Mbeya shule iliyoanza kwa nyasi yaonyesha inawezekana

12Nov 2019
Beatrice Philemon
Mbeya
Nipashe
Mbeya shule iliyoanza kwa nyasi yaonyesha inawezekana
  • Bado inachangamoto zinazohitaji wadau waichangie
  • Taaluma inapanda na utoro unatokomea

UKIZUNGUMZIA Shule ya Msingi Mbeya, si wananchi wote katika Kata ya Mnyeu, Wilaya ya Newala ilipo, wanaoifahamu.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mbeya, Alphan Gama (aliyesimama), akimuelekeza mwanafunzi wa darasa la tano, Jabiza Abdallah somo la kingereza. PICHA: BEATRICE PHILEMON

Ilianza kama shule ya chekechea, watoto wakisoma chini ya mti wa Mwembe ambapo mwalimu wa kuwafundisha kipindi hicho alikuwa akitoka Shule ya Msingi Mnyehu, iliyo Kata ya Mtopwa, Tarafa ya Kitangari, Wilaya ya Tandahimba, mkoani Mtwara.

Ilianzishwa mwaka 2001, ikiwa ni maalumu kwa ajili ya kupunguza umbali mrefu (Access School au satellite) kwa wanafunzi kutoka vijiji vya Mbeya na Mbebede.

Wakati huo wanafunzi walikuwa wakitembea umbali wa kilometa tano kwenda, vivyo hivyo kurudi kutoka Shule ya Msingi Chaume, iliyo Kata ya Chaume, wilayani Tandahimba, walikokuwa wakifuata elimu.

Hayo ni kwa mujibu wa Mwenyekiti, wa Kamati ya Shule ya Msingi Mbeya, Mshamu Tepu, wakati akizungumza na waandishi wa habari na wafanyakazi kutoka Shirika la ActioAid Tanzania walipoitembelea shule hiyo.

Ilikuwa ni katika ziara ya kukutana na uongozi wa shule na kuona mazingira yake lakini pia wanafunzi kutoka vijiji vya Mbeya na Mbebede wanavyoendelea kielimu pamoja na changamoto zinazowakabili.

“Wakati shule inaanza, wanafunzi walikuwa wakipata shida kipindi cha mvua kwani ilibidi wabaki nyumbani hivyo kukosa masomo, lakini sasa hali ni nzuri ingawa baadhi ya miundombinu haijakaa vizuri kwa sababu ya uchakavu wa majengo, ikiwemo vyoo,” anasema na kuongeza:

“Tulipoona kuna changamoto ya umbali kwenda shuleni kwa watoto wetu, tuliamua kama wazazi mwaka 2001, kujenga kibanda cha miti na kukiezeka kwa nyasi ili waweze kusoma hapa hapa kijijini.” Tepu anabainisha kuwa baadaye waliitisha mkutano wa kijiji uliokubaliana wafyatue matofali kwa ajili ya kuboresha darasa hilo la nyasi.

“Bahati nzuri tulipata ugeni kutoka Shirika la ActionAid Tanzania uliotembelea kijiji chetu kabla hatujaanza ujenzi wa darasa, kuangalia changamoto zinazotukabili,” anasema na kuongeza:

“Tuliwaomba ActionAid Tanzania watusaidie kujenga madarasa kwa ajili ya watoto wetu, kwani wanafunzi wengi kutoka katika vijiji vyetu vya Mbeya na Mbebede walikuwa wanatembea umbali mrefu kwenda kutafuta elimu kijiji kingine.”

Aidha, anabainisha kwamba kutokana na umbali uliokuwepo, wanafunzi wa darasa la kwanza walikuwa wakichelewa kufika shule, kwa sababu umri wao mdogo uliowapa shida ya kutembea umbali wa kilometa tano kwenda na kilometa tano kurudi kila siku. “ActionAid Tanzania walikubali kutujengea madarasa lakini waliomba wananchi nao wachangie katika ujenzi na sehemu itakayobaki wao watamalizia,” anasema na kuongeza:

“Wananchi walifanikiwa kufyatua tofali na kuanza ujenzi hadi kufikia hatua ya boma na baada ya hapo ActionAid Tanzania walimalizia ujenzi wote, ikiwemo kutoa viti na meza kwa ajili ya wanafunzi.”

Anasema mwaka 2008, ActionAid Tanzania walikuja tena kuitembelea shule hiyo na walipoona mazingira ya darasa si mazuri, walijenga tena madarasa mengine mawili na matundu manane ya vyoo kwa ajili ya wanafunzi. “Ndipo tulipoamua kuanzisha darasa la kwanza rasmi mwaka huo wa 2008, shule ikianza na wanafunzi 39, wavulana wakiwa 18 na wasichana 21.

CHAKULA SHULENI

Tepu anasema mfumo wa kuchangia chakula na uji shuleni kwa ajili ya wanafunzi ulioanzishwa na ActioAid Tanzania umeleta mafanikio makubwa. Hiyo ni kwa sababu wanafunzi sasa wanapenda kwenda shule tofauti na miaka ya nyuma.

“Kila mwezi ActionAid walikuwa wanaweka fedha kwenye akaunti ya shule kuwezesha wanafunzi kupata chakula… kupitia mfumo huo watoto wengi wanahudhuria shule, utoro umepungua, watoto wanasoma kwa bidii na ufaulu umeongezeka,” anasema.

