Mbinu udhibiti uharibifu wa vifaa umeme hizi hapa

04May 2021
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Mbinu udhibiti uharibifu wa vifaa umeme hizi hapa

TEKNOLOJIA ambayo ni maarifa na ujuzi wa kisayansi unaotumika katika kutatua na kuboresha maisha ya watu, iwe kwa njia ya mashine,vifaa na mitambo inazidi kupanuka na kugundua mambo mapya yanayoongeza ustawi katika jamii.

Zama hizi ubunifu unazidi kupanuka katika nyanja nyingi ukiwamo ujio wa vifaa mbalimbali kwa mfano vya umeme, vinavyotumika kulinda mifumo ya umeme ili kupunguza uharibifu wa vitu viwe vya nyumbani au viwandani pale hitilafu inapotokea, lengo likiwa ni kuviacha salama na kupunguza dosari zisizo zinazoepukika.

Kifaa kinachokabiliana na nguvu ya umeme inapoongezeka kwa kuizuia isiunguze vifaa kama jokofu, runinga, redio nyumbani na jenereta, viyoyozi na mifumo ya kompyuta viwandani ni mojawapo ya manufaa ya ugunduzi huo.

Kifaa hicho kinatajwa pia kuwa ni mahiri kumaliza tatizo kwenye mfumo wa usafirishaji wa umeme hadi unapowafikia watumiaji, ni kwa mujibu wa Ofisa Masoko wa kampuni ya Sine Tamer East Africa, Samson Odera.

Anasema ugunduzi huo unalenga kuzihimiza taasisi za umma na binafsi na wateja binafsi kufunga kifaa hicho cha Sine Tamer Black Box ili kulinda mifumo ya umeme na kupunguza uharibifu na hasara inapotokea hitilafu.

Katika mazungumzo na gazeti hili wakati wa kutambulisha kifaa hicho jijini Dar es Salaam hivi karibuni, anasema wanaunga mkono hatua za serikali za kuipatia Tanzania umeme wa kutosha kwa maendeleo.

"Kumekuwapo na tatizo la umeme kuongezeka ghafla ‘power upsurges’ na wakati mwingine kuwapo na umeme mchafu ‘transient’, kutokana na sababu mbalimbali na kusababisha athari…”

Anasema ili kulinda vifaa hivyo iwe viwandani au nyumbani ni muhimu kuweka mifumo hiyo ili kuwa salama, anaongeza Odera.

Ujio wa kifaa hicho unakuja wakati serikali imefanya jitihada mbalimbali kuongeza umeme ili kuwapatia wananchi nishati ya kutosha kuanzia majumbani, taasisi za umma na binafasi na hata viwandani.

Katika jitihada za kuboresha nishati nchini, inajenga bwawa la umeme la Nyerere au Stigler’s linalotarajiwa kuzalisha megawati 2,100 za umeme utakaotumika kuanzia majumbani, viwandani na hata kuuza ziada nje.

Lakini, pamoja na serikali kufanya jitihada hizo za kuboresha huduma na kuongeza upatikanaji wa umeme, lipo tatizo linalotatiza jitihada hizo, ambalo ni uwezo wa kulinda vifaa vinavyotumia nishati hiyo.

KWA NINI?

Anasema kuna haja ya kuwa na Sine Tamer Black Box ili kuepusha uharibifu na kwamba jitihada hizo zimelenga kuwasaidia wateja wa makundi yote wanaotumia umeme.

"Kwa kushirikiana na kampuni ya Energy Solution tunatoa huduma ya kifaa hicho kulinda mifumo ya umeme kuanzia majumbani, taasisi mbalimbali za huduma, viwandani na popote tunapohitajika," anasema.

Ili kuepusha uharibifu huo kampuni yao inaendelea kutilia mkazo ndoto za serikali ya awamu ya tano ya kutaka kuwa na Tanzania ya viwanda ifikapo mwaka 2025, kwa kuhimiza ufungaji wa kifaa hicho ili kuepusha madhara.

"Hii ni teknolojia mpya iliyovumbuliwa na wataalamu kwa manufaa hata kwa shule zenye nishati hiyo, ili kuepusha tatizo la ukatikaji ovyo wa umeme," anasema.

UFUNGAJI

Ofisa masoko huyo anasema, hadi sasa tayari wameshafunga vifaa hivyo kwenye baadhi ya viwanda, taasisi za fedha na katika maeneo mengine nchini ili kukabiliana na uharibifu unaoweza kusababishwa na hitilafu ya umeme kuongezeka ghafla.

"Tumefunga katika Ofisi za Wakala wa Mkemia Mkuu wa Serikali, Hospitali ya Taifa Muhimbili na katika benki kadhaa ikiwamo NMB na CRDB na tunaendelea kufanya kazi hiyo kwa wale ambao wanahitaji huduma yetu," anasema.

Anafafanua kuwa Tanzania kama mataifa mengine yaliyopitia hatua hiyo ya msingi ya mapinduzi katika teknolojia, kampuni yao imeona kuna haja ya kusaidia kuimarisha huduma ya nishati kwa kuleta kifaa hicho.

Anasema, wao wameamua kuja na teknolojia hiyo, ambayo wanaamini kuwa iwapo taasisi, nyumba na viwanda zitafunga kifaa hicho, hitilafu za umeme zitapungua na hivyo kuwa na manufaa katika shughuli za maendeleo.

"Tunataka kuhakikisha tunatoa mchango, sio tu kuwa na mtazamo wa kuona mafanikio makubwa kwa kutumia teknolojia hii mpya, bali pia kuelekeza njia za kuondoa vikwazo vinavyosababisha umeme kuwa na hitilafu," anasema.

VIPI GHARAMA?

Mwanzilishi na Rais wa Kampuni ya Energy Control System (ECS), Jeff Edwards, kutoka Texas Marekani, anasema, kifaa hicho na kinasaidia upunguzaji wa gharama za matumizi ya ukarabati wa mitambo.

"Baadhi ya vifaa kama balbu, zinaungua kutokana na umeme kuja kwa kasi au kuwa na uchafu, hivyo kampuni yangu iko tayari kushirikiana na East African Sine Tamer kuhakikisha tatizo hilo linaisha nchini," anasema Edwards.

Hivi karibuni, Rais huyo alikuwa jijini Dar es Salaam akishirikiana na East African Sine Tamer kuelezea umuhimu wa kifaa hicho, kwa lengo la kuhimiza matumizi ya kifaa hicho ili kuboresha huduma mbalimbali.

"Kufunga kifaa hicho kunapunguza gharama za matengenezo ya umeme kwa asilimia 80 na kupata faida zaidi, hivyo ni muhimu nchi kuwa na umeme ambao mifumo yake inalinda na kutunza vifaa mbalimbali vinavyotumiwa kwenye uzalishaji," anasema.

Habari Kubwa