Mashabiki wanasubiri matunda ya Uturuki

27Jun 2016
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Mashabiki wanasubiri matunda ya Uturuki
  • ***Kwa mara ya kwanza Yanga watacheza nyumbani dhidi ya TP Mazembe kuwania Kombe la Shirikisho Afrika baada ya zaidi ya wiki mbili kuweka kambi nje ya nchi...

TP Mazembe wako nchini tayari kwa ajili ya mechi yao dhidi ya Yanga kesho kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es salaam.

Ni mchezo wa pili kwa kila timu, lakini ni mara ya kwanza kwa timu hizo kukutana katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga inashuka dimbani ikiwa imepoteza mchezo wake wa kwanza nchini Algeria na Mazembe - mabingwa wa msimu uliopita klabu bingwa Afrika wanashuka dimba la Taifa wakiwa na pointi tatu baada ya kushinda nyumbani mchezo wa kwanza.

Mazembe yenye makao yake makuu katika mji wa kibiashara wa Lubumbashi, inamilikiwa na mfanyabiashara bilionea, Moise Katumbi, ambaye wiki iliyopita alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela na kulipa faini.

TP Mazembe waliwasilina jijini jana usiku katika msafara wa watu 32 tayari kuivaa Yanga.

Timu hizo mbili zitashuka uwanjani kesho kwa ajili ya kuendelea kusaka nafasi ya kusonga mbele katika mashindano hayo yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kwenye kundi lao wakiwa pia na Mouloudia Olympique Bejaia (Mo Bejaia) ya Algeria na Medeama ya Ghana.

Mazembe inatua nchini ikiwa na kumbukumbu ya kupata ushindi wa mabao 3-1 katika mechi yake iliyopita dhidi ya Medeama iliyofanyika Lubumbashi wakati Yanga iliyokuwa ugenini Algeria ilikubali kichapo cha goli 1-0.

Kama ilivyo kwa Yanga, vigogo hao wa Afrika, pia watashuka dimbani kesho wakiwa na kumbukumbu ya kutwaa ubingwa Ligi Kuu DRC baada ya kuishindilia DC Motema Pembe mabao 3-1 wiki iliyopita.

Katika msimamo wa Kundi A, Mazembe inaongoza ikifuatiwa na Mo Bejaia, Yanga na Medeama inaburuza mkia.

MIPANGO YA PLUIJM
Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm aliiambia Spotika kuwa mechi hiyo kwake ni sawa na fainali baada ya kupoteza mchezo wa kwanza ugenini.

"Kwa namna yoyote ile, tunahitaji kushinda Jumanne (kesho), ili tuendelee kuwa kwenye mbio za kuwania ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.

Pluijm alisema licha ya mechi hiyo kutarajia kuwa na upinzani, amewaondoa hofu wachezaji wake kuhusu uwezo wa TP Mazembe, licha ya kuwa na rekodi nzuri kwenye mashindano hayo ya Afrika.

"Ni mechi itakayokuwa na upinzani, lakini kwetu ni muhimu kwa sababu tunahitaji kushinda...ushindi utasaidia kuiweka timu kwenye nafasi nzuri katika kundi letu. Hakuna timu kubwa zaidi ya mwingine, timu zote zilizoingia katika hatua ya makundi ni bora," Pluijm alisema.

Mdachi huyo alisema wachezaji wake wamejiandaa vizuri kuwakabili wapinzani wao na kambi ya Uturuki imesaidia kuimarisha kikosi.

Kuhusiana na mshambuliaji mpya Mzambia Obrey Chirwa, ambaye Yanga wamemsajili kutoka Platnumz ya Zimbabwe, Pluijm alisema haangalii mchezaji mmoja mmoja, kwani anaamini ana kikosi.

"Nimefurahi kupata wachezaji wapya, wataongeza nguvu kwenye timu na hii itatusaidia kupata matokeo mazuri kila mechi tutakayocheza," alisema kocha huyo.

MAZEMBE WANASEMAJE?
Mshambuliaji wa TP Mazembe Mtanzania Thomas Ulimwengu 'Buffalo', amesema kikosi chao kinakuja nchini kwa ajili ya kusaka ushindi.

Ulimwengu alisema kuwa licha ya rekodi nzuri ya mashindano ya kimataifa waliyonayo Mazembe, bado wanauona mchezo dhidi ya Yanga kuwa mgumu kutokana na timu hiyo kupoteza mechi ya kwanza.

Alisema wanakuja Tanzania kupambana na kuhakikisha wanafanya vizuri, wameifuatilia Yanga katika mechi zao kadhaa kuanzia hatua ya awali ya mashindano ya Klabu Bingwa Afrika na Ligi Kuu ya Bara.

"Hakuna mchezaji wa Yanga tunayemhofia, tunakuja kucheza 'kitimu' kwa sababu tunakuja kupambana na timu ya Yanga," Ulimwengu straika huyo wa timu ya Taifa (Taifa Stars) alisema.

REKODI MUHIMU
*Yanga ilianzishwa mwaka 1935 - makao makuu, Dar es Salaam.

*Mazembe ilianzishwa mwaka 1939. Ina uwanja wake wenye uwezo wa kuingiza watazamaji 18,500. Makao makuu yake yako katika mji wa Lubumbashi.

*Kipa mkongwe wa Mazembe, kipa Richard Kidiaba.

*Straika tegemeo wa Yanga Donald Ngoma.

*Mara ya mwisho kwa Yanga kucheza hatua ya makunid michuano ya Afrika ilikuwa mwaka 1998.

*Mwaka 2010, Mazembe iliweka rekodi ya kuwa klabu ya kwanza Afrika kucheza fainali za Klabu Bingwa Dunia.

*Yanga imetwa taji la Ligi Kuu Bara mara 26

*Mazembe imetwaa taji la Afrika mara tano

www.guardian.co.tz/circulation

Habari Kubwa