Mbinde ya safari kwenda visiwani Koma na Kwale

26May 2016
Mary Geofrey
Mkuranga
Nipashe
Mbinde ya safari kwenda visiwani Koma na Kwale

SAFARI ya kwenda visiwa vya Koma na Kwale vilivyoko wilayani Mkuranga, ni mtihani mkubwa uliozingwa na maajabu mengi.

Mtu anapotaka kupata ushuhuda wa maajabu hayo, anapaswa kusogea hadi pwani ya kijiji cha Kisiju kilichoko umbali wa kilomita 40 kutoka mjini Mkuranga.

Hapo ndipo atakaposhuhdua mazito yanayoanza na maandalizi ya safari hadi mwendo mzima wa safari yenyewe.

Wakati jijini Dar es Salaam, daladala la abiria kati ya 24 na 44 huchukua chini ya dakika 10 kujaza abiria, boti linalochukua abiria 20 Kisiju, huchukua kati ya siku mbili na tatu kupata abiria wa kutosha, ili lianze safari.

Namna abiria wa kuelekea Koma na Kwale wanavyopata hifadhi kusubiri safari, wanavyoanza safari katika hatua ya kuingia katika boti na mizigo yao na mfumo wa safari nzima hadi kufika waendako, si wa kawaida.

Kisiju ambayo ni kijiji kikongwe cha wakulima wa mazao kama mihogo na nazi, sehemu kubwa ya wakazi wake ni wavuvi.

Ni mahali kunakotumika kama bandari ya kuanza safari ya kwenda Koma na Kwale. Kuna majengo ya wakazi, mengi yakiwa jirani na ufukweni na kuna maduka kadhaa yaliyoko katika majengo hayo duni.

Pia kuna vibanda vinavyotumiwa na wavuvi na wasafiri wa kwenda na kutoka visiwani, kama sehemu ya kupumzikia.

Huduma nyingine za kupumzika ni magogo ya mnazi ufukweni kuna mitumbwi mingi ya uvuvi na michache inayotumika kusafirisha abiria kwenda visiwani.

Vijiji vingine katika pwani hiyo ya Mkuranga yenye umbali wa kilomita 90, ni; Hungubweni, Mpafu, Kerekese, Mdimni, Magawa na Kifumangao.

SAFARI YENYE MAJANGA

Ni safari inayochukua si chini ya saa moja kutoka Mkuranga mjini kuelekea pwani ya Kisiju.

Mara nyingi ni kawaida kwa abiria anayetoka nje ya Kisiju, lazima kupitia njia hiyo inayochukua si chini ya saa moja ikiwa ni ya vumbi na makorongo mengi.

Usafiri unaotumika ni pikipiki namabasi madogo aina ya Toyota Hiace yaliyochakaa mno na.

Mtu anapofika Kisiju, inakuwa katimizas awamu ya kwanza ya safari, akijiandaa na awamu ya pili kuelekea Koma ambako ni kilomita 50 kutoka Kisiju na Kilomita 30 kuelekea Kwale.

Mtihani mkubwa uko katika safari ya kutoka kijiji cha Kisiju kuelekea visiwa hivyo, kwani usafiri pekee ni wa mashua.

Nauli ya safari hiyo ni Sh. 8,000 na watoto wanatozwa Sh. 3,500, katika safari inayowachukua abiria wastani wa siku mbili hadi tatu kusubiri, kama
hali ya hewa ni shwari.

Inapotokea hali ya hewa si shwari, basi siku zinaongezeka kusubiri hali ya hewa itulie.

Lini boti linaondoka? Ni swali lnalojibiwa kwa abiria kutaarifiana mahali hapo na ndio inayotumiwa na mabaharia kujua idadi ya abiria wanaowasubiri.

Juma Abeid ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mkuranga, anayetamka: “Mashua moja inapakia abiria 15 hadi 20. Hivyo kama hawajatimia abiria hawawezi kupelekwa.”

Abeid anabainisha kwamba katika kipindi cha subira, abiria wa kwenda visiwani wanalazimika kuishi nyumba za wakazi wa Pwani ya Kisiju kusubiri safari yao.

