Mbeya wabanana kukabili upungufu wa madarasa

17Jan 2017
Grace Mwakalinga
Mbeya
Nipashe
Mbeya wabanana kukabili upungufu wa madarasa

AGIZO la Rais Dk. John Pombe Magufuli alilolitoa mwanzoni mwa mwaka jana wakati akiwaapisha Wakuu wa Mikoa, Ikulu Jijini Dar es Salaam kuhakikisha kuwa wanafunzi wote nchi nzima wanasoma wakiwa wamekalia madawati, limetekelezwa kwa kiwango kikubwa, lakini limezua jambo!

Agizo hilo lilikwenda sambamba na utekelezaji wa ahadi yake ya wanafunzi kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne wanasoma bure, limesababisha mafuriko ya wanafunzi katika shule za msingi na Sekondari,ambayo yamekwenda sambamba na ongezeko la madawati ya kutosha katika shule nyingi nchini.

Hata hivyo ongezeko la wanafunzi na uwepo wa madawati ya kutosha limeibua changamoto kubwa ya uhaba wa vyumba vya madarasa hata majengo kwa ajili ya miundombinu mingine kama vile maabara, maktaba na majengo ya utawala katika shule nyingi.

Katika kipindi hiki cha mwanzoni mwa mwaka, shule zimeanza kufunguliwa tayari kuanza muhula mpya wa masomo, tatizo la uhaba wa vyumba vya madarasa limeanza kuwatia hofu wadau wa elimu hususan mkoani Mbeya.

Kipindi hiki,ambacho Shule za msingi na Sekondari nchini zimeanza kufunguliwa, zaidi ya wanafunzi 352 katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu hawana mahali pa kusomea kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa.

Wanafunzi hao watalazimika kuchelewa kuanza masomo, wakisubiri wazazi, wananchi na Serikali washirikiane kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa takriban kumi katika shule takriban kumi ikiwemo Sinde, Uyole, Mwakibete ili wapate mahali pa kusomea.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Tawala Msaidizi Idara ya Elimu, Mkoa wa Mbeya, Protas Mpogole, kwenye Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Mbeya (RCC), mwishoni mwa mwaka jana, ilieleza kuwa wanafunzi 9,450 walifanya mtihani wa kuhitimu elimu ya Msingi.

Ilibainika kuwa kati ya wanafunzi hao, 6,613 sawa na asilimia 69.98 walifaulu na miongoni mwao 6,261 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu.

Kiwango hicho cha ufaulu ni kikubwa kulinganisha na wilaya nyingine zote za mkoa wa Mbeya, hali ambayo inaifanya Halmashauri ya Jiji la Mbeya kuwa na uhitaji mkubwa wa vyumba vya madarasa.

Kutokana na uhaba huo wa vyumba vya madarasa, jumla wanafunzi 352 kati yao wavulana wakiwa ni 102 na wasichana 250 matokeo yao yamezuiliwa kwa muda na hawataanza masomo ya kidato cha kwanza kwa wakati kutokana uhaba wa vyumba vya madarasa.

Kwa mujibu wa taarifa ya elimu ya Mkoa wa Mbeya, Halmashauri ya Jiji la Mbeya pekee lina mahitaji ya vyumba vya madarasa 171 katika shule zake za sekondari, lakini vilivyopo ni vyumba vya madarasa 135 na kuifanya halmashauri hiyo kuwa na upungufu wa vyumba vya madarasa 36.

Upungufu huo ungeweza kusababisha jumla ya wanafunzi 1,620 kukosa mahali pa kusomea, lakini tatizo hilo limeweza kupatiwa ufumbuzi wa muda kwa kuwasambaza wanafunzi waliofaulu katika shule nyingine za jirani na hivyo kupunguza tatizo la uhaba wa vyumba vya madarasa kutoka 36 hadi kufikia vyumba 10.

Kutokana na upungufu wa vyumba vya madarasa pia unazikabili Halmashauri nyingine za mkoa wa Mbeya ingawa kwa kiwango kidogo, hali imemfanya Katibu Tawala Msaidizi katika sekta ya elimu, Mpogole kuagiza Halmashauri zote ikiwemo ya Jiji la Mbeya kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa na upatikanaji wa madawati kwenye vyumba hivyo haraka ili watoto wote waweze kuanza masomo.

