MATUMIZI YA VYANDARUA: Elimu kujikinga Malaria yashika kasi

14Sep 2017
Yasmine Protace
Nipashe
MATUMIZI YA VYANDARUA: Elimu kujikinga Malaria yashika kasi

MALARIA ni ugonjwa hatari unaosambazwa na mbu. Malaria hupatikana sehemu nyingi ulimwenguni.

Katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Malaria inaongoza katika kusababisha vifo, magonjwa na ukuaji na maendeleo mabaya miongoni mwa watoto wachanga. Inakadiriwa kuwa mtoto mmoja hufa kila sekunde thelathini kutokana na malaria sehemu hii.

Malaria husambazwa wakati mtu anapoumwa na mbu aina ya anopheles. Mbu huyu huhamisha vimelea vya malaria, plasmodium, kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine. Watu huugua sana na kuwa na joto kiwango cha juu, kuharisha, kutapika, kuumwa na kichwa, kuhisi baridi na kuwa na dalili kama za homa. Pia kutetemeka na kupapatika kama aliye na kifafa

Miongoni mwa watoto, ugonjwa huu unaweza kuwa mbaya zaidi kwa haraka na kusababisha ukosefu wa fahamu na kifo. Watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano wako kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata ugonjwa huu kwa sababu kinga yao bado ni hafifu sana kukabiliana na ugonjwa huu.

Dalili za malaria kali ni pamoja na mabadiliko katika mwenendo na tabia, uchovu mkubwa kupita kiasi (mgonjwa hawezi kukaa au kusimama, upungufu mkubwa wa damu, kupoteza fahamu, figo kushindwa kufanya kazi na kukojoa mkojo wenye rangi nyeusi/kahawia.

Ni muhimu kuzifahamu dalili za malaria isiyo kali na malaria kali. Iwapo utaona mojawapo au zaidi ya dalili zilizotajwa ni wajibu wako kuwahi kwenye kituo cha huduma za afya ili upate matibabu mapema.

USAFI WA MAZINGIRA:

USAFI wa mazingira ni moja ya kinga muhimu inayoweza kuzuia mbu kushindwa kuzaliana na hivyo kuepusha ugonjwa wa Malaria kushambulia wanadamu katika maeneo wanayoishi.

Tayari wataalamu wa afya wameshatoa elimu ya kutosha kwamba magonjwa ya mlipuko yenye kinga kama Malaria ni muhimu kila familia kuyaweka mazingira katika hali ya usafi.

Serikali kupitia wataalamu hao, imekuwa ikipambana na ongezeko la ugonjwa huo kwa kuhamasisha jamii kujenga makazi bora ili kuudhibiti.

Pia imefanya juhudi kubwa kuhakikisha kuwa inatoa vyandarua kwa kila kaya kujikinga Malaria. Lakini changamoto inayojitokeza mara kwa mara ni baadhi ya watu kutotumia vyandarua hivyo kwa usahihi.

Hivi karibuni mkuu wa kitengo cha uchunguzi na matibabu ya malaria katika mpango wa taifa, Dk. Sisbart Mkunde alisema kuwa, katika utafiti wa mwaka jana asilimia 14. 8 waligundulika na malaria.

Anasema kila mwaka watu milioni 10, hugundulika kuwa na ugonjwa wa malaria na kuongeza kuwa vifo vitokanavyo na ugonjwa huo, huwa 5,000 kila mwaka.

Anasema katika kuhakikisha ugonjwa huo, unatokomea, wamekuwa wakitoa vyandarua ili kuwawezesha wananchi kujikinga .

Anasema pia jamii ambayo inapatiwa chandarua, inapaswa ivitumie kwa matumizi yaliyopangwa na sio kutumia kwa kufugia kuku au kuvulia samaki.

“Kuna baadhi ya watu ambao hawavitumii vyandarua kwa matumizi yaliyopangwa, badala yake kutumia kwa kufugia kuku na kuvulia samaki,’’anasema.

