Matumaini mapya wakulima Chai Kilolo

15Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Matumaini mapya wakulima Chai Kilolo
  • Ni matokeo ya mazungumzo kati ya uongozi wa wilaya na Benki ya Maendeleo ya Kilimo

ILIKUWA kiu ya siku nyingi lakini sasa si kiu tena. Maneno hayo yanasadifu na kutimia njozi za siku nyingi za wananchi wa Kilolo mkoani Iringa juu ya uwapo wa kiwanda cha kuchakata chai wilayani humo.

Kwa miaka mingi, wananchi wa wilaya hiyo hasa tarafa ya Kilolo ambako sehemu kubwa ya ardhi yake inafaa kwa kilimo cha zao hilo, walikuwa na matumaini makubwa ya kujikomboa kiuchumi kupitia chai.

Miaka ya 1980 kilimo hicho kilianzishwa rasmi na iliyokuwa Mamlaka ya Chai Tanzania na wakulima hasa katika kijiji cha Kidabaga na vya jirani, walijitokeza kwa wingi kuanza kuzalisha. Kasi hiyo na shauku ya wananchi ilitokana na kuwapo kwa kiwanda kidogo katika eneo hilo.

Lakini kama msemo wa “furaha ya nyani huishia jangwani” matumaini ya wananchi hao yaliyeyuka baada ya kufungwa kwa kiwanda mwishoni mwa miaka ya 1990. Hatua hiyo ilisababisha mashamba ya chai yaliyokuwa yamestawi kugeuka mapori.

Jitihada mbalimbali zilifanyika ili kufufua kiwanda hicho na kurejesha matumaini ya wakulima yaliyokuwa yamezimika kama mshumaa katika upepo mkali. Juhudi hizo ziliambatana na kutafuta wawekezaji kutoka ndani na nje na mmoja wa wawekezaji ilikuwa kampuni ya Café Direct ya Uingereza.

Mazungumzo yalifanyika kati ya kampuni hiyo na serikali kuanzia mwaka 2006 wakati huo Profesa Peter Msolla akiwa Mbunge wa Kilolo na Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia na baadaye Kilimo na Chakula.

Hata hivyo, jitihada hizo ziligonga mwamba kutokana na mchakato huo kuingiliwa na masuala ya kisiasa, hivyo kubaki wimbo mzuri usioisha masikioni mwa watu na hatimaye matumaini yaliyokuwa yamefufuka yakafifia na hata kuona jambo hilo ni kama maji kupanda mlima.

Matumaini hayo yalifufuka baada ya uongozi wa serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani. Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Asia Abdallah, baada ya kuteuliwa aliliweka suala hilo moja ya vipaumbele vya kuipaisha wilaya hiyo kiuchumi.

“Hakuna kinachoshindikana na hakuna kutaka tamaa, suala la kiwanda cha chai lazima tulivalie njuga kwani jambo hili ni mkombozi kwa wananchi wa Kilolo. Jambo la kwanza ni kuhamasisha wakulima kurejea tena mashambani na lingine ni kutafuta wawekezaji na wafadhili kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda,” alisema mkuu huyo wa wilaya alipohojiwa miezi michache baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo.

UTEKELEZAJI WAANZA

Katika kuhakikisha ndoto hiyo inatimia, uongozi wa wilaya chini ya Abdallah ulianza mchakato wa kutafuta taasisi ambayo ingetoa mkopo wa kuendeleza kilimo cha chai na ujenzi wa kiwanda cha uchakataji wa zao hilo.

Hatimaye Septemba, mwaka jana, uongozi huo ulibisha hodi Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na kufanya mazungumzo kuhusu utekelezaji wa azma hiyo.

Baada ya mazungumzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Japhet Justine, wakati huo akiwa anakaimu nafasi hiyo, alifunguka na kuthiibitisha kufanyika kwa mazungumzo kati ya benki hiyo na uongozi wa wilaya ya Kilolo.

Justine alisema katika mazungumzo na viongozi hao walijadili uwezekano wa kufufua kiwanda cha kuchakata chai ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo lengo kubwa likiwa kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo ili kuwainua wakulima wadogo na wakubwa kutoka wilayani humo.