“Huku watu wanaishi kama ndugu. Hivyo kama abiria akifika kijiji cha Kisiju ukakuta abiria hakuna, analazimika kuomba hifadhi kwenye nyumba za kijiji hicho hadi mashua itakapoondoka,” anasema.

“Abiria wakiwa wachache hawawezi kupelekwa hadi watakapotimia, kwani wachuuzi wanapata hasara. Lakini hali ya hewa ikichafuka, chombo kinalazimika kusubiri hali ya hewa ikae sawa,” anasema Abeid, akifafanua uhalisi wa mfumo wa usafiri uliopo.

Pia anaeleza aina za usafiri unaotumiwa zaidi ni mashua, pia boti za kukodi ambayo nauli yake kutoka Kisiju hadi kisiwani Koma ni Sh. 150,000.

HALI HALISI BAHARINI

Safari ya kwenda visiwani kutoka Kisiju na kurudi kutoka Visiwani, tangu mwanzo msafiri anapaswa kuwa na ‘damu’ ya uhabaria.

Hiyo inatokana na safari kuelekea kupanda chombo cha usafiri inaanza na kuingia majini kufuata usafiri huku wamezingwa na maji kiwango cha magotoni wakiwa na mizigo yao.

Baada ya kuingia katika chombo, hatua inayofuata, wasafiri wanaelekezwa na waendesha chombo wahifadhi bidhaa zao kwenye mifuko ya plastiki, ili kujikinga na maji.

Huo ndio uhalisia wa ilivyokuwa mwanzo wa safari yangu. Niliambatana na viongozi wa wilaya, akiwamo mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ulega, aliyekuwa akielekea kukagua miradi ya maendeleo. Ni safari iliyochukua saa mbili.

MAZITO YA SAFARI

Ilikuwaje? Safari ilianza kijijini Kisiju kwa boti kung’oa nanga saa 2:20 asubuhi, siku ya Jumamosi ya Mei 14 mwaka huu. Katika lugha rahisi ni wiki moja na nusu iliyopita.

Sikuwa na uelewa wa sababu ya kuweka mizigo hiyo kwenye mifuko ya plastiki, kwani katika hisia za kawaida, nilidhani utaratibu wa kupaki mizigo, kumbe hali haikuwa hivyo.

Baada ya dakika 15 tangu safari kuanza kuelekea kisiwa cha Koma, ndipo nilipoanza kuelewa maana ya abiria kusisitizwa kuhifadhi vifaa kwenye mfuko.

‘Kindumbwendumbwe’ kilianza kushuhudiwa baada ya maji yaliyokuwa yanasukumwa na upepo mkali ulioambatana na mawimbi ya habari, kuanza kupiga ukuta wa boti na kutua katika nyuso zetu.

Yalikuwa mawimbi mazito tuliyokabiliana nayo yakitoka upande tunakoelekea na kufanya tuwe ‘tunapanda’ huku boti likiyumba kwa ‘kupanda’ na ‘kushuka’ dhidi ya mawimbi hayo.

Iikuwa salamu tosha ya hali halisi, kwamba sasa niko majini na si nchi kavu. Haraka niliomba msaada wa hifadhi ya simu yangu kwa ajili ya usalama wake, kutoka mkononi nilikoishikilia.

Nilitapatapa kushindwa kuzoea hali hiyo kwa masikitiko ya kujeruhiwa kiafya na urembo wangu, huku mfumo wea maisha unageuka, kila abiria anaonekana na hulka ya kujijali zaidi kuliko kumjali mwenziwe.

Kadri safari ilivyopamba moto, maji yalizidi kuruka kwa kasi pande zote za boti na kunilowesha na abiria wengine wote tuliokuwa kwenye boti.

Ingawaje kuna usemi ‘shida haizoeleki’ lakini binafsi taratibu nilianza kuzoea msukosuko ule baada ya kutumia robo tatu ya safari.

Kwa uzoefu wangu ilikuwa jambo geni, lakini kwa abiria wenzangu akiwamo mbunge Ulega, hawakushangaa chochote kutokana na uzoefu wao. Waliendelea kupiga soga na safari ikiendelea.

