Mbio za Mwenge ziendelee kuumbua wanaofisadi miradi ya maendeleo

12Jun 2019
Sabato Kasika
DAR
Nipashe
Mbio za Mwenge ziendelee kuumbua wanaofisadi miradi ya maendeleo

MWENGE wa Uhuru kwa sasa unaendelea kukimbizwa mikoa mbalimbali nchini ukiwa na kaulimbiu isemayo; “Maji ni haki ya kila mtu, tutunze vyanzo vyake na tukumbuke kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.”

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan (aliyeshikilia mwenge mwenye miwani), akimkabidhi Mwenge kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa kwa mwaka 2019, Mzee Mkongea Ali kuashiria kuanza kwa mbio za Mwenge wa Uhuru 2019. Kulia ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa. (PICHA: OFISI YA MAKAMU WA RAIS

Uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa ulifanywa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan Aprili 2 mwaka huu, kwenye uwanja wa Mlowo mkoani Songwe na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali.

Katika uzinduzi huo, Makamu wa Rais alitoa rai kwa Watanzania kutumia mbio hizo kwa mwaka huu kumkumbuka Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kwa kupinga vitendo vyote vya dhuluma.

Lakini pia ufisadi, rushwa, maradhi, chuki, dharau huku akiwataka kuenzi umoja na mshikamano na kuchapa kazi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

“Nimependezwa na kaulimbiu hii ambayo ina uwiano wa moja kwa moja na jukumu langu la kila siku la kusimamia na kutunza mazingira nchini... sote tunafahamu kwamba bila utunzaji thabiti wa mazingira basi vyanzo vya maji hupotea,” akasema.

Yapo mengi aliyoyasema Makamu wa Rais katika uzinduzi huo, lakini hapa ninataka kujikita zaidi katika kile ambacho kimekuwa kikiibuliwa na mbio hizo.

Mwenge unaendelea kuzunguka mikoa mbalimbali nchini huku kukiwa na kumbukumbu ya miradi hewa ambayo ilibainika katika mbio za mwaka 2018.

WAZIRI MHAGAMA

Wakati akitoa taarifa za mbio za Mwenge wa Uhuru Oktoba 2018 jijini Tanga, Waziri wa Nchi, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, aliweka wazi miradi hewa iliyoibuliwa na mbio hizo.

Kwamba Mwenge wa Uhuru kwa mwaka jana ulizindua miradi 1,432 ya thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 664 kwenye mikoa 31 na halmashauri 195, lakini kati ya miradi hiyo 64 iligundulika kuwa na ubadhirifu wa zaidi ya Sh. bilioni 27.

Mhagama akasema mwenge huo umekuwa ukifanya kazi ya kupambana na kufichua rushwa katika miradi yote iliyozinduliwa na kuwekewa jiwe la msingi nchini kote huku mingine ikiachwa kutokana na kuwa na kasoro.

“Mbio za Mwenge wa Uhuru zimetumika kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo, kumulika na kuchoma uzembe ambapo kwa mwaka huu wa 2018 zimebaini kuwapo kwa kasoro katika kutekeleza miradi ya maendeleo,” akasema na kuongeza:

“Miradi 80 yenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 27 za halmashauri 64 ilionekana kuwa na kasoro hivyo haikuzinduliwa wala kuwekewa jiwe la msingi.”

Kaulimbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka jana ilikuwa ni; ‘Elimu ni ufunguo wa maisha, wekeza sasa kwa maendeleo ya Taifa letu’

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alibainisha dhamira ya serikali kupitia kaulimbiu hiyo ni ya kuwashirikisha wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo kuwekeza katika elimu ili kuzalisha rasilimali watu yenye ujuzi na stadi zitakazowezesha kuchochea mapinduzi ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo 2025.

“Ukitaka kuleta maendeleo ya uchumi ulio imara, ukitaka kujenga jamii inayoheshimu na kufuata misingi ya uwajibikaji na ubunifu, ukitaka kujenga taifa lenye amani na utulivu, lazima uwekeze zaidi katika elimu,” anasema.

MBIO ZA MWENGE 2019

Siku chache baada ya uzinduzi huo, kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa kwa mwaka huu alianza kukumbana na madudu katika miradi ya maendeleo.

Kiongozi huyo, Mkonge Ally, aligoma kuzindua mradi wa kwanza wa ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Igunda kutokana na mgongano wa taarifa.