David Mwashilindi ni Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya, anasema kuwa, vyumba kumi vya madarasa vinahitajika ili kukidhi mahitaji ya wanafunzi hao, ambao awali hawakupangiwa shule za kwenda.

Akizungumzia mpango wa Jiji wa kunusuru hali hiyo anasema wameamua kuunda Kamati kwa ajili ya kushughulikia suala hilo ili waweze kulikamilisha na kuwezesha wanafunzi waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu wanaanza masomo kwa wakati.

Anaongeza mikakati waliyojiwekea kama Halmashauri ni kuwataka Madiwani, Maofisa Watendaji na Wenyeviti wa Mitaa kwenda kuwahamasisha wananchi katika kila kata kuchangia ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa.

Anasema kuwa, ili kuunga mkono jitihada za wananchi katika ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa, Halmashauri yake imechangia shilingi milioni mbili kwa kila chumba cha darasa kinachojengwa.

Meya Mwashilindi anasema umoja wao wameweka pembeni tofauti zao za kisiasa na kuungana ili kutatua changamoto hiyo, iliyokuwa inaleta taswira mbaya kwa Jiji la Mbeya kutokana na Jiji hilo kuwa na sifa ya kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaofaulu kujiunga kidato cha kwanza.

Anasema uhaba wa vyumba vya madarasa Sekondari za Halmashauri ya Jiji la Mbeya ni kiashiria cha ufaulu mzuri na wa kuridhisha kwa wanafunzi, jambo ambalo ni la kupongeza na akaishauri Serikali kuwa na utaratibu wa kujenga vyumba vingi vya madarasa ili kuepuka changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa kila mwaka.

Mwashilindi amewahakikishia wanafunzi wote waliofaulu na kuchaguliwa kujiunga kidato cha kwanza kuwa, wataanza masomo katika muda muafaka na amewataka wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao shule.

Jitihada zinazoendelea amesema, anaamini kuwa ujenzi wa vyumba vya madarasa utakamilika hivi karibuni na kuwezesha wanafunzi wote waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza kuanza masomo mara moja.

“Tunawashukuru wananchi pamoja na Serikali kwa jitihada zao ambazo zinaelekea kumaliza changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa kwa wanafunzi wetu.Lilikuwa suala linaloumiza vichwa sana, lakini sisi kama viongozi tulishikamana na kuweka nguvu ya pamoja katika kufanikisha suala hilo,” anasema Mwashilindi.

Mwashilindi anasema, sehemu kubwa ya ujenzi wa vyumba hivyo unahitaji umaliziaji kutokana na kuwa wananchi pamoja na Serikali walikwisha anza ujenzi wa vyumba kwa baadhi ya shule hata kabla ya agizo hilo ulirahisisha kukabili changamoto hiyo.

Mchango , ambapo mchango wa Serikali ya Jiji ilitoa shilingi milioni mbili kwa kila chumba cha darasa.

Eva Mkalawaye ni Afisa Mtendaji wa Kata ya Sinde, yenye shule moja ya Sekondari iitwayo Sinde, anafurahishwa na ujenzi unaoendelea wa vyumba viwili vya madarasa kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka huu.

Anasema kata yake yenye mitaa minne ya Ilolo kati , Jani bichi, Sinde A na Kagwina, ina wananchi 4,816 na ili kufanikisha ujenzi huo kila mtu mwenye umri wa zaidi ya miaka 18. alitakiwa kuchangia sh 3,000 kwa ajili ya ujenzi huo.

Mkalawaye anasema, hadi sasa shilingi laki sita zimepatikana na watu wengine wameahidi kutoa michango.Fedha .hizo zimesaidia kununulia mabati na kuwalipa mafundi.

Kwa mujibu wa Mkalawaye, shughuli za ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika Sekondari ya Sinde unategemea nguvu kutoka kwa wakazi wa kata mbili za Sinde na Manga ambayo haina Sekondari.

“Tumetii agizo la Halmashauri la kuwahamasisha wananchi kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa katika kata yetu, wengi wamehamasika na wametoa.Changamoto iliyopo ni baadhi kulihusisha suala hili na kisiasa, lakini viongozi wa eneo hili, tumeunda sheria ndogo za kuwabana wale wote ambao hawatatoa mchango wa ujenzi,” alisema Mkalawaye.

Mwalimu mkuu wa Shule ya Sekondari Sinde, Samson Kamendu, anaeleza kuwa, wamejiandaa vyema kuwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza.

Habari Kubwa