Mwenyekiti anabainisha kwamba baada ya wazazi kuona mfumo huu ni mzuri, nao waliamua kuanzisha utaratibu wa kuchangia chakula shuleni, ambapo kila mzazi mwenye mtoto anatakiwa kuchangia.

“Kila mwaka tunachangia chakula kwa ajili ya wanafunzi, huku kila mzazi akichangia kilo 15 za mahindi na kilo tano za kunde na njugu kwa mwaka kwa kila mtoto,” anasema.

Anabainisha, kamati imetenga ekari mbili za shamba kwa ajili ya kilimo cha korosho ili kujiongezea kipato kwa ajili ya maendeleo ya shule, mbegu wakipata kutoka Taasisi ya Utafiti ya Mtopa (Mtopa Research Institute).

MIUNDOMBINU MINGINE

Mwenyekiti anasema kamati yake imepanga kujenga nyumba ya mwalimu kupitia michango ya wananchi. Aidha, anasema imetenga ekari mbili za ardhi kwa ajili ya uwanja wa michezo na kuchimba vyoo viwili vya kudumu kwa ajili ya walimu.

MKUU WA SHULE

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Alphan Gama, anabainisha kwamba shule hiyo ilisajiliwa mwaka 2008, maalumu kuhudumia wanafunzi kutoka vitongoji vya Mbeya na Mbebede.

Mwalimu Gama anasema kuwa mpaka sasa shule ina walimu wa kiume wanne na nyumba moja ya mwalimu. Vilevile, ina jumla ya wanafunzi 123, kati yao, wavulana 67 na wasichana 56.

Kwa upande wa darasa la awali, Mwalimu Gama anasema kuna wanafunzi 102 ambao wanasoma darasa moja na la kwanza, kutokana na uhaba wa madarasa.

UHABA WA WALIMU

Mwalimu Gama anafafanua bado wana uhaba wa walimu, wakiwemo wa kike.

“Kwa mara ya mwisho walimu waliletwa katika shule yetu mwaka 2014, kipindi hicho kulikuwa na walimu watatu tu,” anasema.

Kwa upande wa miundombinu, Mwalimu Gama anasema bado wanahitaji darasa moja kwa sababu darasa la kwanza na la awali wanasoma kwenye chumba kimoja cha darasa na kimechakaa.

“Pia hali ya vyoo si nzuri, vinahitaji ukarabati na kuna darasa lililojengwa na wananchi linahitaji kumaliziwa na kupakwa rangi,” anasema.

TAALUMA

Akizungumzia ufaulu, mwalimu Gama anasema ingawa shule imekuwa na changamoto, bado inafanya vizuri upande wa taaluma.

“Kwa mfano mwaka 2017, jumla ya wanafunzi 14 walifanya mtihani wa darasa la saba na kati yao 10 walichaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari, huku shule ikishika nafasi ya 28 kiwilaya kati ya shule 74,” anasema na kuongeza:

Mwaka 2018, jumla ya wanafunzi 11 walifanya mtihani wa darasa la saba na wanafunzi watano miongoni mwao walichaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari, huku shule ikishika nafasi ya 56 kiwilaya kati ya shule 74.

KUTHAMINI ELIMU

Mwalimu Gama anabainisha kwamba ingawa kwa hivi sasa wazazi wamekuwa na mwamko mzuri wa kupeleka watoto wao shuleni, bado changamoto ipo kwenye suala la umuhimu wa elimu.

“Wazazi wanaturudisha nyuma kwa sababu walimu tunatumia nguvu nyingi zaidi kuhamasisha wazazi katika suala la elimu na chakula. “Unakuta masuala ya sherehe za unyago, ngoma na sherehe zingine ndizo zinazochangiwa fedha nyingi zaidi kuliko suala la elimu,” anasema.

USHAURI

Mkuu huyo wa shule anaasa kuwapo mikutano ya pamoja kati ya wadau wa elimu na wazazi ili kuwaelimisha wazazi juu ya umuhimu wa elimu kwa watoto wao.

“Lakini pia mikutano ya jamii ili kuielimisha juu ya umuhimu wa elimu ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa chakula shuleni kwa ajili ya wanafunzi.

RUZUKU YA ELIMU

Kwa upande wa ruzuku inayotolewa na serikali (Capitation grant), Mwalimu Gama anasema bado haitoshi.

“Kwa mwezi tunapokea Sh. 47,000/- tu za Capitation grant kwa ajili ya matumizi ya stationery, kuchangia mitihani ya elimu, michango ya elimu, kununua chaki, utawala, michezo, ukarabati na gharama za ujenzi,” anasema na kuongeza:

“Fedha hii ni ndogo ukilinganisha na matumizi ya shule, angalau tungepewa Sh. 100,000/- kwa mwezi.”

MAKAMU MWENYEKITI

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Shule, Fatuma Abdallah, anasema kamati imekuwa ikitumia nguvu nyingi kuhamasisha wazazi kuhusu masuala ya elimu.

Hiyo ni kwa sababu kabla ya mwaka 2002, asilimia kubwa ya wazazi walikuwa hawajui kusoma wala kuandika kwa sababu katika maeneo hayo hapakuwa na shule.

Anasema, kabla ya utoaji chakula shuleni, asilimia 25 ya watoto walikuwa watoro.

Habari Kubwa