Hata ile hali ya kuloa chapachapa, haikuwakwaza, jambo ambalo kwangu mkazi wa Dar es Salaam niliyezoea daladala na usafiri mwingine wa magari, ulikuwa mtihani mkubwa.

MTIHANI WA KUSHUKA

Saa 4:20 asubuhi tuliwasili kijijini Koma, ikiwa ni safari ya saa mbili kamili kwa boti kutia nanga katika kisiwa hicho.

Hata hivyo, mabaharia wanafahamisha kuwa safari hiyo mara nyingine huchukua hadi saa nne, pindi hali ya bahari inapokuwa mbaya.

Hata hivyo, dhana ya hatari kutokana na haikuishia hapo, kwani nilikutana na mtihani wa kushuka. Ili kufika ufukweni, abiria tuliomaliza safari tulitakiwa kudumbukia. Baadhi walifanya hivyo katika maji yanayofikia kiunoni na kuanza kutembea taratibu kuelekea ufukweni.

Kutokana na ugeni wa baadhi yetu wageni, ilikuwa ngumu sana hadi mabaharia walipotoa msaada kwa ujira mdogo kutubeba ‘tuliochemka’ kwenye uvukaji huo.

Nililazimika kupanda juu ya shingo ya kijana mwenye mwili wa miraba minne, aliyeninyanyua mithili ya kifaranga cha kuku.

“Utulivu wako ndio usalama wako. Mimi siwezi kukudondosha, ila ukiangaika utajidondoha mwenyewe kwenye haya maji,” alimtamkia kijana aliyenibeba na kunishikilia miguu yangu, mithili ya mwali wa Kimakonde anayenema.

Sauti ile na hali halisi ya maji aliyokuwa ameyakanyaga kijana yule, ndio iliyonifanya kushusha pumzi na kupiga moyo konde kutulia juu ya mabega hayo.

Ni kazi iliyofanywa kwa ujira wa Sh. 500 kwa kila abiria aliyetaka huduma ya kubebwa.

Mbebaji huyo anajitetea kuwa ni kazi inayompa posho za ziada, mbali na malipo anayopewa na mmiliki wa chombo ca usafiri.

Nilipofika ardhini, ndipo nilipoanza kuona raha ya safari iliyotaka kuniharibikia njiani.

Taratibu nilianza kusogea ardhini huku nikiletewa mkoba wangu uliokuwa umefunikwa na turubai chini ndani ya boti.

Katika hali ambayo niliona watu wa huko wamezoea, ni pale mbunge Ulega alipoungana na wananchi wake kukanyaga maji yaliyowalowanisha maungo yao bila kujua chochote.

MKAKATI WA MBUNGE
Abiria wanaotoka Koma, wanalazimika kuelezana au kukubaliana siku ya kusafiri kuelekea wilayani Mkuranga, kwa ajili ya shughuli zao, ili kupanda usafiri wa pamoja.

Wafanyabiashara wa bidhaa za majumbani, nao wanalazimika kuagiza siku maalum na boti ambazo hupelekwa kwa pamoja, ili kupunguza usumbufu.

Ulega ambaye ni muonja machungu ya boti, anaahidi kuboresha huduma hizo kwa kuhakikisha kunakuwapo boti za kisasa pamoja na vifaa vya kujiokoa.

“Wageni wanaotoka nje ya wilaya ya Mkuranga ndio wanaopata shida ya kutumia usafiri huu, hivyo tunalazimika kuboresha mazingira na vifaa ili kuwarahisishia maisha na kufanya shughuli zao,” anasema.

Anaongeza kuwa ili watumishi wanaopelekwa kufanya kazi katika visiwa hivyo wasikimbie wanatakiwa, kupata mahitaji muhimu kama usafiri na mahitaji muhimu.

“Kwale na Koma ni visiwa ambavyo vilisahaulika. Nimeamua kwa dhati kuhakikisha nawapatia huduma muhimu wanazohitaji,” anasema.

Habari Kubwa