Mawaziri wa Mnangagwa waapishwa Zimbabwe

06Dec 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mawaziri wa Mnangagwa waapishwa Zimbabwe

RAIS mpya wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa ameliapisha baraza lake la kwanza la mawaziri baada ya kuchukua hatamu za uongozi nchini humo wiki mbili zilizopita.

Hata hivyo, rais huyo aliwaondoa katika nafasi zao baadhi ya mawaziri aliokuwa ametangaza kuwateua awali.

Miongoni mwa aliowatupa nje ni waziri wa elimu ambaye alikuwa pia waziri katika uongozi wa mtangulizi wake Robert Mugabe. Baadhi ya watu walipinga kuteuliwa kwake.

Mawaziri wengine aliwaacha baada ya kugundua uteuzi wao ulikuwa unakiuka katiba, anasema mwandishi wa BBC jijini Harare, Shingai Nyoka.

Jumla ya mawaziri 21 walikula kiapo katika baraza linaloundwa na mchanganyiko wa wanasiasa ambao wamekuwa madarakani kwa muda mrefu pamoja na majenerali wa jeshi.

Wakosoaji wanasema uteuzi wa baraza hilo la mawaziri unaonyesha jinsi jeshi lilivyoidhibiti serikali.

Waziri mpya wa ardhi ambaye alikuwa mkuu wa jeshi la anga, Perrance Shiri ameyapuuza madai hayo.

“Nilipokuwa jeshini nilikuwa chini ya wizara ya ulinzi ambayo ni sehemu ya serikali. Na nani amesema wanajeshi hawawezi kuwa wanasiasa? Mimi ni raia wa Zimbabwe na nina haki ya kushiriki katika siasa za nchi hii,” amenukuliwa akiiambia BBC.

Mwanajeshi mwingine, Meja Jenerali Sibusiso Moyo ambaye alitangaza kwamba jeshi lingechukua udhibiti wa serikali ameapishwa kuwa waziri mpya wa mambo ya nje na biashara ya kimataifa.

Amesema atahakikisha uchumi na diplomasia vinaipaisha nchi hiyo.

Rais Mnangagwa ameahidi kufanikisha enzi mpya ya ustawi kwa kuimarisha uhusiano kati ya nchi hiyo na nchi za Magharibi, ambao ulikuwa umedorora chini ya Rais Mugabe pamoja na uhusiano wake na wawekezaji kutoka nje ya nchi hiyo.

Rais Mnangagwa aliwatangaza mawaziri aliokuwa amewateua wiki iliyopita, lakini aliwabadilisha wengine baada ya kugundua kwamba hawakuwa wabunge kinyume na katiba.

Kitendo hicho kimetafsiriwa kuwa ni ishara kwamba rais huyo anawasikiliza wananchi, huku wengine wakisema alifanya haraka kufanya uteuzi katika jambo ambalo ni muhimu kwa ustawi wa taifa hilo.BBC

 

Habari Kubwa