Matumizi haya ya Kiswahili yanaangukia katika makosa

19Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Arusha
Nipashe
Matumizi haya ya Kiswahili yanaangukia katika makosa
  • Tujipange matumizi ya neno ‘kama’

SI mara ya kwanza kuwaona au kuwasikia, wataalamu wa Kiswahili, lugha yetu adhimu, wakiendelea kuelekeza matumizi sahihi ya baadhi ya maneno ya Kiswahili au hata sentensi zake katika vyombo vya habari.

Suala hilo ni la kupongezwa sana na linafaa kuendelezwa, pindi nafasi inapopatikana katika vyombo habari, ili lugha hiyo – Kiswahili izidi kuenziwa.

Licha ya juhudi hizo, kuna ambalo limekuwa gumu kuachwa katika matumizi ya wataalamu wa lugha na hata wazungumzaji wa kawaida.
Neno ‘kama’ limekuwa likitumika katika muktadha tofauti. Mara utamsikia mzungumzaji wa lugha, akitamka: “Mimi kama baba; kama mama; mimi kama diwani; mimi kama waziri.”

Tatizo hilo ni kubwa sana katika lugha, ingawa neno ‘kama’ ni pana. Kuna wakati inachukua nafasi ya kifananishi cha dhana ya sawasawa na inatumika kuonyesha msisitizo wa kitu au jambo, mathalan ‘amependeza kama nini,’ kwa maana ya amependeza sana. Pia ‘kama’ hutumika kuonyesha makisio.

Lengo la makala hii ni kujikita katika maana ya neno ‘kama’ katika nafasi ya kifananishi inavyotumiwa na watumiaji na wazungumzaji wa Kiswahili katika muktadha mbalimbali.

Je, ni sahihi kujifananisha wakati wewe ndiye? Kwa mantiki hiyo, ukisema kuwa ‘mimi kama mtangazaji’ inabeba ujumbe wewe sio mtangazaji, ila unajifananisha tu na mtangazaji.

Ukisema ‘ninatangaza mpira kama Mpenja,’ maana yake unajifananisha tu na Mpenja na kamwe huwezi kuwa Mpenja. Watumiaji wengi wa lugha ya Kiswahili, kupitia sanaa zao za lugha, wamekuwa wakiwasilisha ujumbe katika mtazamo wa kujifananisha, wakati wanachomaanisha ndio kwenye uhalisia wa ujumbe.

Kwa matumizi hayo, neno ‘kama’ ni wazi kuwa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), lina kazi na nafasi kubwa ya kuyaelekeza matumizi sahihi ya baadhi ya maneno yanayotumiwa ndivyo sivyo. Hiyo, binafsi naona ndio kazi kubwa iliyoko mezani mwa BAKITA.

Ni lazima matumizi holela ya lugha ya Kiswahili yadhibitiwe ingawa si kwa kiboko, ila kwa kutumia vyombo vya habari kama magazeti, redio, runinga na hata mitandao ya kijami, vikatoa maelekezo ya matumizi sahihi ya baadhi ya maneno.

Kutegemea vipindi vya lugha katika runinga na redio, haitoshi. Magazeti na mitandao ya kijamii, pamoja na redio zitumike kwa lengo la kuelimisha umma juu ya matumizi sahihi ya baadhi ya maneno.

Sioni haja ya kujifananisha na baba, mama, kiongozi, mwalimu, au mwanafunzi wakati ndiye. Itakuwa sahihi kujifananisha hivyo, kama siye mhusika halisi anayebeba wasifu huo.

Kwa mfano mtu akisema: “Mimi kama mwalimu wenu nitawafundisha vizuri,” ni kwamba anaeleweka kuwa yeye sio mwalimu wao, ila anajifananisha na mwalimu mhusika. Tayari inakuwa imeangukia katika upotoshaji.

Kusema “Mimi kama baba nimejitahidi kuyatekeleza majukumu yangu,” maana yake ni kwamba wewe sio baba ila unajifananisha tu na baba aliyepo.

Kwanini ujifananishe wakati wewe ni baba au mama, mwalimu au kiongozi? Mara nyingi lugha inatawaliwa na muktadha, mada ya mazungumzo na hata uhusiano baina ya wanaozungumza.

Kwa maana hiyo, muktadha au mada unaweza kubaini maana ya sentensi. Kwa mfano. inatosha tu kusema kwamba ‘Mimi nitawafundisha vizuri’ na itakuwa imekamilishwa na mazingira anayozungumzia, mada husika na uhusiano kati ya unaozungumza nao.

Kwa mfano, iwapo mtu anajijua kuwa hadhi na cheo chake ni mwalimu, kwa nini atamke tena “Mimi kama mwalimu wenu?” Pia, pasipo shaka unajijua wewe ni baba, kwa nini useme tena mimi kama baba?

Inatosha tu kusema: “Mimi nimeyatekeleza majukumu yangu,” kwa sababu unaozungumza nao wanakujua wewe ni nani au nafasi yako.
Ikumbukwe kuwa, kinachojaribiwa kufafanuliwa au kutolewa ufafanuzi, ni matumizi ya neno ‘kama’ kwa maana ya kifananishi.

Mtui akisema: “Mimi baba yenu nimeyatekeleza majukumu yangu,” bado ni sahihi ili mradi tu neno kama lisiwepo katika sentensi hiyo. Mifano mingine ni: “Mimi diwani wenu nitawachimbia visima vya maji” na siyo “mimi kama diwani….”

Pia, kuna mfano: “Mimi Waziri wa Nishati, nitahakikisha umeme utawashwa katika kila kijiji” na siyo “mimi kama waziri…”

Chonde walumbi wa lugha, ninawaasa turudi kwenye mstari kwa kuzingatia matumizi fasaha ya lugha ya Kiswahili, ili wanaotuiga waondoke na kilichocheemeka kwa ufasaha.

Ni jukumu la kila mwana lugha kuyatambua na kuyarekebisha makosa katika matumizi ya lugha. Kwa kufanya hivyo, kamwe lugha hii muhimu, yenye heshima na kukua kwa kasi, haiwezi kukosa mwelekeo.

Yapo matumizi mengi holela ya lugha ya Kiswahili yanayoibuka kila baada ya muda na hata kuwapo baadhi ya maneno yasiyo sahihi kuibuka kwa kulazimishwa tu kimatumizi.

Chonde tunaambiwa kupitia usemi: “Mjenga nchi ni mwananchi, pia mbomoa nchi ni mwananchi mwenyewe. Katika lugha, mjenga lugha ni mwanalugha na mbomoaji ni mwanalugha mwenyewe.” Tusiyaruhusu haya.

• Mwandishi anapatikana kupitia simu: (+255) 0752631092 na baruapepe: [email protected]

Habari Kubwa