Mazingira ya Jiji Dar yanavyolindwa na wanaouza miche ndani ya mitaa

21Jan 2021
Maulid Mmbaga
Dar es Salaam
Nipashe
Mazingira ya Jiji Dar yanavyolindwa na wanaouza miche ndani ya mitaa
  • Kilio: Elimu ndogo, mauzo yanasuasua

UPANDAJI wa miti ni harakati inayohimizwa katika mataifa yote duniani. Lengo kubwa ni kuhakikisha miti mingi zaidi inapandwa, ili kusaidia mabadiliko ya tabianchi.

Katika kulihimiza hilo, wapo wauzaji wa miche ya miti wanachangia kwa kiasi kikubwa katika utunzaji mazingira, ingawa kuna sura nyingine ya kutokuwapo mwitikio wa kutosha katika ununuzi wa miti hiyo.

Biashara ya uuzaji miche ya miti nchini, hususan katika Jiji la Dar es Salaam tayari ina miaka mingi, wauzaji bado wanalalamika kuwapo hali ya kusuasua.

Umoja wa Mataifa katika Ripoti ya Mwaka 2020, inawataka viongozi wa mataifa yote duniani, kulichukulia jambo la upandaji ni la dharura.

Ripoti hiyo ilieleza kwamba kutoka mwaka 1994 hadi 2020 zaidi ya hekta 420 za misitu zimepotea kutokana na watu kukata miti na kuweka miundombinu mbalimbali ikiwamo kujenga makazi, hivyo ni jukumu la kila mtu kuhakikisha anapanda mti hata mmoja katika mazingira anayo ishi.

Pia kunasisitizwa umuhimu wa kila mmoja, kufahamu kwamba uharibifu wa mazingira unasababisha umaskini, sambamba na madhara mbalimbali ya moja kwa moja.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, madhara yanayoangukia humo yanajumuisha shida ya upatikanaji majisafi, rutuba nzuri katika udongo, mazao na huduma nyingine muhimu za afya na maisha ya binadamu.

Aidha, katika umaskini, pia kunatajwa madhara ya uharibifu wa mazingira yanayoangukia katika kudhoofisha juhudi na uwezo wa binadamu kusimamia na kutumia rasilimali kwa njia endelevu.

SERA YA TAIFA

Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 1997, inaainisha vikwazo sita vilivyoko ambavyo ni uharibifu wa ardhi; uharibifu wa misitu; kupotea kwa makazi ya viumbepori na baianuai; kukosekana maji salama mjini na vijijini; kupungua ubora wa mifumo ya maji; na uchafuzi wa mazingira hasa katika maeneo ya mijini.

Hizo zinatakwa kuingia katika orodha ya vikuu vinavyochangia kuzorotesha ukuaji uchumi na juhudi za serikali katika kupunguza umaskini, hivyo kuathiri maisha na ustawi wa jamii.

Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004, inaeleza wajibu na majukumu ya wadau mbalimbali kuanzia, serikali za mitaa hadi taifa.

Mambo yanayosisitizwa katika sheria hiyo yanajumuisha mazingira kupitia; mipango na usimamizi wa matumizi endelevu; kudhibiti uchafuzi wa mazingira; utunzaji taarifa na takwimu zake; utafiti na ushiriki wa jamii; utekelezaji wa majukumu yatokanayo na mikataba ya kimataifa.

Mengine yanayotajwa ni utii na utekelezaji wa sheria, pamoja na matumizi ya dhana mbalimbali za kusimamia hifadhi ya mazingira hususani tathmini ya athari katika mazingira; tathmini ya mazingira kimkakati; na dhana za kiuchumi na viwango vya mazingira.

Hadi sasa, tayari kuna kanuni, miongozo na programu mbalimbali zilizotungwa kufanikisha utekelezaji sheria hiyo na ni jukumu la serikali, wadau wa mazingira na wananchi kwa jumla kuhakikisha utunzaji mazingira unazingatiwa.

WAUZA MITI

Wauza miti wanasema, uhusiano kati ya miti na mazingira uko wazi, lakini kwa upande wao wanashuhudia aina ya sintofahamu katika mauzo, kutokana mwitikio mdogo wa wananchi katika kuunga mkono suala hilo.

Alli Ramadhani, mkazi wa Tabata Kinyerezi, Dar es Salaam, anasema katika biashara hiyo wapo baadhi ya watu wanaopenda mazingira na hao ndio mara nyingi wananunua miti ya kuipanda katika mazingira yao.

Anasema kati ya miti anayouza ni pamoja ni ya matunda na inayotumika kwa nafasi ya dawa, yote inabaki kuwa na faida inapopandwa katika mazingira ya nyumbani, inazalisha matunda na chanzo cha matibabu.

“Nashauri watu wawe na utaratibu wa kupanda miti mingi katika mazingira yao, kwani ina faida nyingi, ikiwamo utunzaji mazingira, kuleta kivuli nyumbani, pamoja na kusaidia kulinda ardhi,” anasema Ramadhani.

Juma Simba, anayejihusisha na kuu miche ya miti, anasema katika biashara yake amejiwekea utaratibu maalumu wa kuwasaidia wateja kwa kuwapa elimu, namna ya kuipanda na kuitunza, mimea hiyo ikuwe vizuri.

Anasema watu wengi wanashindwa kuikuza vyema miti wanayoipanda, kwa sababu ya kukosa sehemu sahihi ya kupanda mti ikue vizuri, kwa kuzingatia aina ya mti husika.

“Jitihada zaidi zinahitajika katika kuwaelimisha watu umuhimu wa miti, kwani ni idadi ndogo sana ya watu wanao jitokeza kununua miti. Tunachokifanya sisi ni mbinu mojawapo ya kurudisha misitu na tunawarahisishia watu katika utunzaji wa mazingira,” anasema Simba.

Muuza miche huyo anatoa wito kwa wadau wa mazingira na serikali, kuwatatulia changamoto ya upatikanaji vifungashio mbadala vinavyotumika kukuzia miche ya miti, kwani vina uhaba tangu kupigwe marufuku utumiaji mifuko ya plastiki.

Tabu Bakari, mkazi wa Dar es Salaam, ana maelezo kwamba suala la upandaji miti kwa wakazi wa jiji hilo, bado haridhii kiwango cha kipaumbele wanachokipa, kwani sababu ya mazingira yanayowazunguka hayaruhusu upandaji miti mikubwa.

“Asilimia kubwa ya wananchi tunamiliki maeneo madogo, hivyo si rahisi mtu kujiwa na wazo la kupanda miti mingi kutokana na uhaba wa eneo, ‘sana sana’ tunapanda maua kuyafanya mazingira yaonekane vizuri na miti midogo kwa ajili ya kivuli,” anahitimisha Tabu.

Habari Kubwa