Mbabazi anamtaka Museveni kuiga Tanzania

10Feb 2016
KAMPALA, UGANDA
Nipashe
Mbabazi anamtaka Museveni kuiga Tanzania

MGOMBEA urais wa kujitegemea nchini Uganda, Amama Mbabazi amesema viongozi wazuri huwa hawafii madarakani na badala yake hufundisha na kuwaandaa raia wao kuendeleza mfumo wa kuachiana madaraka.

Akiongea kwenye mkutano wa kampeni kwenye shule ya serikali ya Kitgum, Ijumaa iliyopita, Mbabazi alitoa mfano wa nchi ambayo viongozi wake hawang’ang’anii madaraka.

Mgombea huyo wa kujitegemea aliitaja Tanzania kama mfano wa kuiga kwa kuwa rais wake wa kwanza, Julius Nyerere alistaafu baada ya miaka 24 ya uongozi wa taifa hilo.

“Nyerere alimkabidhi madaraka Ali Hassan Mwinyi, ambaye naye akamkabidhi Benjamin Mkapa baada ya miaka 10, kisha Jakaya Kikwete, na sasa wanaye Rais John Pombe Magufuli,” anasema Mbabazi anasema hakuna kitu kipya ambacho mgombea urais kupitia chama tawala cha National Resistance Movement (NRM),

Rais Yoweri Museveni anachoweza kukifanya katika kipindi cha miaka mitano ijayo, alichoshindwa kukifanya katika kipindi chake cha kuwa madarakani kwa miaka 30.

“Nipeni fursa ya kuwa rais wenu ili niweze kuleta mabadiliko ndani ya nchi hii, kwani nilipokuwa ndani ya serikali, hakukuwa na namna ambayo ningeweza kufanya kazi za rais,” anasema.

Mbabazi aliitumikia serikali ya rais Museveni katika nyadhifa mbalimbali za juu, ikiwamo Waziri Mkuu kabla ya kufukuzwa mwezi Septemba, mwaka 2014. Mbabazi anasema anataka kujenga serikali inayowajibika itakayotoa huduma bora kwa wananchi.

“Tunataka utawala wa sheria uchukue nafasi nchini Uganda, na kila mtu awajibike mbele ya sheria, kwani kimsingi hakuna mtu aliye juu ya sheria,” anasema 
 Aliahidi kufufua huduma za afya ikiwamo kumaliza uhaba wa dawa katika hospitali za serikali pamoja na kuongeza madaktari.

Habari Kubwa