Mbegu bora zilivyowaamsha kwa mara ya pili walima miti Mufindi

09Aug 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mbegu bora zilivyowaamsha kwa mara ya pili walima miti Mufindi
  • Neema ya misonobari na mikaratusi

KWA Aidan Fitavangu, kilimo cha miti ni kila kitu kwake, kama ilivyo kwa wakazi wenigne wa kijiji cha Nzinyi, wilayani Mufundi, ambako ni  umbali wa kilomita 600 kutoka soko kuu la jijini Dar es Salaam.

Miche ya miti ikiwa shambani wilayani Mufindi.

Anakitazama kilimo hicho kama nyenzo muhimu katika kupambana na umasikini maeneo ya milimani na anaendelea:“Katika miaka ile nilikuwa ninakiangalia kilimo cha miti kuwa kinaweza kuwa moja ya miradi yenye tija katika kilimo kijijini hapa.”

“Tulikuwa tumezoea kilimo cha chai na nafaka kama chanzo cha mapato, lakini sasa miti imeanza kutuonyesha njia mbadala,” anaeleza Fitavangu, huku amejikita katika kazi ndogo kwenye shambani lake la ekari tatu na nusu.

“Nilianza kilimo hiki miaka michache iliyopita na ndoto zangu zinaelekea kutimia. Nina matarajio makubwa kwenye kilimo hiki. Haikuwa rahisi kwangu kuingia katika kilimo hiki hadi nilipoelezwa kuhusu matumizi ya mbegu bora za miti,” anasema.

Fitavangu, baba wa  watoto watatu na muumnini wa biashara ya kilimo cha miti, anabainisha kuwa mbegu bora za miti ni muhimu kuwezesha mavuno bora na kipato zaidi.

Huku akiwataka wakulima wenzake katika eneo hilo kuanza kilimo cha miti kwa kutumia mbegu bora ili kupata manufaa ya haraka, anatamka: “Ninatarajia kuvuna miaka michache ijayo kwa kuwa nimetumia mbegu bora.

“Uzalishaji mbegu za miti ni hatua muhimu kwa mnyororo wa thamani, kama ambavyo huwezi kuoka mkate mzuri kwa unga mbovu. Kadhalika, unahitaji mbegu bora ili miti ikue sawa sawa.”

Anasema mbegu bora za miti, zinatoka kwenye vitalu vilivyopandwa kitaalamu kutoka vyanzo vinavyojulikana vya miti iliyoboreshwa na ina uwezo mkubwa wa kukua vizuri.

Pia, Fitavangu anasema mbegu hizo zenye ufanisi zinasaidia kuondoa hisia kwamba ‘kilimo cha miti hakilipi’ kwa kuwa kinachukua muda mrefu kukomaa kati ya miaka 15 hadi  20.

Mbegu mpya

Mwakilishi wa asasi ya Jambe Agro, Stephen Salum ana ufafanuzi: “Vifaa vya kupandia na huduma za kuwapa wakulima wa ngazi zote utaalamu na ujuzi unaweza kuongeza ubora wa msitu.”

Salum anasema, huwa wanawawezesha wakulima wa miti kuongeza kipato cha ngazi ya kaya, ikiwa na ziada kulinganishwa na matumizi ya mbegu za kawaida.

Mageuzi hayo ya mbegu yanaelezwa kuwezesha mkulima kupanda hadi kuvuna katika kipindi cha miaka kati ya mitano hadi saba tu, huku Salum anatoa mfano wa miti  milingoti ya umeme, inayotofautiana kulingana na aina ya mti anaolima akifurahia tija .

Anafafanua, mbinu kwamba matumizi ya mbegu bora yanapaswa kwenda sambamba na mbinu za kisasa za ukulima, ikiwamo kutumia mbolea na kupanda kwa umbali unaotakiwa kitaalamu.

“Tunachukua jukumu la kuambaza mbegu zilizoboreshwa na mbinu za ukulima wa kisasa kuongeza ubora wa mazao ambao kwa kufanya hivyo pia tunaongeza tija na kipato kwa mkulima,” anasema.

Salum anadokeza kwamba upandaji miti kama mikaratusi na misonobari ina nafaida kubwa ya ‘kumtoa’ mkulima kiuchumi kutokana na kuwapo soko kubwa, akiinyooshea kidole mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya.

Miti shambani

Salum anasema, unapofanyika upandaji wa miti bora pembezoni mwa mshamba, chanzo kizuri cha mbegu bora za miti kwa wakulima wenyeji, wenye nia ya kuanza ukulima wa kisasa wa miti.

Kutokana na hilo, kuchagua chanzo sahihi cha mbegu za miti ni jambo muhimu kwa mkulima anayetaka kuanzisha mradi wa ukulima wa miti ya kisasa, huku akisisitiza kwamba upandaji una mengi ya tija, ukijumuisha upatikanaji na hali ya hewa.

“Ikiwa ubora wa kijenetiki kwa mbegu haukubaliani na mazingira zinapopandwa, basi sio rahisi kuboresha mazao yatakayotokana na mbegu hizo na hutumia gharama akubwa,” anasema.

Ukulima wa miti nchini, unaelezwa bado una changamoto  ya kukosekana uzalishaji unaotosheleza mahitaji, upatikanaji wa mbegu bora  na jenetiki misituni.

Anaeleza wasiwasi wake katika eneo la wazalishaji kuwa hawana vitalu binafsi na wanaegemea mbegu zinazogawiwa kiholela na zilizokosa ubora.

Kiongozi aliponena

“Wakulima wengi wa miti wakubwa kwa wadogo, hawajui uwepo wa manufaa ya mbegu bora za miti, uwepo wa vifaa bora vya upandaji na hakikisho na ubora wa miche,” anasema Charles Tizeba, alipokuwa Waziri wa Kilimo.

Ni kauli yake katika kuelezea ubora za mbegu kama jambo la msingi katika kuongeza tija katika kilimo. Tizeba anasema: “Ni jukumu la serikali kuhakikisha kuwa mnyororo wa ugavi wa pembejeo unafanya kazi vizuri,”

Kwa mujibu wa Taarifa ya Upatikanaji Mbegu Tanzania ya Mwaka 2017, tasnia ya mbegu nchini ina mifumo miwili; rasmi na usio rasmi.

Mfumo rasmi, unaelezwa ni kwa mkulima anazalisha, anavuna na kisha anatunza na kusambaza mbegu kutika msimu mmoja wa kilimo hadi mwingine.

Kutokana na sababu kama vile ukosefu wa ujuzi na aina za mbegu, pia upungufu wa rasilimali za kumwezesha mkulima kununua mbegu na kutofikika kwa masoko, wakulima wadogo wengi nchini bado wanategemea mfumo usio rasmi.

 

 

 

 

Habari Kubwa