGIRA
Kaimu Mtendaji Mkuu wa shirika la kujitolea la wanyamapori lililo chini ya WWF ya Uingereza, Glyn Davies, anasema tembo mmoja huuawa kwa ujangili kila baada ya dakika moja.

Davies aliliambia gazeti la The Times, la nchini Uingereza muda mfupi baada ya tangazo hilo kuwa:

“China imeonyesha uongozi mahiri na kwa sasa tunayatupia macho masoko mengine, ili nayo ifunge biashara hii na kuchukua hatua kali dhidi ya biashara hiyo.”

Kupitia ilani yake, Chama cha Wanamazingira wa Uingereza, kiliahidi kuharamisha biashara zote za pembe za ndovu.

Lakini marufuku iliyotolewa na Katibu wa chama hicho, Andrea Leadsom, iliruhusu kuuzwa kwa akiba ya pembe za ndovu zilizokuwapo kabla ya mwaka 1947.

Naye Charlie Mayhew, Mtendaji Mkuu wa Shirika la Kujitolea la Uhifadhi wa Tembo Afrika, anasema: “Hatua iliyochukuliwa na China, inatoa msisitizo kwa Uingereza kuona hoja hiyo na kufuata nyayo.”

Mayhewa ambaye ni mwana wa Mfalme wa Uingereza, anazituhumu serikali nyingi duniani kwamba mara nyingi zinatoa ujumbe unaotofautiana na maagizo yake kuhusu marufuku ya biashara hiyo. Wito wake nchi yake na nyingine nyingi kupiga marufuku biashara hiyo.

MTAALAMU WA IKOLOJIA
Kwa upande wake mtaalamu Profesa Stuart Bearhop, kutoka Kituo cha Ikolojia na Uhifadhi cha Chuo Kikuu cha Exeter, Uingereza aliliambia gazeti la Independet kuwa:

“Nadhani pendekezo hili la China litaleta tofauti na kwa kiasi kikubwa linatia moyo katika suala zima la usalama wa tembo na uhifadhi kwa ujumla.”

Profesa Bearhop anasema kuongezeka kwa ujangili, kumechangiwa na ongezeko la utajiri nchini China na sehemu zingine za Kusini Mashariki mwa Asia.

“Ninadhani pembe za ndovu haziwezi kukosa thamani hata siku moja. Bila shaka kutaendelea kuwapo soko haramu la nyara hiyo ndani ya China,” anasema mwana – Ikolojia huyo.

Profesa Bearhop anatoa mfano kwamba, wakati baadhi ya nchi za Afrika Mashariki ziko mstari wa mbele kupigania kutokomezwa ujangili, biashara haramu ya pembe za ndovu imestawi kwenye mataifa mengine ya Kusini Mashariki ya Bara Asia, ambako kuna marufuku.

“Uwezekano niuonao mimi kwa hatua hii ya China ni kwamba, mahitaji ya pembe za ndovu na kiwango cha ujangili yataporomoka,” anasema.

Hata hivyo, profesa anatahadharisha kuwa, wanyama hawa huzaliana taratibu, japo huishi kwa muda mrefu na kwa hali hiyo, itachukua miaka kuona tena ishara za kuongezeka kwao.

Aidha, kwa mujibu wa makadirio, zaidi ya tembo 10,000 wamefyekwa na majangili barani Afrika katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, kutokana na mahitaji makubwa ya soko la China.

Baadhi ya wawekezaji wa Kichina huita pembe za ndovu kuwa ni ‘dhahabu nyeupe’

Makala haya imetafsiriwa na Raphael Kibiriti, kutoka gazeti la Independent la Uingereza.

Habari Kubwa