Mradi huo uko wilayani Mbozi, ambapo taarifa aliyosomewa na Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Igunda, Mwanyukwa Myuki ilionyesha kwamba Sh. 537,000 za ujenzi wa zahanati hiyo, zilitokana na michango ya Mwenge wa Uhuru zilizochangishwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.

Mtendaji huyo alisema jengo hilo limegharimu Sh. 32,726,400 zilizotolewa na wadau ambapo wananchi wametoa Sh. 13,721,300, halmashauri Sh 10, 355,011, Mfuko wa Jimbo Sh. 1, 278, 000 na Sh. 6, 835, 000 zimetoka kwa wadau wa maendeleo.

Wakati akiendelea na mbio za Mwenge mikoa mbalimbali nchini, kiongozi huyo ameendelea kubaini kuwapo kwa madudu kwenye baadhi ya miradi ya maendeleo, hali ambayo imesababisha miradi hiyo isizinduliwe.

Kwa mfano mwezi huu wa Juni kuna miradi kadhaa ambayo amekataa kuizindua ukiwamo wa maji uliopo Halmashauri ya Geita, ambao taarifa zimepishana.

Kwamba hawezi kufungua mradi huo kutokana na taarifa za utekelezaji wake kupishana kwa gharama ya Sh. milioni 9, ambapo ameagiza Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) kuchunguza taarifa za mradi huo na kukabidhi taarifa kwa wakimbiza mwenge ndani ya siku 10.

Siyo hapo tu bali mwezi huu pia amekataa kupokea mradi wa sekta ya maji na barabara wenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 484.9 kwa sababu nondo zilizotumika katika ujenzi huo hazikupimwa.

Mradi upo wilaya ya Tarime mkoani Mara na kuagiza mkuu wa wilaya hiyo, Charles Kabeho kutoa taarifa ndani ya wiki mbili.

Vilevile kiongozi huyo amekataa kutoa hundi ya Sh. milioni 100 kwenye Saccos ya Tuimarike, kwenye Halmashauri ya Mji wa Kahama, kutokana na kile alichodai kwamba mkurugenzi amekiuka sheria ya vikundi iliyopo.

Safari ya mbio za Mwenge wa Uhuru inaendelea hadi Oktoba mwaka huu,  sasa ni mwezi Juni, na tayari baadhi ya miradi ya maendeleo imekataliwa. Je, kama hali itaendelea kuwa kama hivi, kufikia Oktoba itakuaje?

MASLAHI YA UMMA MBELE

Moja ya mambo ambayo Rais John Magufuli anahimiza viongozi, ni  kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, sambamba na kuhakikisha wanasimamia matumizi ya rasilimali za umma kwa maslahi ya wananchi.

Rais anaamini kwamba utekelezaji wa majukumu kwa kuzingatia sheria, ni njia ambayo inasaidia kuepusha uchakachuaji kwenye miradi ya maendeleo, lakini inaonekana bado wapo ambao hawajazingatia hilo.

Mfano hai ni taarifa hizi za kuwapo kwa miradi ya maendeleo ambayo haikuzinduliwa na mbio za Mwenge wa Uhuru za mwaka jana na za mwaka huu ambapo pia ipo baadhi ya miradi imekataliwa wakati mbio hizo zikiendelea.

Ninaamini kwamba kama wahusika wangezingatia wito ambao umekuwa ukitolewa mara kwa mara na Rais, basi wangetimiza wajibu wao kwa kuzingatia kwamba katika maendeleo yoyote yale kuna haja ya kuzingatia ushirikishwaji wa wananchi ili kuepuka uchakachuaji.

Ikumbukwe kwamba ushirikishwaji wa wananchi katika miradi ya maendeleo ni hatua ambayo wale waliokusudia kuanzisha mradi kwenye eneo fulani hushirikisha wananchi husika, ambao kimsingi ndio mradi unaowalenga.

Pamoja na hayo, wale ambao bado hawajafikiwa na mbio za Mwenge wa Uhuru na wamefanya vitu ambavyo ni kinyume na utaratibu, basi wajue kuwa watajikuta katika mnyororo huo wa miradi yao kukataliwa.

Taarifa ya baadhi ya miradi ya maendeleo kutozinduliwa katika mbio za Mwenge wa Uhuru za mwaka jana zilitosha kuwa fundisho, lakini hali hiyo inapoanza kujitokeza tena mwaka huu, ni wazi bado kuna tatizo.

Habari Kubwa