Mbunge ahoji utitiri leseni wachimbaji wa tanzanite

28May 2019
Na Mwandishi Wetu
DODOMA
Nipashe
Mbunge ahoji utitiri leseni wachimbaji wa tanzanite

MBUNGE wa Mtwara Mjini, Maftaha Nachuma (CUF), amehoji bungeni sababu za serikali kutoa leseni nyingi kwa wachimbaji wa madini ya tanzanite.

Akichangia bungeni jijini Dodoma jana mjadala wa makadirio ya bajeti ya Wizara ya Madini kwa mwaka ujao wa fedha, Maftaha alisema kutokana na wingi huo wa leseni za uchimbaji wa tanzanite, kumekuwa na changamoto ya migogoro inayosababisha wachimbaji kuwa na wakati wakitekeleza majukumu yao migodini.

"Nataka niweze kufahamu utekelezaji ukoje kuhusiana na tanzanite, tuliona kumekuwa na mrundikano wa leseni na kubaini leseni 900 ambazo zimetolewa na wizara.

"Na changamoto kule chini kuna mtobozano, je, pendekezo lile tumefikia wapi? Kule chini wanauona, utekelezaji wake ukoje?" Mbunge huyo alihoji.

"Pia nilitaka kujua One Stop Centre itajengwa Arusha na utaratibu ukoje kwani tatizo ni kubwa sana hasa kwenye uchenjuaji.

"Watanzania wanakosa ajira sababu madini ya tanzanite wanachenjua nje, na kule China zaidi ya watu 6,000 wamepata ajira," alisema.

Mbunge huyo pia aliitaka serikali kulieleza Bunge kuhusu hatua ilizozichukua kudhibiti njia zaidi ya 400 za utoroshwaji wa madini ya tanzanite.

"Waziri atueleze, wakati tunapopitia taarifa, tulielezwa kutokana na utoroshaji Arusha na Kilimanjaro kuna njia za panya zaidi ya 400, hivyo Watanzania tunakuwa wa mwisho kunufaika. Wa kwanza ni Marekani na wanufaikaji wa pili ni Afrika Kusini.

"Wengine ni Wakenya, sisi ni wa mwisho sababu kuna njia nyingi za panya, Kenya imeendelea kwa sababu ya madini, kwa sababu ya utoroshaji wa madini yetu.

Tunadhibitije hizi njia? Naomba utupe maelezo," mbunge huyo alisema.Katika mjadala huo, Mbunge wa Viti Maalum, Neema Mgaya (CCM), alisema ukuta wa Mirerani mkoani Manyara umeweza kuokoa madini ambayo yalikuwa yakitoroshwa kwenda nje ya nchi.

"Nimpongeze Rais na Mkuu wa Majeshi kwa kujenga ukuta Mirerani wenye Km 235 kwa Sh. bilioni 5.2, tumeona matunda ya ukuta huu, mapato ya tanzanite yameongezeka kutoka Sh. milioni 700 mpaka Sh. bilioni 2.3, hongera sana kwa kazi nzuri," mbunge huyo alisifu.

Mgaya aliishauri serikali kuhakikisha masoko ya madini yanafanya kazi iliyokusudiwa ili kuwasaidia wachimbaji wadogo.

"Ushauri wangu, hakikisheni masoko haya yanafanya kazi iliyokusudiwa, masoko yawasaidie wachimbaji wadogo. Endeleeni kuwatengea maeneo," alisema.

Mbunge huyo pia alihoji sababu za kukwama kwa mradi wa Liganga na Mchuchuma, akieleza kuwa mradi huo ukikamilika, utatoa ajira kwa watu 5,000 na utachangia pato la taifa kwa asilimia tatu hadi nne.

"Huu ni mradi wa kielelezo lakini miaka minne imepita kilio chetu Njombe tunataka kujua ukoje?" Mgaya alihoji.

Mbunge wa Viti Maalum, Catherine Magige (CCM), alisema wachimbaji wadogo bado wanateseka kutokana na tozo zinazotozwa na Mamlaka ya Mapato (TRA) kuwa juu licha ya Rais Dk. John Magufuli kuagiza tozo hizo ziondolewe.

"Wachimbaji wanateseka sana, tozo bado zipo juu, TRA bado wanatoza tozo kubwa, tulipitisha hapa bungeni. Waziri wa Fedha unanisikia na leo ninashika shilingi, wafanyabiashara wana mitaji midogo, lakini tozo bado zipo tu," alisema.

Mbunge wa Nyang'wale, Hussein Amar (CCM), aliitaka serikali ichukue hatua za haraka kuhakikisha wachimbaji wadogo wanapata leseni, akieleza kuwa bado kuna changamoto ya upatikanaji wa leseni hizo.

Habari Kubwa