“Ni muhimu sana kufanya hivyo ili wakulima washirikiane na benki mpaka watakaposimama wenyewe pasipo msaada wowote.

“Kilimo ni uti wa mgongo wa taifa letu. Suala kama hili linawanufaisha wakulima wetu, hivyo ni jukumu letu kuhakikisha wakulima wanapata msaada ambao utawawezesha kujiendeleza katika kilimo na kuinua uchumi wa taifa,” alisema.

Pia alisisitiza kuwa katika maongezi yao, walijadiliana kuhusu uanzishwaji wa kiwanda ili kuhakikisha bidhaa ndogo kama majani ya chai yanatengenezwa nchini kwa ubora wa hali ya juu na kutumiwa ndani na nje ya nchi.

“Kuwapo kwa kiwanda hicho itakuwa moja ya njia za kuunga mkono azma ya serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli ya kujenga uchumi wa kati na wa viwanda ifikapo mwaka 2025 kwa vitendo,” alisema.

Naye Abdalla aliushukuru uongozi wa TADB kwa kupokea wazo hilo litakalowezesha kutimia kwa ndoto hiyo lakini pia kwa jitihada zake za kuisogeza benki hiyo karibu na wakulima.

YAMETIMIA

Matokeo ya mazungumzo hayo yameanza kuzaa matunda baada ya TADB kutangaza zabuni ya ujenzi wa kiwanda cha chai wilayani Kilolo pamoja na maendeleo ya kilimo cha chai kwa ujumla.

Benki hiyo licha ya kutangaza zabuni hiyo, pia imeelezea kufadhili mradi wa uendelezaji wa kilimo cha chai unaofanywa kwa ushirikiano kati ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Chama cha Wakulima wa Chai wa Dabaga (Datega) na Kampuni ya Chai ya Kilolo (KTC).

Kupitia mradi huo, wanachama wa Datega wanamiliki hekta 3,600 ambazo zinafaa kwa kuanzisha mashamba madogo na makubwa ya chai, kiwanda cha kuchakata majani ya chai mashamba ya miti kwa ajili ya nishati ya mkaa.

Sambamba na eneo hilo, kuna ardhi yenye ukubwa wa hekta 10,000 zinazomilikiwa na wakulima wadogo katika vijiji 26. Ardhi hiyo inafaa kwa kuanzisha mashamba na uendelezaji wa kilimo cha chai.

WAJIBU WA TADB

Kupitia mradi huo, TADB inatarajia kutoa msaada wa kifedha kwa ajili ya uendelezaji wa mashamba ya chai katika hekta 3,600 zilizopo, ukarabati na uendelezaji wa hekta 184 zilizopo na uendelezaji wa wakulima wadogo wa chai katika kuibua fursa na kuongeza mashamba ya chai kutoka hekta 170 zilizopandwa chai hadi kufikisha hekta 13, 600.

Katika uendelezaji wa kilimo cha zao hilo, benki hiyo inakusudia uwezeshaji wa uanzishaji na uendelezaji wa kilimo cha mkataba cha chai na mashamba ya miti kwa ajili ya nishati iwapo kutakuwa na uhitaji huo.

Kwa upande wa kiwanda, benki hiyo inatarajia kuwezesha upatikanaji wa zana za kilimo kwa ajili ya kuongeza kasi ya uzalishaji wa majani ya chai katika mashamba yatakayoanzishwa, njia bora na za kisasa za uchumaji wa majani ya chai kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

TADB kupitia mradi huo, inatarajiwa pia kutoa msaada wa kifedha kwa mwekezaji, kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na benki hiyo ili kujenga kiwanda kitakachokuwa na uwezo wa kuchakata kilo 30,000 kwa siku, ujenzi wa vituo vya kukusanya majani ya chai na ununuzi wa magari ya kusafirishia majani kutoka mashambani mpaka kiwandani.

Ujio wa mradi huo ni neema kubwa kwa wananchi wa Kilolo ambao walikuwa na kiu ya kuwapo kwa kiwanda ambacho kingewezesha kufufua kilimo cha chai na kuwakomboa kiuchumi.

Habari Kubwa