Anasema mwaka 2002 ulianzishwa mpango wa ugawaji vyandarua ambapo mwaka 2014 vilianza kusambazwa kwa hati punguzo.

Anasema mwaka 2006 wigo ukaongezeka na kufanya mama na mtoto chini ya miaka 5 kunufaika na chandarua. Anasema lengo ilikuwa ni kukinga kundi hilo dhidi ya Malaria.

2007 ulianzishwa mpango wa kupulizia dawa katika wilaya za Kagera na Karagwe kutokana na mlipuko ya malaria wa mara kwa mara.

Na ilipofika mwaka 2009, kampeni ya kuwapatia chandarua watoto chini ya umri wa miaka mitano ilifanyika.

2011 walipata fedha kutoka mfuko wa pamoja na walisambaza vyandarua kila kaya, lengo likiwa ni kujenga jamii ambayo haina tatizo la Malaria.

Anasema kuwa katika kukabilia na ugonjwa huo, wamekuwa wakitoa vyandarua kwa kinamama wajawazito na watoto walio na umri chini ya miaka mitano.

Kila mama mjamzito anao wajibu wa kupatiwa chandarua na mtoto aliye na umri chini ya miaka mitano, lakini kama kuna mtu ambaye ataviuza na akakamtwa hatua kali zitachukuliwa dhidi yake, anasisitiza.

Anasema semina za mara kwa mara zimekuwa zikitolewa katika vituo vya afya kwa kinamama wajawazito ambao hufika kliniki kupata matibabu na wamekuwa wakishauriwa kulalia vyandarua ili kuwanusuru kupata ugonjwa wa Malaria.

Charles Mwalimu kutoka kitengo cha mpango wa Taifa wa kuthibiti Malaria kutoka Wizara ya Afya, anasema kuwa katika kipindi cha mwaka 2002-2016 idadi kubwa ya vyandarua ililetwa.

Anasema 2015 hadi 2016 vyandarua vingi wa ukubwa tofauti vilitolewa kwa utaratibu ambao pia uliwezesha chandarua kimoja kutolewa kwa kitanda kilichoweza kulaliwa na watu wawili.

Vyandarua milioni 27 vilisambazwa katika kipindi cha mwaka 2015/16 nchi nzima. Anasema kuwa vyandarua vinasambazwa kwa njia ya kampeni kila baada ya miaka mitatu.

Anasema hadi kufikia kipindi cha mwaka 2019, vyandarua bilioni 15 vitakuwa vimesambazwa nchi nzima. Katika kipindi cha mwaka 2018 hadi 2020, vitasambazwa vyandarua milioni 12 kupitia kiliki. Hivi vitaanza kusambazwa katika mikoa ya Kusini na Kagera ambako tatizo ni kubwa.

Hata hivyo anasema kutokana na ukubwa tatizo eneo hilo, inakusudiwa kuongezewa vyandarua milioni 10.

Aliwaondoa hofu jamii inayohusisha vyandarua hivyo kuwa unapovitumia unaharibu nguvu za kiume au ukitumia unakuwa free masoni. Anasema huo uvumi sio ukweli ni upotoshaji wa baadhi ya watu.

Alitoa onyo kuwa vyandarua hivyo visitumike kuvulia dagaa au kufugia kuku bali kwa malengo yaliyokusudiwa.

Aidha, akinamama wajawazito wanaofika katika vituo vya afya vya serikali wasikubali kuuziwa vyandarau na endapo atauziwa atoe taarifa katika kituo alichoenda kupata huduma ili hatua za kisheria zichukuliwa kwa mtumishi huyo.

Na kwa wale ambao wanabahatika kupata vyandarua wasivitumie kwa mambo mengine kwani atakayebainika hatua kali dhidi yake zitachukuliwa.

Elimu inaendelea kutolewa kwa makundi yote juu ya matumizi sahihi ya vyandarua ili kuwasaidia watumiaji wasipate ugonjwa wa Malaria.

Habari Kubwa